Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-15 16:18:33    
Utatuzi wa suala la nyuklia umekuwa ni ushirikiano mzuri kati ya Korea ya Kaskazini na Marekani

cri

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Nishati ya Atomiki duniani Bw. Mohammed El Baradei tarehe 14 alimaliza ziara yake nchini Korea ya Kaskazini, baada ya ziara hiyo alisema Korea ya Kaskazini imekubali kurudi tena kwenye shirika hilo. Katika siku hiyo Wizara ya Fedha ya Marekani iliamua kuondoa vikwazo vya fedha kwa Korea ya Kaskazini. Hali hiyo inaonesha kuwa utatuzi wa suala la silaha za nyuklia katika peninsula ya Korea umeanza kuwa ni ushirikiano mzuri kati ya pande mbili.

Kuanzia tarehe 14 Bw. Mohammed El Baradei alifanya ziara ya siku mbili nchini Korea ya Kaskazini. Kwenye mkutano na waandishi wa habari alipoeleza mafanikio ya ziara yake alisema ziara yake imefungua mlango wa kuufanya uhusiano kati ya Shirika la Nishati ya Atomiki duniani na Korea ya Kaskazini uwe wa kawaida. Korea ya Kaskazini inapenda kushirikiana vyema na Shirika hilo na kusimamisha miundombinu ya nyuklia. Bw. Baradei alisema, Korea ya Kaskazini inapenda kutekeleza ahadi zake za kuacha nyuklia, lakini ni sharti Marekani iondoe kwanza vikwazo vya fedha kwa nchi hiyo.

Katika siku hiyo, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza kumaliza ukaguzi wake uliofanywa kwa miezi 18 kuhusu akaunti ya Korea ya Kaskazini katika benki ya Macau na kusema kuwa mfumo wa mambo ya fedha wa Marekani hautakuwa tena na uhusiano wowote na benki hiyo yenye akaunti ya Korea ya Kaskazini. Taarifa hiyo inamaanisha kuwa Marekani imeondoa vikwazo vya fedha kwa Korea ya Kaskazini. Vyombo vya habari vinasema, uamuzi huo wa Wizara ya Fedha ya Marekani umetolewa baada ya mwezi mmoja tokea tarehe 13 Februari mazungumzo ya pande sita katika kipindi cha tatu yalipomalizika. Wakati huo Bw. Christopher alisema, Marekani itatatua suala la fedha ndani ya siku 30. Vyombo vya habari vinaona kuwa kuondoa vikwazo vya fedha kumeikwamua Korea ya Kaskazini kutekeleza ahadi zake za mwanzo. Hivi sasa Korea ya Kaskazini haijatoa jibu lolote kutokana na hatua hiyo ya Marekani.

Mwezi Oktoba mwaka 2005 Marekani ilizuia dola za Kimarekani milioni 24 za Korea ya Kaskazini kwenye benki ya Macau kwa kuituhumu Korea ya Kaskazini kutengeneza dola bandia za Marekani na kuingiza fedha haramu kwenye mzunguko, kutokana na hali hiyo Korea ya Kaskazini iligoma kurudi kwenye mazungumzo ya pande sita kwa miezi 13. Korea ya Kaskazini inaona kuwa kitendo hicho cha Marekani ni cha uhasama dhidi yake na inatetea kuwa haitarejea kwenye mazungumzo na kuacha shughuli za silaha za nyuklia kabla ya Marekani kuondoa vikwazo vya fedha. Ni kutokana na Marekani kulegeza msimamo kuhusu vikwazo hivyo, Korea ya Kaskazini imechukua msimamo wa kutoa ushirikiano.

Kadhalika vyombo vya habari pia vimegundua kuwa, baada ya mazungumzo ya kipindi cha tatu cha duru la tano la mazungumzo ya pande sita kumalizika, Korea ya Kaskazini ilijitahidi kufanya shughuli za kidiplomasia na sasa imekubali kurejesha uhusiano uliosimamishwa kwa miaka minne kati yake na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki na kukubali kurejea tena kwenye shirika hilo. Kutokana na hali hiyo iliyotokea hivi karibuni, mkuu wa mazungumzo wa Marekani Bw. Christopher Hill alisema ziara ya Baradei nchini Korea ya Kaskazini imeleta dalili nzuri.

Vyombo vya habari vinasema, duru la sita la mazungumzo ya pande sita litaanza kabla ya tarehe 19 mwezi huu, licha ya kuwa Korea ya Kaskazini inataka kupata hali nzuri katika mazungumzo hayo kwa kufanya shughuli nyingi za kidiplomasia, pia imeona nia thabiti ya pande zote ya kutokubali kuwepo kwa silaha za nyuklia katika peninsula ya Korea.

Lakini kwenye mkuktano na waandishi wa habari Bw. Baradei hakusema lini Korea ya Kaskazini itafunga miundombinu ya nyuklia, wala hakusema lini wakaguzi wa nyuklia wa shirika la Nishati ya Atomiki duniani watarudi tena nchini Korea ya Kaskazini. Na ahadi ya Korea ya Kaskazini ya kufunga miundombinu ya nyuklia ni hatua ya mwanzo tu, bado ni mbali sana kabla ya kufikia lengo la kuacha kabisa nyuklia. Ni kama Bw. Baradei alivyosema kuwa kuifanya peninsula ya Korea isiwe na nyuklia ni mchakato mrefu wenye utatanishi, utatuzi wa suala hilo unahitaji juhudi za pande zote na za muda mrefu.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-15