Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-21 16:23:02    
Ziara ya jahazi la Sweden la Goetheborg nchini China

cri

Katika nusu ya pili ya mwaka 2006 kundi la Wasweden lilikuja nchini China kwa jahazi la Goetheborg lililotengenezwa kwa kuiga mfano wa jahazi kama hilo lililokuwepo karne ya 18. Katika ziara ya miezi minne nchini China, watu wa Sweden walitembelea mkoa wa Anhui wakiwa na chai ya kale ya China iliyozalishwa kwenye mkoa huo.

Katika karne ya 18 kulikuwa na jahazi la wafanyabiashara wa Sweden lililoitwa Goetheborg. Katika karne hilo hili lilikuwa ni jahazi la kisasa la masafa marefu, liliwahi kufanya safari mara tatu kati ya China na Ulaya, likipeleka bidhaa za vito na saa za Ulaya nchini China na kupeleka chai, vyombo vya kauri, hariri na viungo kutoka China hadi Ulaya. Kwa bahati mbaya jahazi la Goetheborg liligonga mwamba na kuanguka katika eneo karibu na Sweden mwaka 1745, hasara iliyosababishwa na ajali hiyo ililingana na pato la Sweden kwa mwaka mzima kwa wakati huo.

Kuanzia miaka ya 80 ya karne iliyopita, watu walifanya majaribio kadhaa ya kuliibua jahazi la Goetheborg. Bidhaa mbalimbali zilizookolewa kutoka kwenye jahazi hilo zilifungua mlango wa historia kwa watu wa hivi sasa. Bw. Matts Larsson ni raia wa Sweden aliyeshiriki kwenye majaribio ya kuliibua jahazi hilo, alikumbusha akisema"Kwenye mabaki ya jahazi hilo, tuligundua tani 370 za chai za Kichina ambazo zilihifadhiwa vizuri ndani ya vyupa vya kauri vilivyowekwa ndani ya masanduku ya mbao. Usiku mmoja tuliandaa tafrija ya chai kwa kutumia chai hiyo, ladha ya chai hiyo ni nzuri sana kiasi ambacho ninashindwa kusimulia."

Kati ya tani hizo 370 za chai, sehemu moja ni chai adimu sana iitwayo Wuliqing iliyozalishwa mkoani Anhui, mashariki mwa China. Miti ya chai hiyo inakua kwenye Mlima Xianyu wenye mwinuko wa mita 1,300 kutoka usawa wa bahari, mahala ambapo panazungukwa na mawingu na ukungu siku zote. Kutokana na mazingira maalumu ya kijiogrofia, chai ya Wuliqing ina harufu nzuri ya maua na madini kadhaa adimu yanayojenga afya ya binadamu. Chai ya namna hii iliorodheshwa kuwa miongoni mwa chai maarufu za China miaka 800 iliyopita.

Mwanzoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, Bw. Larsson na wenzake walipata wazo moja la kutengeneza jahazi moja mfano wa jahazi la Goetheborg, na kuliendesha tena kuja China likiwa na bidhaa za chai, kauri na hariri za China zilizookolewa.

Mwezi Oktoba, mwaka 2005 jahazi hilo jipya lilifunga safari kuja China kwa kufuata njia lililopita jahazi la zamani la Goetheborg.  Mwezi Julai mwaka 2006 jahazi hilo lilifika Guangzhou, na kuanza ziara nchini China. Katika miezi minne iliyofuata, jahazi hilo lilikaribishwa na watu wa sehemu mbalimbali za China.

