Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-16 18:40:43    
Baraza jipya la mawaziri la serikali mpya ya Palestina laundwa

cri

Tarehe 15 pande mbalimbali za Palestina zilikubaliana kuhusu orodha ya baraza la mawaziri la serikali mpya ya Palestina. Siku hiyo waziri mkuu wa serikali ya Palestina Bw. Ismail Haniyeh alikabidhi orodha hiyo kwa mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas, na Bw. Abbas aliikubali orodha hiyo. Lakini baadaye Israel ilisema haitawasiliana na serikali mpya ya Palestina, na watu wa Palestina pia wana maoni tofauti kuhusu serikali hiyo mpya.

Baada ya mazungumzo zaidi ya mwaka mmoja na migogoro mingi ya umwagaji damu, makundi mawili makubwa nchini Palestina Fatah na Hamas, tarehe 15 yalikubaliana orodha ya serikali ya muungano. Waziri mkuu wa uangalizi wa serikali ya Palestina Bw. Ismail Haniyeh, ambaye pia ni kiongozi wa Hamas siku hiyo baada ya kumkabidhi Bw. Abbas orodha hiyo alisema, serikali mpya itafungua ukurasa mpya wa Palestina. Alisema, ?

"Tunatumai kuwa serikali hiyo itafungua ukurasa mpya wa Palestina. Hakika Israel na Marekani zina misimamo tofauti kuhusu serikali hiyo, lakini tutafanya juhudi kadiri tuwezavyo ili kulinda umoja wa taifa, kuondoa vikwazo vya jumuiya ya kimataifa kwa Palestina na kuimarisha mawasiliano kati ya Palestina na jumuiya ya kimataifa."

Kutokana na makubaliano yaliyofikiwa na makundi ya Hamas na Fatah mwezi uliopita huko Mekka, Hamas itachukua nafasi 10 za uwaziri katika baraza la mawaziri, akiwemo waziri mkuu Bw. Haniyeh, na Fatah itachukua nafasi 6 za uwaziri. Mawaziri watatu muhimu wa serikali watakuwa watu huru, wakiwemo waziri wa mambo ya nje Bw. Ziad Abu Amr, waziri wa fedha Bw. Salam Fayyad na waziri wa mambo ya ndani Bw. Hani Kawasmi. Bw. Azzam al-Ahmed kutoka kundi la Fatah atakuwa naibu waziri mkuu.

Moja ya kazi muhimu inayokabili serikali mpya ni kutambuliwa na jumuiya ya kimataifa, ili kumaliza vikwazo vya kiuchumi vya jumuiya ya kimataifa kwa Palestina. Lakini mwongozo wa serikali mpya unawafanya watu wengi wawe na wasiwasi kuhusu hayo. Imefahamika kuwa, ingawa mwongozo wa serikali mpya unasema kuwa utaendelea kusimamisha vita kati yake na Israel, lakini haukusema wazi kuitambui Israel ila tu "kuheshimu" mikataba ya zamani iliyosainiwa na nchi hizo mbili. Mwongozo huo hata unasema "kupinga kithabiti ukaliaji wa Israel". Hivyo serikali ya Israel tarehe 15 ilisema kwa wazi kuwa haitaki kuwasiliana na serikali mpya ya Palestina.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Israel Bw. Mark Regev alisema, serikali mpya ya Palestina haijapokea masharti matatu ya jumuiya ya kimataifa, yaani kutambua wazi Israel, kuacha vitendo vya kimabavu na kupokea mikataba iliyosainiwa kati ya Palestina na Israel. Alisema, ?

"Israel haitawasiliana na serikali mpya ya Palestina. Pia tunatumai kuwa jumuiya ya kimataifa itashikilia kanuni, na kutowasiliana na serikali hiyo inayokataa amani na maafikiano."

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Bw. Sean McCormack siku hiyo pia alisema, Marekani itasubiri hadi serikali mpya ya Palestina iapishwe na kutangaza mwongozo wake. Ofisa mwandamizi wa serikali ya Marekani alisema ataendelea kuwasiliana na Bw. Abbas, lakini kama serikali mpya ya Palestina haitapokea masharti matatu ya jumuiya ya kimataifa, Marekani itaendelea kuiwekea vikwazo serikali mpya ya Palestina. Russia na baadhi ya nchi za Ulaya zililegeza kidogo msimamo, na kukubali kufikiria kutoa msaada kwa Palestina.

Hivi sasa kazi nyingine muhimu inayoikabili serikali mpya ya Palestina ni kumaliza mgogoro wa ndani. Ingawa pande mbalimbali za Palestina zimefikia makubaliano ya kusimamisha vita, lakini hali ya usalama bado ni mbaya. Waziri mpya wa mambo ya ndani wa Palestina Bw. Kawasmi alipohojiwa na waandishi wa habari alisema anatumai pande mbalimbali za Palestina zitashirikiana.

Kamati ya utungaji sheria ya Palestina tarehe 17 itapiga kura kupitisha orodha hiyo, na baada ya hapo serikali mpya ya Palestina itaapishwa. Wakati huo huo watu wa Palestina pia wana wasiwasi kuwa, katika hali ya kuendelea kuwepo kwa mgogoro kati ya Hamas na Fatah, na kutojulikana wazi kwa misimamo ya Israel na jumuiya ya kimataifa, hawana uhakika kama serikali hiyo mpya itadumu kwa muda gani.