|
Mkutano wa siku mbili wa nchi za Asia ya Kusini Mashariki kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi ulimalizika tarehe 6 mjini Jakarta. Wajumbe kutoka nchi sita za kanda hiyo kwa kauli moja waliona kuwa kuimarisha ushirikiano ni muhimu zaidi katika mapambano dhidi ya ugaidi, na ni njia pekee ya kuhakikisha usalama wa kanda hiyo.
Mkutano huo uliandaliwa kwa pamoja na serikali za Indonesia na Australia, na mawaziri wa mambo ya nje na wakuu wa vyombo vya sheria kutoka Philippines, Malaysia, Singapore na Thailand walialikwa kuhudhuria mkutano huo. Kwenye ufunguzi uliofanyika tarehe 5, waziri wa mambo ya nje wa Indonesia Bw. Hassan Wirajuda alitoa hotuba akisema, ushirikiano wa kimataifa dhidi ya ugaidi ni njia muhimu katika shughuli za kupambana na ugaidi. Alisema ugaidi sio tu unawaathiri vibaya raia wasio na hatia, kuvuruga utulivu wa jamii, vile vile unaleta msukosuko wa kisiasa na hata unaharibu uchumi. Tishio la ugaidi haliwezi kuondolewa kwa juhudi za nchi moja tu, bali ni kwa ushirikiano na nchi jirani.
Hotuba ya waziri huyo imezungumzia mada ya mkutano huo. Wachambuzi wanaona kuwa mkutano huo ulifanyika katika hali ambayo nchi hizo zinakabiliwa na tishio kubwa la ugaidi. Tokea mwaka 2000, kundi la kigaidi la Indonesia, "Jemaah Islamiah", lilifanya mashambulizi mfululizo ya kigaidi ikiwa ni pamoja na milipuko ya kisiwa cha Bali na hoteli ya JW Marriot, ambayo yalisababisha watu mia kadhaa kupoteza maisha.
Mkutano umefanikiwa katika mambo matatu. Kwanza, mkutano huo ulifafanua kwa kina hali ilivyo ya makundi ya kigaidi na tishio lilivyo katika sehemu ya Asia ya Kusini na Mashariki, na uliandaa namna ya kupambana na magaidi katika siku za usoni.
Pili, Wajumbe wa nchi sita walioshiriki kwenye mkutano huo wameufanya ushirikiano katika mapambano dhidi ya ugaidi kuwa hatua halisi, tokea namna ya kushirikiana katika utekelezaji wa sheria, kupashana habari na kufanya ushirikiano kati ya vyombo vya sheria. Kwenye mkutano huo waziri wa mambo ya nje wa Indonesia Bw. Hassan Wirajuda alisema, mwaka 2004 Indonesia na Australia zilifanya mkutano wa kupambana na ugaidi katika kisiwa cha Bali, baadaye nchi wanachama wa Umoja wa Asia ya Kusini Mashariki zilishirikiana na Australia katika kutekeleza sheria, kufanya doria, kutunga sheria na kuandaa wataalamu katika shughuli za kupambana na ugaidi. Lakini katika miaka miwili ya karibuni magaidi wamekuwa na ujanja mwingi, kwa hiyo ushirikiano ni lazima uimarishwe zaidi ili kuzuia magaidi wasiweze kupata silaha kali na kufanya mashambulizi ya kusababisha vifo vya raia wengi.
Tatu, mkutano huo ulijadili namna ya kushirikiana katika mapambano dhidi ya shughuli za kimataifa za ugaidi na magendo ya silaha. Kwenye mkutano huo waziri wa mambo ya nje wa Australia Bw. Alexander Downer alisema ingawa makundi mawili ya kigaidi ya "Jemaah Islamiah" na "Abu Sayyaf" yalidhoofishwa vibaya katika miaka ya karibuni, lakini bado yanaendelea kuwaandikisha wanachama wapya na kuendelea kuzusha matukio. Kwa hiyo haifai ushirikiano wa kimataifa dhidi ya ugaidi kuwa ni mawasiliano ya habari na utekelezaji wa sheria tu, bali ni lazima pia ushirikiano huo uimarishwe kwa kina zaidi.
Idhaa ya kiswahili 2007-03-07
|