Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-12 16:11:59    
Matembezi ya kuangalia vyungu katika mji wa Jieshou, mkoani Anhui

cri

Ufundi wa jadi wa utengenezaji wa vyungu wa mji wa Jieshou, mkoa wa Anhui ulioko sehemu ya kati mwa China ulianza zaidi ya miaka elfu moja iliyopita. Vyungu hivyo vinafinyangwa kwa udongo wa mfinyanzi, kupakwa rangi na kuchomwa moto katika tanuri. Vyungu hivyo vya ufinyanzi vilivyotengenezwa kwa ufundi wa jadi vimetunzwa katika jumba la sanaa ya uchoraji la China, jumba la makumbusho la taifa la China na jumba la makumbusho la Victoria nchini Uingereza. Lakini ni kwanini vyungu vilivyotengenezwa mjini Jieshou vinapendwa sana na watu?

Historia ya utengenezaji wa vyungu vilivyopakwa rangi ilianza katika kipindi cha enzi za Sui na Tang za China, kiasi cha miaka 1,100 iliyopita. Vyungu vilivyotengenezwa na mji wa Jieshou vimetengenezwa vizuri sana, michoro iliyoko kwenye vyungu ilichongwa au kukatwa kwa kisu, kisha inatiwa rangi mbalimbali na kuchomwa kwa moto ndani ya tanuri. Vyungu na vyombo vingine vya ufinyanzi vinavyopendeza zaidi vya mji wa Jieshou ni vile vyenye picha ya mtu aliyepanda farasi na kushika kwa mkono upanga wenye mpini mrefu, ambayo ilisanifiwa kwa mujibu wa wahusika katika michezo ya drama ya jadi nchini China.

"Wasikilizaji wapendwa, mnayosikia sasa hivi ni baadhi ya maneno ya mhusika wa mchezo wa uimbaji wa jadi wa mkoa fulani nchini China, yaliyosemwa na mzee Lu Shanyi mwenye umri wa miaka 87, ambaye ni mwanzilishi wa ufundi wa ukataji wa michoro kwenye vyungu na vyombo vya ufinyanzi vya mji wa Jieshou vinavyojulikana kama michero ya "upanga, farasi na mtu". Kwa kawaida michoro ilivyokatwa kwa kisu kwenye vyombo vya ufinyanzi vya jadi vya mji wa Jieshou ni picha yenye mtu aliyepanda farasi akishika mjeledi mkononi, lakini vyombo vya aina ya "Dao, Ma, Ren", ni vyenye michoro ya "upanga", "farasi" na "mtu" kwa pamoja. Mzee Lu Shanyi anachonga michoro hiyo kwenye vyungu, chupa za kuwekea maua, mitungi na magudulia, na kutia rangi za aina tatu nyekundu, nyeupe na kijani, halafu kuvichoma kwa moto ndani ya tanuri.

"Michoro iliyoko kwenye vyombo vya ufinyanzi nilivyotengeneza, ni michoro iliyochongwa kwa kisu, hata vyombo vyenyewe vikivunjika, rangi zilizoko juu yake hazitoki, hapo zamani picha za rangi zilizoko kwenye vyombo vya ufinyanzi zilipauka na kufifia baada ya kupita miaka mingi, lakini rangi zilizotiwa kwenye michoro iliyochongwa hazitoki.

Vyombo vya ufinyanzi vyenye michora ya rangi ya "upanga, farasi na mtu" vinapendeza zaidi. Inasemekana kuwa vyombo vilivyochongwa nakshi na michoro na kuchomwa kwa ufundi mkubwa, vikitiwa maji na kuwekwa katika mwangaza wa jua, watu na wanyama walivyochongwa kwenye vyombo hivyo wanaonekana ni wa hai. Habari zinasema vyombo vya ufinyanzi vilivyotengenezwa na mzee Lu Shanyi vimetunzwa katika majumba ya makumbusho ya zaidi ya nchi kumi, au vilinunuliwa na watu na kutunzwa majumbani mwao. Mzee Lu Shanyi alipozungumzia oda za wageni wa nchi za nje, alisema kwa furaha,

"Wageni wengi wanapenda vyombo vya ufinyanzi vya aina hiyo, wageni wa nchi kadhaa ikiwemo Poland walikuja kwangu kuagiza bidhaa, licha ya hapo hakuna sehemu nyingine ya China inayozalisha vyombo vya ufinyanzi vya aina hiyo, hata katika dunia nzima hakuna sehemu inayozalisha vyombo vya aina hiyo."

