Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-13 16:22:23    
Barua 0311

cri

Msikilizaji wetu Hamisi Hassan wa shule ya sekondari ya Mtakatifu Carol sanduku la Barua 21 Sengerema Mwanza Tanzania, anaanza barua yake kwa kusema, Idhaa ya Kiswahili ya CRI ni idhaa ambayo urushaji wake wa matangazo unaridhisha, nchini Tanzania wanaifurahia sana kwa mchango wake katika kukieneza Kiswahili kimataifa. Na Inawapa faraja sana kuwasikia wachina wakiongoza matangazo kwa lugha ya Kiswahili.

Bwana Hassan anaendelea kusema, kutoka na matangazo ya Idhaa ya Kiswahili kuwa ya kuridhisha hivyo yanapaswa kuboreshwa zaidi, na maoni yake ni kuwa uboreshwaji huo unaweza kufanywa kwa kurusha matangazo yake kupitia vituo vya radio vikubwa na maarufu katika Afrika mashariki na ukanda wa maziwa makuu, hii itawawezesha watu wengi wa Afrika ya mashariki na eneo la maziwa makuu kupata matangazo yake vizuri na kwa uhakika zaidi. Anasema kwa kutumia vituo hivi vya radio kutaifanya idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa ijulikane zaidi kama zilivyo idhaa nyingine za Kiswahili, na bali watu wengi watanufauka kwa kujua mambo mengi yanayohusu China.

Pili, bwana Hassan anaomba kuanzishwa vituo vidogo katika nchi zinazozungumza Kiswahili kama vile Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi ili iweze kuwa rahisi kwa taarifa zinazohusu mataifa hayo kutangazwa na kusikika kote Afrika ya Mashariki na kati, hii itasaidia kuongeza hamasa ya usikilizaji kwa watu wengi zaidi.

Tatu, matangazo yanayohusu China yasiwe mengi sana kwani itawafanya wasikilizaji wengi kuchoka, lakini bwana Hassan anasema hana maana kuwa matangazo yanayohusu China yasitangazwe, ila maana yake ni kuwa habari zinazohusu nchi mbalimbali hasa bara la Afrika ziongezwe, na pia kianzishwe kipindi cha habari za magezetini.

Nne, Msikilizaji wetu anasema, kipindi cha Jifunze Kichina kiboreshwe zaidi kwani kimepewa muda mfupi ambao hautoshi kwa msikilizaji kupata misimiati mingi kwa wakati. Pia uendeshwaji wa kipindi usiende haraka ili wasikilizaji waweze kwenda sambamba, na bwana Hassan anasema anapenda sana siku moja aweze kuongea kichina. Anamalizia barua yake kwa kusema, "Idhaa ya Kiswahili ya CRI yaangaza kote duniani"

Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kimalija wa sanduku la posta 1067 Kahama Shinyanga Tanzania, anasema ni matumaini yake kuwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio china Kimataifa ni wazima wakiendelea kurusha matangazo kutoka mjini Beijing, kwa upande wake ni mzima akiendelea kuitegea sikio Radio China Kimataifa.

Anasema anapenda kutumia fursa hii kuipongeza Jamhuri ya watu wa China kwa kuadhimisha miaka 57 tangu kuasisiwa kwake, na anaipongeza zaidi kwa kuendelea na uhusiano na nchi za Afrika na ulimwengu kwa ujumla. Vilevile anawapongeza wasikilizaji wenzake Ras Franz Manko Ngogo wa Tarime, Mara nchini Tanzania na Mutanda Ayub Sharif wa Bungoma nchini Kenya kwa kupata ushindi wa zawadi maalum wa kuitembelea China katika maadhimisho ya miaka 65 tangu kuanzishwa kwa radio China Kimataifa.

Pia anawaomba wasikilizaji wenzake wote popote walipo ambao hawakubahatika kuchaguliwa katika ushindi wa nafasi maalum wasife moyo, kwani radio China kimataifa inaendelea kuwaletea chemsha bongo kila mwaka. Mwisho anatutakia wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa kazi njema na yenye mafanikio mema katika mwaka huu mpya wa 2007, na urafiki kati yake na Radio China Kimataifa uendelee.