Marafiki hao kutoka Sweden pia walitembelea mlima wa Xianyu, mkoani Anhui, ambayo ni maskani ya chai ya Wuliqing. Katika shamba la chai, Bw. Larsson na wenzake walionesha chupa ya kauri iliyohifadhiwa chai ya Wuliqing kilichookolewa kutoka kwenye jahazi la zamani la Goetheborg. Bw. Larsson alisema "Miaka zaidi ya 300 iliyopita watu walichuma chai kwa mikono. Hivi sasa ufundi huo wa kale bado unafuatwa na watu, watu wa huko walipokezana ufundi huo kizazi baada ya kizazi. Wakati huo nilisimama katika shamba la kale la chai, niliweza kuhisia historia ya zaidi ya miaka 300, hali ambayo ilinifanya niwe na heshima kubwa kwa sehemu hiyo."

Baada ya kipindi cha karibu karne tatu, chai za kale za Wuliqing sasa zimerudi nyumbani. Kwenye safari hiyo ndefu chai hizo zilipita mabara matano, bahari tatu na nchi kadhaa za Sweden, Hispania, Brazil, Afrika Kusini, Australia na Indonesia. Njia ya safari hiyo ukioneshwa kwenye ramani, unaonekana kama ni utepe wa hariri unaopeperuka.

Katika maskani ya chai ya Wuliqing, watu wa huko walitoa zawadi maalumu kwa marafiki hao wa Sweden, nazo ni chupa 100 za chai ya Wuliqing iliyozalishwa mwaka 2006, na kila chupa yaa kauri iliyokuwa na nembo ya jahazi la Goetheborg.

Naibu mkuu wa mji wa Chizhou Bibi Liu Guoqing alisema Tunafurahia kupata habari kuwa chai zilizozalishwa miaka 260 iliyopita hapa kwetu ziliokolewa kutoka kwenye jahazi la biashara la Goetheborg. Nahodha Peter alituoneshea chai hiyo kale. Naona huu ni mwujiza."

Bibi Liu alifahamisha kuwa, ufundi wa kutengeneza chai ya Wuliqing uliwahi kupotea. Maprofesa wa kitengo cha chai cha chuo kikuu cha kilimo cha Anhui walifanya utafiti kwa miaka 20, wakafanikiwa kufufua ufundi huo wa jadi miaka kadhaa tu iliyopita. Bibi Liu alieleza matarajio yake kuwa, kutokana na kurudi kwa ufundi huo wa kutengeneza chai ya Wuliqing na ziara hiyo ya jahazi la Goetheborg, urafiki na biashara kati ya China na Sweden utapata maendeleo makubwa zaidi. Alisema  "Natoa heshima kubwa kwa juhudi za kutengeneza upya jahazi la Goetheborg na kurudi kwa safari ya jahazi hilo kuja China, pia napongeza juhudi hizo. Natumai sisi na Swenden tutaweza kuendelea na urafiki na biashara zilizokuwepo karne kadhaa iliyopita, na kuzidi kukuza uhusiano huo."

Tukio hilo la Wasweden kuleta chai cha kale cha Wuliqing liliwavutia sana wafanyabiashara wa chai huko Anhui. Mkuu wa kampuni ya chai ya Tianfang ya Anhui Bw. Zheng Xiaohe alimwambia mwandishi wa habari kuwa, miaka zaidi ya 100 iliyopita, mfanyabiashara mmoja wa chai wa Anhui aliyeitwa Huang aliwahi kusanifu nyumba yake kuwa kama umbo la meli, akionesha nia yake ya kusafirisha chai nje ya China. Hivi sasa wafanyabiashara wa chai wa Anhui wanatekeleza nia hiyo. Bw. Zheng Xiaohe alisema "Nina mpango wa kuanzisha maduka nchini Sweden, na kuuza chai ya Wuliqing."

Jahazi la Goetheborg liliondoka China mwishoni mwa mwaka 2006, likirudi nyumbani nchini Sweden. Imefahamika kuwa kati ya miezi ya Julai na Agosti, mwaka 2007 jahazi hilo litapita London, Uingereza, ambapo ujumbe mmoja kutoka mji wa Chizhou, maskani ya chai ya Wuliqing, utapanda jahazi hilo na kwenda kutembelea Stockholm, mji mkuu wa Sweden.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-21