Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-19 20:52:19    
Watu wa Iraq wana matarajio ya kuishi maisha kwa utulivu

cri

Jeshi la muungano la Marekani na Uingereza lilianzisha vita vya Iraq tarehe 20 Machi mwaka 2003, kwa lengo la kupindua utawala wa Saddam Hussein. Sasa ni miaka minne imepita, vita hivyo vimemalizika lakini askari wa Marekani na Uingereza bado wako nchini Iraq na mapambano ya kimabavu yanaendelea kutokea mara kwa mara nchini humo. Je, hivi sasa maisha ya watu wa Iraq yanaendelea vipi? Bw. Najam Mazin mwenye umri wa miaka 33 ni mkazi wa Basra, mji maarufu wenye historia ndefu uliopo kusini mwa Iraq. Mjini Basra wakazi wengi ni waislamu wa madhehebu ya sunni, hakuna wanamgambo wa madhehebu ya shia wala vituo vya kundi la Al-Qaeda, na hali ya huko ni tulivu zaidi kuliko sehemu za kaskazini na katikati za Iraq. Hata hivyo milipuko ya mabomu ni jambo la kawaida huko Basra. Bw. Najam Mazin alisema

"Sisi sote tumeshuhudia milipuko ya mabomu. Ilikuwa siku moja kabla ya sikukuu ya Idi el-Fitri ya mwaka 2005, nilikuwa nikienda kwenye eneo lenye maduka mengi kununua nguo kwa ajili ya sikukuu hiyo. Nilipotoka gari moja lililokuwa limeegeshwa kando ya barabara lililipuka. Wakati huo nilikuwa karibu sana, niliona watu wengi wameanguka kwenye damu nyingi, nilishuhudia mwenyewe tukio hilo. Lakini nina bahati, kwani nilishuhudia tu mlipuko wa mabomu."

Miundo mbinu mingi ya Iraq iliharibiwa kwenye vita hiyo, kwa hiyo maisha ya watu wa Iraq yameathiriwa vibaya. Hali hiyo pia iko mjini Basra ambapo barabara nyingine zina hali mbaya na baadhi ya nyumba zilibomolewa kwa mabomu, maisha ya huko ni magumu sana. Bw. Najam alisema shida kubwa inayowakabilia wakazi wa Basra ni kukatika umeme kila siku. Alisema

"Hivi sasa umeme unakatika mara kwa mara, hili ni tatizo kubwa katika maisha yetu. Ikilinganishwa na hali ya sehemu nyingine nchini Iraq, shirika la umeme la Basra ilianzishwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, zana zake zimepitwa na wakati. Hadi sasa shirika hilo halijapata zana za kisasa za kuzalisha umeme, na huduma za umeme hazipatikani siku nzima, kwa wastani tunapewa umeme kwa saa 3, halafu umeme unakatwa kwa saa 3 nyingine, na hali hiyo inatokea kila siku."

Bwana huyo aliongeza kuwa, nchini Iraq majira ya siku za joto yanaendelea kwa muda mrefu na joto ni kali sana. Kutokana na kutokuwa na umeme wa kutosha, viyoyozi na majokofu hayawezi kufanya kazi, hali hiyo inawafanya wazee na watoto wapate shida sana. Pamoja na tatizo la umeme, familia nyingi za watu wa Iraq zinakabiliwa na matatizo ya kiuchumi. Hivi sasa nchini Iraq bei za vitu zimepanda sana, kiasi ambacho familia nyingi zinashindwa kumudu. Bw. Najam analipwa mshahara unaolingana na dola za kimarekani 200 kwa mwezi, pato hili ni cha kiwango cha wastani huko Basra. Alisema

"Baada ya mwaka 2003 nilikuwa siwezi kupata mshahara kwa uhakika, hivi sasa hali imeboreshwa kwa kiasi. Kwa watu wa kawaida wa Iraq, kama mume na mke wa familia moja wote, wanaweza kukidhi mahitaji ya familia, lakini kama wanapaswa kuwatunza wazazi na kuwasomesha watoto, basi pesa hazitoshi."

Mdogo wa Bw Najam, Mohammad Mazin mwenye umri wa miaka 21 anasoma kwenye chuo kikuu huko Basra. Alisema

"Natumai kuwa hali ya Iraq itatulia, natumai kuwa serikali itatuletea usalama na maisha yenye baraka, pia natumai kuwa Iraq inaweza kuishi kwa urafiki na nchi nyingine duniani."