Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-14 15:02:38    
Hali ya usalama mjini Mogadishu bado ni mbaya

cri

Tarehe 13 mashambulizi ya mabomu yalitokea mjini Mogadishu kwa lengo la kumuua rais Yusufu wa serikali ya mpito ya Somalia. Ingawa rais Yusuf aliponea chupuchupu, lakini kutokana na kuwa tukio hilo lilitokea tu baada ya bunge la Somalia kuamua kuhamisha serikali ya mpito mjini Mogadishu, watu wanazidi kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa mji huo.

Asubuhi ya siku hiyo, rais Yusuf aliondoka Baidoa ambapo serikali ya mpito ilikuwepo na kwenda Mogadishu bila kutoa taarifa. Baada ya muda mfupi ikulu iliyoko kwenye sehemu ya kusini ya Mogadishu ilishambuliwa kwa mabomu sita. Watu walioshuhudia walisema, mabomu mawili yalilipuka ndani ya ikulu, na bomu moja lililipuka kwenye nyumba iliyo jirani na ikulu na kusababisha mtoto mmoja wa kiume mwenye umri wa miaka 12 kuuawa na watu wengine watatu kujeruhiwa. Kabla ya ikulu kushambuliwa msururu wa magari ya naibu meya wa mji wa Mogadishu pia ulishambuliwa na kusababisha vifo vya watu wawili, naibu meya huyo pamoja na watu wengine wanne walijeruhiwa.

Katika siku kabla tukio hilo, bunge la Somalia liliamua kuhamisha makao ya serikali ya mpito hadi mjini Mogadishu. Kwa mujibu wa mpango, serikali ya mpito itahamia mjini Mogadishu kutoka Baidoa, na baadhi ya mawaziri wataanza kufanya kazi katika mji huo kuanzia wiki ijayo. Ni dhahiri kwamba mashambulizi hayo yaliyofanywa na vikundi vyenye silaha vya upinzani yanalenga kupinga serikali kuhamia mjini Mogadishu.

Tokea mwaka 1991 Somalia ilikuwa katika hali ya kutokuwa na utawala wa serikali. Mwaka 2004 kutokana na msaada wa jumuyia ya kimataifa serikali ya mpito ilianzishwa Nairobi, lakini serikali hiyo haina uwezo wa kuidhibiti hali ya nchi, na baada ya serikali hiyo kuingia nchini Somalia haikuweza kuingia mjini Mogadishu ambako kulikuwa kunatawaliwa na vikundi vya upinzani vyenye silaha, kwa hiyo serikali hiyo ilipaswa kufanya kazi katika mji wa Baidoa kwa miaka mingi. Katika nusu ya pili ya mwezi Desemba mwaka jana, kutokana na msaada wa jeshi la Ethiopia, jeshi la serikali ya mpito lilisambaratisha vikosi vya kundi la Mungano wa Mahakama za Kiislamu na kudhibiti baadhi ya maeneo ukiwemo mji wa Mogadishu. Hata hivyo kutokana na kuwa vikosi vilivyobaki vya upinzani vilikataa kusalimisha silaha, hali ya Mogadishu haikuwa salama toka mwanzo, na hata rais Yusufu hakuthubutu kwenda mjini Mogadishu, na serikali ya mpito haikuweza kuhamia mjini humo.

Tarehe 23 Januari Ethiopia ilitangaza kuondoa jeshi lake kutoka Somalia, hali ya usalama katika maeneo fulani ukiwemo mji wa Mogadishu ikawa mbaya. Ingawa Umoja wa Afrika umeamua kutuma jeshi lenye askari 8,000 nchini Somalia baada ya kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kujaza pengo lililoachwa na jeshi la Ethiopia, lakini kutokana na hali mbaya ya usalama na ukata, jeshi hilo hadi leo halijaundwa kikamilifu na kufika mahali linapotakiwa. Hadi kufikia tarehe 6 mwezi huu kikosi chenye askari 300 cha Uganda ikiwa ni sehemu ya jeshi hilo kilifika Mogadishu, lakini kikosi hicho kilipokuwa kwenye sherehe ya kukaribishwa kwenye uwanja wa ndege mjini Mogadishu kilishambuliwa na makombora, na huko mjini Mogadishu pia yalitokea mapambano makali ya kisilaha. Jioni ya tarehe 7 msururu wa maderaya ya kikosi cha Umoja wa Afrika ulishambuliwa na watu wasiofahamika na kusababisha vifo vya watu 9 na wengine 22 kujeruhiwa wakiwemo askari wawili wa jeshi la kulinda amani. Habari kutoka hospitali kwenye eneo la tukio hilo zilisema, tarehe 13 watu wasiopungua 42 waliuawa, wengi wao wakiwa ni watoto.

Vyombo vya habari vinasema, nia ya bunge la Somalia kuhamishia serikali ya mpito mjini Mogadishu, ni kwa ajili ya kuandaa mkutano wa maafikiano ya kitaifa utakaofanyika hivi karibuni na kutaka kuwaonesha watu wa Somalia na jumuyia ya kimataifa uwezo wake wa kutuliza hali ya Somalia, lakini hali ilivyo imedhihirisha kuwa, kuwa na nia tu peke yake hakutoshi, bali ni lazima nia iambatane na hatua za uhakika kabla ya kuweza kudhibiti hali ya Mogadishu.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-14