Wasikilizaji wapendwa, katika historia vyombo vingi vya ufinyanzi vya mji wa Jieshou vinasafirishwa katika sehemu mbalimbali za nchini China kwa kupitia mfereji mkubwa wa karibu, ambavyo vilitolewa kwa maofisa na matajiri wa wakati ule vikiwa vitu vya anasa. Katika karne ya 19, vijiji 13 vilivyoko karibu na mji wa Jieshou vilianza kutengeneza vyombo vya ufinyanzi, ambavyo vilijulikana sana kama matanuri maarufu 13. Hivi leo, matanuri hayo 13 yote yametoweka, lakini majina ya vijiji hivyo 13 yote yana neno "tanuri", tena matanuri madogo madogo ya binafsi yanaonekana katika sehemu nyingi za huko.

Kwa watalii, kuweza kushiriki kwenye utengenezaji wa vyombo vya ufinyanzi ni furaha kubwa. Utengenezaji wa vyombo vya ufinyanzi vya rangi kwanza kabisa unahitaji kuchagua udongo unaofaa, udongo huo unakandwa kwa mara nyingi sana hadi kiwango cha kuweza kutengenezwa kuwa vitu vyenye maumbo mbalimbali. Baada ya hapo waalimu watawafundisha watalii kupaka tope la kupamba vyombo vya ufinyanzi, kwani kuchora au kuchonga michoro kwenye tope lililokauka kwenye sehemu ya nje ya vyombo vya ufinyanzi ni kazi rahisi kidogo. Vyombo vilivyokwisha chongwa michoro sehemu ya nje, vinachomwa kwa moto ndani ya tanuri; vyombo hivyo huchomwa moto mara ya pili baada ya kupakwa kauri ya rangi. Kauri iliyoko kwenye sehemu ya nje ya vyombo vya kauri ni kama kioo, vyombo vya ufinyanzi vilivyopakwa kauri ya rangi na kuchomwa moto, ni kama vimevaa nguo laini isiyo na mikunjo ya rangi nyeupe au rangi nyingi mbalimbali. Baada ya kutiwa kauri ya rangi na kuchomwa moto katika tanuri, ndipo vyombo vya ufinyanzi vinakuwa vimekamilika.

Utengenezaji wa vyombo vya ufinyanzi vya mji wa Jieshou unaunganisha ufundi wa sanaa ya jadi ya ukataji karatasi na sanaa ya uchongaji mbao. Hivyo wawe wasanii wa nchini na wa nchi za nje au ni watalii wa kawaida, wote wanasifu sana sanaa ya kipekee ya vyombo vya ufinyanzi vyenye michoro ya rangi. Bingwa mfinyanzi wa China Bibi Yan Yumin alisema,

"Vyombo vya ufinyanzi vya Jieshou ni maarufu sana, vinasafirishwa kwa baadhi ya nchi za Ulaya mashariki zikiwemo Poland, Czech, Slovakia na Hungary, watu wa nchi hizo wanapenda sana rangi za vyombo vya ufinyanzi vilivyotengenezwa katika mji wa Jieshou."

Mwezi Desemba mwaka 2005, ufundi wa kutengeneza vyombo vya ufinyanzi wa mji wa Jieshou uliidhinishwa kuwa moja kundi la kwanza ya mabaki ya kiutamaduni yasiyo ya vitu ya ngazi ya taifa yanayohifadhiwa, vyombo hivyo vya Jieshou, ambavyo ni vitu vya sanaa ya kiutamaduni vimeanza kuzingatiwa na kufuatiliwa. Sasa ufundi wa uchongaji michoro ya "upanga", "farasi" na "mtu" unafundishwa kwa wanafunzi. Mke wa mtoto wa mzee Lu Shanyi Zhang Qianwen ni mmoja wa wanafunzi kijana zaidi wanaojifunza ufundi wa kuchonga michoro ya "upanga", "farasi" na "mtu", alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa kwa hatua ijayo, wasanii wa vyombo vya ufinyanzi watabuni michoro mipya itakayochongwa kwa vyombo vya ufinyanzi kutokana na kitabu kikubwa cha hadithi cha kale cha nchini China kinachojulikana kama "Hadithi za Nchi Tatu" ili kuunganisha vizuri ufundi wa utengenezaji wa vyombo vya ufinyanzi vya jieshou na utamaduni wa jamii wa China. Alisema,

"Mabingwa wa vyombo vya ufinyanzi wanachonga michoro kwenye vyombo vya ufinyanzi kwa mujibu wa wahusika wa michezo ya uimbaji, jambo ambalo linafanya watu kuona kuwa hiyo ni sanaa inaweza kuonesha vitu vya jadi vya China, na kuongeza ufahamu wa nchi za nje kuhusu utamaduni wa China."

Idhaa ya kiswahili 2007-03-12