|
Tarehe 20 saa nane mchana katika miji mikubwa nchini Israel, kutokana na milio ya king'ora mazoezi ya kujikinga dhidi ya mashambulizi ya kigaidi yalianza katika miji hiyo. Mazoezi hayo yalifanyika kwa siku mbili, polisi, askari wa jeshi, wazimamoto na waokoaji wa dharura walishiriki kwenye mazoezi hayo.
Shule moja ilishambuliwa, magaidi walifyatua risasi na kulipua mabomu ya kikemikali, ndani ya shule hiyo kulikuwa na moshi mnene.
Mashambulizi hayo yalisababisha watu wengi kufa na kujeruhiwa, watu waliosalimika walikimbia kutoka kwenye shule hiyo kwa kelele.
Baada ya dakika chache, magari ya wagonjwa mahututi yalifika kwenye shule hiyo, watu waliovaa nguo na kofia za kukinga sumu waliingia shuleni, walipambana na magaidi, walimwua "mgaidi mmoja" na kumkamata mmoja mwingine.
Sambamba na kuwaokoa majeruhi, magari ya zimamoto pia yalifika kwenye shule na kujenga mara moja chumba cha kuwahudumia watu walioathirika kwa sumu.
Watu wenye huzuni na hasira wakafanya maandamano nje ya shule na walipurukushana na askari polisi.
Baada ya muda wa saa mbili hivi mazoezi yalimalizika.
Hayo ni mazoezi yaliyofanyika tarehe 20. Msemaji wa jeshi la Israel Bw. Micky Rosenfeld alisema,
"Askari polisi elfu tano walihudhuria mazoezi hayo. Hayo ni mazoezi ya kwanza kuwashirikisha askari polisi, askari wa jeshi, waokoaji wa dharura na wazimamoto. Lengo lake ni kuimarisha uwezo na ushirikiano wa idara hizo wakati magaidi wanapofanya mashambulizi."
Bw. Rosenfeld alisema mazoezi kama hayo yatafanyika kila baada ya miaka miwili.
Naibu waziri wa ulinzi wa Israel Bw. Ephraim Sneh alisema, mazoezi hayo yanafanywa ili kuwafanya askari wa Israel wayakumbuke mafunzo waliyopata katika migogoro kati ya Israel na Lebanon mwaka jana, na kujiandaa kwa ajili ya vita vitakavyotokea baadaye.
Ingawa mazoezi hayo yaliathiri mawasiliano ya barabara lakini watu wa Israel wanaunga mkono. Mkuu wa hoteli ya Tel Aviv Bw. David alisema, vita kati ya Israel na Lebanon au Iran hakika vitatokea, kwa hiyo ni lazima tujiandae kabla ya wakati. Alieleza,
"Iran ni nchi hatari. Kabla ya nchi hiyo haijawa na silaha za nyuklia haithubutu kuishambulia Israel. Lakini baada ya kuwa na silaha hizo huenda ikaishambulia, kwa hiyo lazima tuwe tayari."
Kwenye mkahawa mmoja kijana aitwaye Alon ana maoni tofauti akisema,
"Vita kati ya Israel na nchi nyingine vitatokea, lakini Israel haitashambuliwa kwa silaha za nyuklia, kwani Israel ina uwezo mkubwa kurudisha mashambulizi hayo. Pengine magaidi fulani wataishambulia Israel lakini mashambulizi hayo hayatakuwa makubwa."
"Ndani ya mkahawa, muziki mwororo unasikika, watu wanaburudika na kahawa kwa starehe. Hali hiyo haina tofauti na sehemu nyingine, ila tu mlinzi anamkagua kila mteja. Milio ya ving'ora inasikika kwa mbali, ambayo inawatahadharisha watu wazingatie usalama kila wakati."
Idhaa ya kiswahili 2007-03-21
|