Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-20 20:47:50    
Barua 0318

cri
Leo kwanza tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu, na baadaye tutawaletea maelezo kuhusu maoni na mapendekezo ya wajumbe waliohudhuria mikutano ya mwaka wa Bunge la umma la China na Baraza la mashauriano ya kisiasa.

Msikilizaji wetu Zaharan Mohamed al Rujaibi wa sanduku la posta 868 wa Sultanate of Oman ametuletea barua pepe akisema, anapenda kutujulisha kuwa barua pepe zetu kwake zinachelewa vibaya sana labda sio makosa yetu, labda hatuzipati, hivyo mpaka sasa hajapata chochote ama majibu, hivyo ametutumia barua pepe kwa taabu na mashaka mpaka ameipata, njia hii ya e mail atakuwa akitutumia barua nyingi zake kwa e mail, anataka sisi hatutamsahau kwa kalenda na picha za watangazaji na zawadi zozote zile tunazowatumia jamaa wengine.

Anasema yeye ni msikilizaji wa Radio China kimataifa tangu zamani hata kwa miaka arubaini iliyopita, wakati ule Radio Peking ilimtumia zawadi kemkem kama vile kalenda, begi ya kuvaa kifuani, vitabu na magazeti mengi mazuri sana.

Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kimalija wa sanduku la posta 1067 Kahama Shinyanga Tanzania, anasema ni matumaini yake kuwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio china Kimataifa ni wazima wakiendelea kurusha matangazo kutoka mjini Beijing, kwa upande wake ni mzima akiendelea kuitegea sikio Radio China Kimataifa.

Anasema anapenda kutumia fursa hii kuipongeza Jamhuri ya watu wa China kwa kuadhimisha miaka 57 tangu kuasisiwa kwake, na anaipongeza zaidi kwa kuendelea na uhusiano na nchi za Afrika na ulimwengu kwa ujumla. Vilevile anawapongeza wasikilizaji wenzake Ras Franz Manko Ngogo wa Tarime, Mara nchini Tanzania na Mutanda Ayub Sharif wa Bungoma nchini Kenya kwa kupata ushindi wa zawadi maalum wa kuitembelea China katika maadhimisho ya miaka 65 tangu kuanzishwa kwa radio China Kimataifa.

Pia anawaomba wasikilizaji wenzake wote popote walipo ambao hawakubahatika kuchaguliwa katika ushindi wa nafasi maalum wasife moyo, kwani radio China kimataifa inaendelea kuwaletea chemsha bongo kila mwaka. Mwisho anatutakia wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa kazi njema na yenye mafanikio mema katika mwaka huu mpya wa 2007, na urafiki kati yake na Radio China Kimataifa uendelee.

Bwana Noel E. Mshauri wa Seminari ya Mtakatifu Patrick Dun'gunyi, S.L.P 275 Singida nchini Tanzania, anasema ni matumaini yake kuwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya radio China Kimataifa wanaendelea vyema na kazi na kuboresha matangazo, yeye ni mzima akiendelea na majukumu yake ya kila siku. Anasema anapenda kutoa pongezi zake nyingi na hongera kwa mzee aliyesimama kidete (yaani CRI Kutimiza 65) akiendelea kukamilisha shabaha aliyojiwekea, Hongera sana.

Lakini msikilizaji wetu anapenda kutujulisha kuwa, ingawa hana klabu ya wasikilizaji huko aliko, lakini alifanya sherehe pamoja na CRI ya kuadhimisha miaka minane (8) ya uanachama hai wa CRI pamoja na matatizo ya hapa na pale ya usikivu. Anasema yeye alipenda asherekee miaka yake nane ya uanachama wa CRI akiwa nchini China, lakini bahati mbaya hakubahatika. Pia radio anayotumia sasa si nzuri sana kwa usikivu hivyo anaomba kufahamishwa gharama ya radio hapa Beijing ili atume pesa za manunuzi na CRI imtumie radio hiyo.