Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-16 19:19:54    
Wananchi wa Kenya walivyosherehekea siku ya mwaka mpya wa jadi wa China

cri

Ni siku chache tu zimepita tangu sikukuu ya Spring ambayo ni sikukuu ya mwaka wa jadi wa China imalizike. Wakati wa sikukuu hiyo, wachina walioko nchini China na sehemu mbalimbali duniani, walisherehekea sikukuu hiyo. Tuangalie nchini Kenya, mbali na wachina wanaoishi huko, baadhi ya wakenya vilevile walishiriki kwenye shamrashamra za sikukuu ya Spring.

Tano, nne, tatu, mbili, moja?vijana hao ambao ni wanafunzi wa taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Nairobi wakiongozwa na walimu wao wachina walikuwa wanahesabu sekunde na kukaribisha mwaka mpya wa jadi wa China. Sherehe hiyo ya "kuagana na mwaka uliopita na kukaribisha mwaka mpya kwa kula Jiaozi" ilifanyika kwenye mkahawa mmoja wa Kichina mjini Nairobi, alasiri ya tarehe 17 mwezi wa Februari kwa saa za Beijing, ni usiku wa kuamkia mwaka mpya wa 2007 kwa mujibu wa kalenda ya kilimo ya China.

Sikukuu ya Spring ni sikukuu gani? na Jiaozi ni nini? Kwa nini wachina hula Jiaozi wakati wa sikukuu hiyo? Ili kuwapatia wanafunzi picha ya juujuu kuhusu mila na desturi za Wachina zinazohusu Sikukuu ya Spring, kabla sherehe haijaanza balozi wa China nchini Kenya Bw. Zhang Ming aliwaelezea wanafunzi hao utamaduni ya Sikukuu ya Spring.

"Sikukuu ya Spring yaani Sikukuu ya Mwaka mpya wa jadi wa China ni sikukuu muhimu zaidi kwa Wachina, ambayo ni kama sikukuu ya Krismasi kwa wakristo au sikukuu ya Eid el fitr kwa waislamu. Sikukuu ya Spring ni siku ya kujumuika kwa familia, ni siku ya kusalimiana, vilevile ni siku ya kula Jiaozi."

Bw. Zhang aliendelea kueleza Jiaozi ni chakula gani.

"Kwa kifupi Jiaozi ni kijazo kinachofungwa kwa ganda linalotengenezwa kwa unga wa ngano, kijazo hicho huwa ni nyama na mboga, hiki ni chakula cha jadi cha China, tangu miaka 2600 iliyopita, wachina walianza kutengeneza na kula Jiaozi."

"Wachina wanapotengeneza Jiaozi, wakati fulani wanachanganya sukari, njugu, au tende katika kijazo ambacho huwa ni nyama na mboga, lakini hawaweki katika Jiaozi zote, ni chache tu, watu wanaobahatika ndio wanaoweza kukuta Jiaozi yenye vijazo hivyo. Wachina walisema, ukila Jiaozi yenye Sukari ndani yake, utaishi maisha matamu katika mwaka mpya, na ukikuta tende ndani ya Jiaozi utakuwa na mtoto mmoja, kama ni njugu, utapata watoto wawili, wa kike na wa kiume."

Wanafunzi walivutiwa sana na maelezo ya kusisimua ya Bw. Zhang, isipokuwa baadhi yao walikuwa wanaendelea kutupia macho juu ya nyama na unga ya ngano uliowekwa mezani pembeni ambazo zilikuwa ni za kutengenezea Jiaozi.

Mvumilivu hula mbivu, na kusubiri kwa muda mrefu kuna matokeo. Sasa wanafunzi wanaweza kujaribu kutengeneza Jiaozi wao wenyewe. Wanafunzi hawawezi kuvumilia kusubiri tena hata sekunde moja.

Msichana mmoja alipotengeneza Jiaozi huku akizungumza mwenyewe.

"Nachukua nyama kidogo, nafinya, naendelea kufinya, hapana, ninayotengeneza sio Jiaozi bali ni bata!"

Na baadhi ya wanafunzi hao ni hodari.

Wakisaidiwa na mke wa balozi na walimu, wanafunzi hao walitengeneza Jiaozi nyingi. Lakini Jiaozi hizo ni tamu kweli? Hehe, tusikilize watengenezaji wenyewe wasemaje.

" Ni tamu sana sana sana!"

"Nilijaribu kula Jiaozi pamoja na siki ya pilipili?ladha yake ni nzuri sana, Jiaozi ni chakula kizuri!"

"Wiki ya Utamaduni ya Sikukuu ya Spring ya China" ambayo iliandaliwa na Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Nairobi ilifikia kilele chake katika sherehe ya siku hiyo. Katika wiki hiyo, Profesa Sa Dequan na mwalimu Liu Yong waliandaa shughuli mbalimbali zinazohusu utamaduni ya China, kama vile, mafundisho kuhusu utamaduni wa vyakula wa China, meonesho ya vitabu, video na maandiko na uchoraji wa kichina, wanafunzi wa Taasisi ya Confucius na wanafunzi wengine wa chuo kikuu walifurahia shughuli hizo. Mwanafunzi mmoja anayeitwa Elizabeth Ngiga alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema:

"Natumai kuwa walimu Wachina wataandaa shughuli nyingi zaidi kama hizo, ambazo zitasaidia masomo yetu ya Kichina, na kwa kupitia shughuli hizo sisi wanafunzi tunaona kuwa ili kuwasiliana na marafiki zetu kutoka China na kufahamu utamaduni wa China, ni lazima tujifunze lugha ya Kichina, hali ambayo itaongeza ufanisi wa kusoma. Kama leo nimepata ujuzi mpya kuhusu China, yaani chakula kinachopatikana nchini China pekee----Jiaozi, na sasa hivi nilijaribu mwenyewe kutengeneza Jiaozi, ambacho ni chakula kitamu sana."

Naibu Mkuu wa taasisi ya Confucius Profesa Sa Dequan alieleza hivi:

"Lugha huambatana na utamaduni, ukijifunza lugha peke yako, lugha unayojifunza haitakuwa na kazi yoyote. Wakati unapowasiliana na watu kutoka nchi za nje, unapaswa kufahamu utamaduni wao, ama sivyo utakutana na shida nyingi katika mawasiliano. Taasisi ya Confucius ni taasisi ya kufundisha lugha ya Kichina na Utamaduni wa China, tunafundisha kwa njia ya kuwashirikisha wanafunzi kwenye shughuli za kijamii, na kwa kupitia shughuli hizo, wanaweza kuelewa kihalisi utamaduni wa China, njia ambayo kazi yake ni kubwa zaidi kuliko kufundisha darasani. Kuchagua sikukuu za jadi za Wachina kama kauli mbiu ya shughuli hizo, kama leo, hiyo nafikiri ni njia mwafaka ya mafunzo.