|
Tarehe 8 Machi, siku ya wanawake duniani, wanawake wa kila pembe duniani wanafanya shughuli mbalimbali kusherehekea siku hiyo. Lakini kutokana na kukabiliana na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Israel na nchi za magharibi, wanawake wa Palestina wanaoishi katika ukingo wa magharibi wa mto Jordan, wanakumbwa na hali ngumu sana. Hata hivyo wanawake hao hawakuwa wanyonge mbele ya uchungu bali wanajitahidi kujiendeleza na kustawisha maisha yao.
Katika kituo cha ukaguzi cha jeshi la Israel kilichopo kusini mwa mji wa Nablus kwenye ukingo wa magharibi wa Mto Jordan, kila siku Wapalestina wakiwa pamoja na wanawake na watoto wanasimama kwenye msururu mrefu wakisubiri kukaguliwa. Kutokana na ukaguzi wa makini sana mtu akipita kwenye kituo hicho huwa anasubiri dakika kumi kadha na hata masaa kadha kabla ya kuvuka kituo hicho, na baadhi ya wajawazito walipaswa kujifungua kituoni, na wagonjwa wengi walichelewa matibabu yao.
Bi. Shatha Odeh wa kituo cha kutoa ushauri na misaada ya kisheria katika ukingo wa maghaaribi wa mto Jordan alisema, katika miaka ya karibuni hapakosi wanawake waliojifungua kituoni. Alisema,
"Katika muda wa miaka minne tu tokea mwaka 2002 hadi sasa, jumla ya wanawake 69 walijifungua katika kituo hicho, na watoto 36 waliozaliwa walikufa. Wajawazito wengi walijifungua kabla ya wakati na kuvuja damu nyingi bila msaada wowote wa tiba."
Licha ya usumbufu wa kituo cha ukaguzi wa jeshi la Israel, wanawake wa Palestina wanakabiliwa na tishio. Katika mji wa Nablus, jeshi la Israel limemaliza operesheni hivi punde, mkazi Raed Aghber aliwaambia waandishi wa habari akisema, wanawake na watoto ni waathirika wakubwa zaidi katika operesheni hiyo.
"Askari wa Israel waliwafungia watu vyumbani, siku mbili au tatu bila chakula wala maji wakiwa na hofu."
Bi. Shatha Odeh aliongeza kuwa, kwa sababu wanaume wengi wa Palestina walikamatwa katika migogoro kati ya Palestina na Israel, wanawake wanapaswa kubeba jukumu la kulisha familia zao.
Ingawa wanawake wa Palestina wanaoishi katika hali hiyo ngumu lakini hawakuwa wanyonge, bali wanajitahidi kujiendeleza na kustawisha maisha yao kadiri wawezavyo.
Katika shule binafsi mjini Hebron kwenye ukingo wa magharibi wa Mto wa Jordan. Mwalimu wa kompyuta mwenye umri wa miaka 24 Bi. Zuhour Zaitoon anawafundisha wanafunzi wa kike huku akiandika kwenye ubao. Mwanafunzi mwenye umri wa miaka 20 Jalilah Abu Seif alisema,
"Nia yangu ya kusomea elimu ya kompyuta ni kutaka kujipatia kazi nzuri, sitaki kukaa nyumbani tu, nataka kujikimu."
Mkuu wa shule hiyo Bw. Yasser O. Khatib alieleza,
"Miaka 20 iliyopita, wanafunzi wa kike walikuwa 20% ya wanafunzi wote, lakini sasa wanafunzi hao wamekuwa na 80%. Ukweli ni kwamba tunapokea wanafunzi wa kike zaidi ya 20 kila mwezi. Wanafunzi hao licha ya kufundishwa elimu ya kompyuta, vile vile wanafundishwa uhasibu na ususi wa nywele."
Hivi sasa wanawake wa Palestina wanazidi kubeba majukumu ya wanaume na kuwa watu muhimu katika jamii. Bw. Khatib alisema,
"Utakuta wanawake wengi katika vyuo vikuu na jumuyia za umma."
Licha ya kuwa, wanawake wa Palestina wanajitahidi kujiimarisha, nao pia wanajistawisha maisha yao. Meneja wa klabu ya kuimarisha afya Bi. Rula Sharawi alisema,
Klabu yangu ilianzishwa mwaka 1996, wakati huo watu waliona ajabu, na waliokuja kwenye klabu yangu walikuwa wachache sana. Lakini sasa kufanya mazoezi hapa kwenye klabu imekuwa ni sehemu muhimu ya maisha yao. Niliwaambia, wasijizamishe kufikiria uchungu, muda wa binadamu humu duniani ni mfupi, ni lazima tujitahidi kuishi vizuri kadiri tuwezavyo."
Idhaa ya kiswahili 2007-03-08
|