Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-20 14:54:07    
Wajumbe wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China wazingatia tatizo la kupata tiba kwa wakulima

cri

Kutokana na kuwa hali ya uchumi wa vijijini na maisha ya wakulima bado haiyajaendelea sana, wakulima wana tatizo la kupata matibabu. Ili kupunguza tatizo hilo, kuanzia mwaka 2006 China ilianzisha na kueneza kwa majaribio utaratibu wa ushirikiano wa matibabu vijijini, na utaratibu huo umepata matokeo mazuri. Kwenye mkutano wa tano wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China tatizo hilo lilizungumwa sana.

Kwenye ripoti ya kazi ya serikali waziri mkuu Wen Jiabao alilipa kipaumbele tatizo hilo. Mjumbe Zhou Dingbiao alisema,

"Watu wengi wanalalamikia tatizo la kupata matibabu na gharama kubwa, na tatizo hilo ni kubwa zaidi kwa wakulima. Kwa hiyo kama tatizo la wakulima likitatuliwa, basi tatizo hilo litakuwa limetatuliwa kote nchini."

Mjumbe kutoka mkoa wa Shanxi alisema, huko kwao wakulima wanasema, wakiwa na ugonjwa mdogo wanaishi nao, wakiwa na ugonjwa mkubwa wanavumilia na wakiwa wanapelekwa hospitali basi wamekuwa wagonjwa mahututi." Kwa hiyo anaona kuwa baada ya wakulima kutokuwa na shida ya chakula, tatizo la kupata matitibabu limekuwa linawasumbua zaidi. Alisema,

"Wazazi wangu wako vijijini, na kila mwezi nakwenda kuwatazama, nimeelewa kwamba kweli wakulima wana tatizo la kupata matibabu, wakiwa na ugonjwa mdogo wanavumilia, na wanaposikia vibaya ina maana ugonjwa umekuwa mkubwa kabisa. Hali kama hiyo ni ya kawaida vijijini."

Mwaka 2006 serikali ya China ilianzisha ushirikiano wa matibabu katika sehemu kadhaa kwa majaribio. Huu ni ushirikiano ambao serikali kuu na serikali za mitaa kila moja inachangia yuan 20 na mkulima anachangia yuan 10 na kuunda mfuko wa matibabu kwa fedha hizo.

Mjumbe kutoka hospitali Prof. Hou Shuxun anaona ushirikiano wa aina hiyo unafaa kwa hali ilivyo sasa ya vijijini. Alisema,

"Ushirikiano huo umetoa uhakikisho wa kimsingi wa kupata tiba kwa wakulima na umehakikisha wakulima walioambukizwa ugonjwa wanapata matibabu kwa wakati, na wagonjwa wenye magonjwa sugu au magonjwa makubwa wanapunguziwa mzigo wa malipo. Katika wakati ambapo uchumi wa vijijini bado haujaendelea sana, ushirikiano huo ni mzuri."

Mjumbe mwingine Shi Xinmin alipozungumza na waandishi wa habari alisema, ushirikiano huo umeanza kutekelezwa kwao vijijini, kutokana na uchunguzi aligundua kwamba idadi ya wakulima wanaokwenda kwenye zahanati wameongezeka, hali ambayo zamani walikuwa wanavumilia magonjwa imebadilika. Alisema,

"Wakulima niliozungumza nao wote wanasema ushirikiano huo ni mzuri."

Naibu waziri wa zamani wa afya ambaye pia ni mjumbe wa Baraza hilo Bw. Zhu Qingsheng aliwaambia waandishi wa habari akisema,

"Katika miaka miwili iliyopita, wizara ya afya ilifanya uchunguzi vijijini kuhusu ushirikiano huo, na baadhi ya wenzetu walitoa mapendekezo ya kuuboresha zaidi ushirikiano huo."

Kutokana na uchunguzi, wajumbe wamegundua kwamba upungufu wa madaktari vijijini ni mkubwa, ambao miongoni mwa wakulima milioni 900 nchini China kuna madaktari laki 8 tu na kati ya madaktari hao baadhi hawana uwezo wa kutosha wa udaktari.

Kuhusu upungufu huo mjumbe Hou Shuxun alipendekeza kuhamisha baadhi ya madaktari wa mijini kwenda vijijini na kutoa huduma kwa muda.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-19