Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-09 20:07:03    
Kikundi cha kwanza cha vijana wanaojitolea wa China waliotumwa na serikali ya China kwenda kutoa huduma nchini Zimbabwe

cri

Tarehe 24 Januari huko Harare, mji mkuu wa Zimbabwe ilifanyika sherehe moja ya kuwalaki vijana 15 wanaojitolea kutoka China, hiki ni kikundi cha kwanza cha vijana wanaojitolea wa China waliotumwa na serikali ya China kwenda kutoa huduma nchini Zimbabwe. Katika kipindi cha mwaka mmoja, vijana hao watafanya shughuli zinazohusiana na mifugo, kilimo, elimu na matibabu nchini Zimbabwe.

Vijana hao walihudhuria sherehe hiyo wakiwa wamevaa suti nyeusi zenye nembo ya vijana wanaojitolea wa China. Kijana mmoja aliwavutia sana watu, yeye anaitwa Xu Benyu ambaye aliwahi kufanya kazi ya ualimu kwa muda mrefu katika sehemu ya milimani yenye umaskini iliyopo magharibi mwa China. Kijana huyo alisema:

"Kujitolea kwenda ng'ambo kuwasaidia wengine ni nia niliyoweka mwaka 2002. Niliwahi kufanya kazi ya ualimu mkoani Guizhou na nilisikikitika kuwaaga watoto wa huko, lakini kila mtu ana ndoto ambayo anatakiwa kuitimiza wakati wa ujana. Nikishirikiana na kijana mwingine anayejitolea, tutafundisha lugha ya Kichina katika chuo cha ualimu cha Harare, nitafanya kila niwezalo katika kazi hii."

Mwezi Novemba mwaka 2006, rais Hu Jintao wa China akifungua mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika hapa Beijing, alitoa ahadi kuwa China itatuma vijana 300 wanaojitolea barani Afrika katika miaka mitatu ijayo. Safari ya vijana hao nchini Zimbabwe ni mradi wa kwanza kutelekezwa baada ya China kutoa ahadi hiyo. Vijana hao wana umri wa wastani wa miaka 29, baadhi yao wamehitimu masomo ya chuo kikuu katika siku za karibuni, mmoja kati yao ana shahada ya udaktari, vijana sita wana shahada ya pili na wengine pia ni wahitimu wa vyuo vikuu. Katika mwaka mmoja ujao vijana hao watapelekwa kwenye vyuo vikuu na shule za mafunzo ya kazi katika miji mitano nchini Zimbabwe, kufanya shughuli zinazohusiana na mifugo, utengenezaji wa mazao ya kilimo, mafunzo ya lugha ya Kichina, mafunzo ya ujuzi wa kompyuta, mafunzo ya michezo na matibabu ya Kichina.

Kwenye sherehe ya kuwakaribisha vijana hao wa China, waziri wa vijana na ajira wa Zimbabwe Bw. Ambrose Mutinhiri alieleza kuwa, hatua ya serikali ya China kutuma vijana wanaojitolea nchini Zimbabwe, itaimarisha urafiki kati ya nchi hizo mbili na kukuza uhusiano wa nchi hizo mbili. Alisema:

"Serikali ya Zimbabwe inawakaribisha vijana wanaojitolea kutoka China. Idara mbalimbali za serikali ya Zimbabwe zitawasaidia vijana hao wa China ili wafanye shughuli zao bila matatizo."

Waziri Mutinhiri aliongeza kuwa, Zimbabwe inatumai kuwa China itatuma watu wengi zaidi wanaojitolea kutoa huduma katika shughuli za upashanaji habari, utamaduni, utalii na matibabu ya jadi ya Kichina. Alisema serikali ya Zimbabwe inaamini kuwa, vijana hao wa China na shughuli watakaofanya nchini Zimbabwe zitasaidia kuongeza maelewano, maingiliano na ushirikiano kati ya watu wa nchi hizo mbili.

Balozi wa China nchini Zimbabwe Bw. Yuan Nansheng alisema, "China na Zimbabwe zina urafiki mkubwa kwa miaka mingi, China siku zote inaichukulia Zimbabwe kuwa ni rafiki mkubwa anayeaminika. Serikali ya China pia imekuwa inatoa misaada kadiri iwezavyo kwa serikali ya Zimbabwe na wananchi wake. Serikali ya China inaamini kuwa vijana wanaojitolea wa China watachangia ujenzi wa Zimbabwe katika sekta mbalimbali."

Kujenga urafiki, kusaidiana na kupata maendeleo ya pamoja ni lengo la vijana wanaojitolea wa China, ambao wanataka kujenga daraja la kufanya maingiliano ya kiutamaduni na kihisia kati ya watu wa China na Afrika.

Naibu katibu mkuu wa shirikisho la vijana wanaojitolea la China Bwana Guo Ping alisema, kutokana na uungaji mkono wa wizara ya mambo ya nje na wizara ya biashara ya China, mwaka 2002 shirikisho hilo lilizindua rasmi mpango wa kutuma vijana wanaojitolea wa China kwenda kutoa huduma katika nchi za nje, hadi hivi sasa shirikisho hilo limeshawatuma vijana 200 wanaojitolea kutoa huduma katika nchi za nje.

Habari nyingine zinasema kuwa, vijana wengine 10 wanaojitolea wa China kutoka mji wa Guangzhou, kusini mwa China tarehe 26 Januari mwaka huu walifunga safari kwenda visiwani Shelisheli kutoa huduma za matibabu, elimu ya muziki na lugha ya Kichina.