Bwana Noel E. Mshauri wa Seminari ya Mtakatifu Patrick Dun'gunyi, S.L.P 275 Singida nchini Tanzania, anasema ni matumaini yake kuwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya radio China Kimataifa wanaendelea vyema na kazi na kuboresha matangazo, yeye ni mzima akiendelea na majukumu yake ya kila siku. Anasema anapenda kutoa pongezi zake nyingi na hongera kwa mzee aliyesimama kidete (yaani CRI Kutimiza 65) akiendelea kukamilisha shabaha aliyojiwekea, Hongera sana.

Lakini msikilizaji wetu anapenda kutujulisha kuwa, ingawa hana klabu ya wasikilizaji huko aliko, lakini alifanya sherehe pamoja na CRI ya kuadhimisha miaka minane (8) ya uanachama hai wa CRI pamoja na matatizo ya hapa na pale ya usikivu. Anasema yeye alipenda asherekee miaka yake nane ya uanachama wa CRI akiwa nchini China, lakini bahati mbaya hakubahatika. Pia radio anayotumia sasa si nzuri sana kwa usikivu hivyo anaomba kufahamishwa gharama ya radio hapa Beijing ili atume pesa za manunuzi na CRI imtumie radio hiyo.

Bwana Mshauri pia ametutumia shairi linalopongeza Radio China kimataifa kuadhimisha miaka 65 tangu ianzishwe, shairi hilo linasema

1. Ilianza ka' utani tena chini ya mapango

Ni kwa moyo kujitoa. Ka'nza huyo mjapan

Askari pinga vita, kutangaza hili lile

Mradi kufahamisha, yale yote natukia

2. Jikongoja kama jua, asubuhi kuchomoza

Shika bango kaza buti, na neema ikashamiri

Fika hatua murua, hata jina badilisha

Asili ikawa China, Radio Kimataifa

3. Yote hayo yalitokea, miaka ile tano ziro,

Enzi hizo tu viziwi, jui hili wala lile

Fika mwaka tisa nane, natoka usingizini

Sasa mengi yameshajiri, taifa zaidi kukua.

4. Muda zaidi songa mbele, maboresho enda juu

waanzisha mashindano, wasikilizaji tuwe gado

Tufahamu china Nzima, vipengele mbalimbali

Pata nafasi muhimu, wenda tembelea China

5. Mbili ziro ziro moja, waanzisha matangazo,

Kwa nia ya mtandao, yaani China Online

Ukifungua utaona habari, nyingi kedekede

Anzia za pale China, pia za kimataifa

6. Ilipofika mbili sita, mwezi machi mbili tisa

Pia fungua kituo tisa moja doti tisa

Kituo cha efu emu, Nairobi pale Kenya

Huduma imesogezwa, Afrika mashariki

7. Nami nawapongeza, kwao wenu ushirika

miaka nane mpo nami, taratibu tunasonga

Tudumishe ushirika, mimi nanyi siku zote

Munkali ukinipanda, kimbilio ni Cri

Msikilizaji wetu Ali Hamisi Kimami wa Kenya, ametuandikia barua pepe akisema anapenda kutumia fursa hii kutoa shukurani zake za dhati kwa zawadi kadha wa kadha tulizomtumia ikiwa ni pamoja na picha mbili za ndege, kalenda mbili nzuri za mwaka huu ambapo moja amempa rafiki yake, na hivi karibuni pia alipokea fulana moja nzuri ikiwa na maandishi ya Radio China kimataifa, ikiwa ni takrima kutokana na kuwa katika nafasi ya tatu katika chemshabongo ya mwaka jana. Anasema ama kweli, mgaagaa na upwa, hali wali mkavu!.

Anasema kwa hakika amejawa na furaha kubwa, hasa anapoona kuwa Radio China kimataifa inawajali wasikilizaji wake. Ni matumaini yake kuwa siku moja ataweza kupata nafasi ya mshindi maalum, ili aweze kuitembelea China. Kwa hiyo sasa anafanya juhudi kuhusu Chemsha bongo ya mwaka huu iliyoanza mwishoni mwa mwaka jana. Anakamilisha barua yake kwa kuwapongeza wasikilizaji wenzake wote walioshiriki katika Chemshabongo hiyo na kupata zawadi mbalimbali.