Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-15 16:08:35    
Ufuatiliaji kwa watoto yatima wa Ukimwi

cri

Filamu inayoonesha hali halisi ya maisha ya watoto yatima wa Ukimwi ya sehemu ya Yingzhou, mji wa Fuyang mkoani Anhui, China inayoitwa "Watoto wa Yingzhou" imepata tuzo katika mashindano ya 79 ya filamu ya tuzo ya Oscar. Hii ni mara ya kwanza kwa wapigaji filamu wa China kupata tuzo katika mashindano hayo. Maofisa wa afya wa huko na mashirika ya kiraia ya utoaji msaada wa Ukimwi wamefurahia sana kupata habari hiyo, wakieleza kwa nyakati tofauti kuwa kupata tuzo kwa filamu hiyo kutawahimiza watu wengi zaidi kuwafuatilia watoto yatima wa Ukimwi.

Filamu hiyo iliyopigwa kwa ushirikiano wa China na Marekani imeonesha hali ya maisha ya watoto maskini na watoto yatima wa Ukimwi katika mji wa Fuyang, wanaoishi chini ya msaada wa shirika la msaada kwa watoto maskini wa Ukimwi la Fuyang na wanavyopitisha sikukuu na likizo. Kutokana na ukweli wa mambo, filamu hiyo inawafanya watazamaji waiamini na kuifurahia.

Mkuu wa shirika la msaada kwa watoto maskini wa Ukimwi Bi. Zhang Ying alisema, shirika hilo limewasaidia watoto maskini zaidi ya 400 wa Ukimwi katika mji wa Fuyang, linachangisha fedha kutoka kwa sekta mbalimbali za kijamii, kila mwezi linampa mtoto mmoja Yuan 400 kwa ajili ya matumizi, kuwatafutia watoto yatima wa Ukimwi familia mpya, na kueneza ujuzi wa kukinga Ukimwi na kuondoa unyenyepa kutoka kijiji kimoja hadi kingine. Bi. Zhang Ying alifahamiana na wapiga filamu alipowaongoza watoto maskini wa Ukimwi kuja Beijing kushiriki katika shughuli za watoto za likizo ya majira ya joto. Alisema:

"Mimi sielewi sana mambo ya filamu, lakini ni jambo la kufurahisha kuwaoneshea watazamaji wa duniani hali ya maisha ya watoto maskini wa Ukimwi, bila shaka kuanzia hapo watoto hao watafuatiliwa na watu wengi zaidi."

Mji wa Fuyang mkoani Anhui ni sehemu yenye idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya Ukimwi kutokana na kuwepo kwa vitendo vya kuuza damu. Mkuu wa kituo cha udhibiti wa magonjwa cha sehemu ya Yingzhou Bwana Xu Zhenghou alisema, sehemu hiyo ina watu 615 walioambukizwa virusi vya Ukimwi, na watoto yatima 36 wa Ukimwi. Sehemu hiyo imekuwa sehemu ya kielelezo cha kinga na tiba ya Ukimwi nchini China.

Bw. Xu Zhenghou alisema sehemu ya Yingzhou kila mwaka inatenga Yuan milioni moja katika kinga na tiba ya Ukimwi. Serikali kuu ya China kila mwezi inawapa watoto maskini wa Ukimwi Yuan 100. Licha ya shirika la msaada kwa watoto maskini wa Ukimwi, shirikisho la wanawake la huko pia limeanzisha nyumba ya watoto yatima wa Ukimwi, kuwatunza watoto yatima wa Ukimwi wasiokuwa na jamaa na marafiki wa kutegemea.

Bw. Xu Zhenghou alisema, sehemu hiyo inatumai kufanya mawasiliano zaidi na mikoa mingine nchini China na nchi za nje ili kutafuta njia nzuri zaidi ya kukinga na kutibu Ukimwi na kuwasaidia watoto yatima wa Ukimwi. China inakabiliwa na changamoto ya ugonjwa wa Ukimwi. Kwa mujibu wa takwimu hivi sasa nchini China kuna watu laki 6.5 wenye virusi vya Ukimwi, na watoto yatima elfu 76 kutokana na ugonjwa huo.

Siku chache zilizopita wizara ya afya ya China ilisema itaanzisha harakati za kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi, na itaimarisha harakati za kutoa upendo kwa watoto hao kwenye sehemu za makazi na familia na kupambana na unyenyepa, na kukamilisha sera za kutoa msaada kwa watoto yatima wa Ukimwi.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-15