Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-08 15:13:11    
Kwa heri makazi ya muda!

cri

Katika miaka mingi iliyopita, mkoa wa Liaoning wa China ulikuwa unajulikana kwa kuwa na viwanda vingi. Ili kuwapa wafanyakazi makazi, nyumba nyingi za muda zilijengwa mkoani humo. Hivi sasa nyumba hizo zimeharibika na hazifai kuwa makazi ya watu, lakini baadhi ya nyumba hizo bado zinatumiwa na watu, kwa sababu ukarabati wa makazi hayo unahitaji fedha nyingi sana. Tangu mwaka 2005, serikali ya mkoa wa Liaoning ilianza kutilia mkazo kubomoa nyumba hizo mbovu na kuwatafutia wakazi wa huko nyumba mpya. Hatua hiyo imeboresha maisha ya maelfu ya familia za huko.

"Unajua kwa mara ya kwanza nilipoona nyumba hii, nilitokwa na machozi, sikutarajia kama ningeweza kuishi kwenye nyumba nzuri namna hii. Nikalia kutokana na furaha kubwa. Mtoto wangu alisema, mama usilie, kwa nini unalia? Nilimwambia sikutarajia kama ningeweza kuishi kwenye nyumba za ghorofa, sasa sina masikitiko mengine."

Mama huyo mliyemsikia anaitwa Li Zhenchun, ni mkazi wa mji wa Fushun, mkoani Liaoning. Hivi karibuni alihamia kwenye nyumba mpya za ghorofa kutoka kwenye nyumba za muda zilizochakaa. Mama Li ni mmoja kati ya watu walionufaika na mradi wa kukarabati makazi ya muda ya mkoa wa Liaoning. Katika nyumba za muda alikoishi mama huyo zilikuwa na hali mbaya, ambazo paa la nyumba lilifunikwa kwa vitambaa gandamizo vya lami, kuta zilikuwa na nyufa, na hakukuwa na choo.

Katika mkoa wa Liaoning, kuna watu wengi kama mama Li ambao waliwahi kuishi kwa muda mrefu kwenye nyumba za muda. Kwa mfano mjini Fushun, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2004, kulikuwa na mitaa zaidi ya 10 ya nyumba za muda yenye eneo la mita za mraba elfu 50 na familia elfu 70. Kwenye mitaa ya eneo hilo iliyokuwa imejengwa kwa miaka kati ya 50 na 60, kuna nyumba nyingi za hali duni zilizopangwa kwa karibu sana. Katika kipindi kirefu, serikali katika ngazi mbalimbali mkoani Liaoning zimekuwa zikitilia maanani ukarabati wa mitaa ya nyumba za muda, ambapo makazi ya muda yamebomolewa na wakazi wa huko kuhamishiwa kwenye nyumba mpya. Lakini baadhi ya makazi ya muda yako mbali sana na katikati ya miji, ambapo kuna wakazi wengi sana, kwa hiyo inabidi kutumia fedha nyingi katika shughuli za kuboresha makazi kwenye mitaa hiyo. Ndiyo maana suala hilo halikupata ufumbuzi muafaka hadi kufikia mwaka 2005, ambapo baada ya maandalizi ya muda mrefu, serikali ya mkoa wa Liaoning ilianza kutilia mkazo kukarabati makazi yote ya muda yaliyobaki.

Kiongozi wa mkoa huo Bw. Li Keqiang alisema  "Wakazi wengi wa mitaa ya nyumba za muda ni wachimba migodi waliostaafu, ambao waliwahi kutoa mchango kwa ujenzi wa taifa. Hivi sasa tunawaandalia makazi ya msingi, ili watu wengi zaidi wanufaike na maendeleo ya mkoa wetu."

Utekelezaji wa mradi wa kukarabati makazi ya muda ulikuwa na matatizo mengi, hata hivyo serikali ya mkoa wa Liaoning haikupuuza imani ya watu, ikafanikiwa kukusanya Yuan bilioni 3 zitumike kwa ajili ya mradi huo. Mitaji mingine ya Yuan zaidi ya bilioni 10 pia ilipatikana kutokana na serikali za mkoa na miji kutenga fedha, mikopo ya benki, na kusamehe kodi.

Mwanzoni mwa mwaka 2005 nyumba za muda za mji wa Fushun zilitangulia kubomolewa, huu ulikuwa ni mtaa wa kwanza kubomolewa katika mradi wa kukarabati makazi ya muda yenye eneo la mita za mraba elfu 50 mkoani Liaoning. Baada ya ujenzi wa miezi 7, nyumba mpya za kwanza zilikamilika, na wakazi waliaga nyumba za muda na kuhamia kwenye nyumba mpya za ghorofa zenye zana mbalimbali.

Mzee Yuan Huaxing ni mfanyakazi mstaafu aliyekuwa anafanya kazi mgodini, alisema hili ni jambo ambalo watu waliokuwa wanaishi kwenye nyumba za muda walikuwa wanalitarajia. Alisema "Siku nilipohamia kwenye nyumba mpya, mtoto wangu alinunua fataki, mkwe wangu na watoto wangu wawili waliwasha fataki kwa pamoja. Wakati huo huo nilifurahi sana kiasi kwamba nikatokwa na machozi. Nafurahi kuona serikali inachukua hatua za kuwapa wazee mazingira ya kuishi kwa raha mustarehe."

Mbali na mji wa Fushun, katika miji mingine ya mkoa wa Liaoning kama vile Shenyang, Dandong, Yingkou na Benxi, pilika pilika nyingi za uhamiaji zinaonekana hapa na pale.

Kwenye mtaa mpya wa makazi uliojengwa kwa ajili ya watu walioishi katika nyumba za muda mjini Shenyang, pia ilijengwa maktaba, chumba cha mchezo na kituo cha ajira. Kwenye mtaa mmoja wa makazi ambao ukarabati wake umekamilika, wazee walikuwa wakifanya matembezi, na watoto wakicheza kwenye mazingira safi.

Mtaa wa Beicaijie ni mtaa mkubwa kuliko mingine miongoni mwa mitaa ya makazi ya muda mjini Benxi iliofanyiwa ukarabati. Katika mtaa huo ukarabati wake umekamilika, mkazi Zhao Guirong na familia yake walikuwa wanatizama televisheni, huku wakipika chakula na kupiga gumzo, kila mmoja alionekana na furaha kubwa ya kuishi kwenye nyumba mpya.

Mama Zhao Guirong alisema "Binti, mwana na mkwe wangu wote wamekuja, tunapika maandazi kwa pamoja tukisherehekea kuhamia kwenye nyumba mpya."

Mume wa mama Zhao alisema"Nyumba ya zamani ilikuwa ndogo, nilisikia baridi kukaa katika nyumba hiyo, na mazingira ya karibu yalikuwa si mazuri. Kama mvua ikinyesha maji yalikuwa yanaingia ndani. Nyumba ya ghorofa ya sasa ni nzuri sana."

Mwaka 2005 katika miji 11 ya mkoa wa Liaoning, familia zaidi ya laki moja zilizoishi kwenye makazi ya muda zilihamia kwenye nyumba mpya. Na idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia familia zaidi ya laki 1 na elfu 50 mwaka 2006.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-08