Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-21 16:27:39    
Wataalamu wa usingaji wenye ulemavu wa macho wafundisha wanafunzi

cri

Hivi karibuni sherehe moja ya kumkaribisha mwalimu ilifanyika kwenye hospitali ya usingaji ya Beijing ambayo ni hospitali kubwa kabisa ya usingaji wa matibabu ya kichina nchini China. Madaktari vijana 10 walitoa heshima kwa madaktari wazee watano, na kukabidhiwa nyaraka na vitabu vilivyorekodi maarifa na utaalamu wao wa miaka mingi. Madaktari hao wazee wote wana ulemavu wa macho, mwenye umri mkubwa zaidi ana miaka 71 na mdogo ana umri wa miaka 62, wote ni wataalamu wa usingaji katika hospitali ya usingaji ya Beijing. Na umri wa wastani wa wanafunzi hao 10 ni 28, na sita kati yao pia ni wenye ulemavu wa macho.

Kwenye sherehe hiyo, mzee Shi Ruihua mwenye umri wa miaka 67 alikuwa mwalimu kwa wanafunzi wawili. Bw. Shi Ruihua alipata uzoefu Kutokana na uzoefu wa miaka mingi katika kazi ya matibabu ya usingaji na kufundisha wanafunzi, hasa ana maarifa maalum kuhusu matibabu ya magonjwa ya kiuno. Alishiriki kwenye kazi ya kuandika vitabu kadhaa kuhusu matibabu ya jadi ya kichina. Kwenye sherehe hiyo, Bw. Shi Ruihua alisema:

"sisi wazee tunapenda kuwafundisha vijana maarifa yetu, na kuwasaidia kupata maendeleo kwa haraka. Tutawafundisha kwa tuwezavyo ili kuwasaidia wawe hodari zaidi."

Matibabu ya usingaji yenye historia ya zaidi ya miaka 2000 ni hazina kubwa ya matibabu ya jadi ya kichina. Matibabu hayo yanasaidia kutibu magonjwa ya mfupa wa shingo, kiuno na viungo vya bega kwa njia ya usingaji kwa mujibu wa nadharia ya matibabu ya jadi ya kichina. Kutokana na maendeleo ya muda mrefu, hivi sasa matibabu ya usingaji yanatumiwa katika matibabu ya magonjwa ya aina zaidi ya mia moja. Usingaji wa kimatibabu, pamoja na dawa za kichina na akyupancha zinatiliwa maanani zaidi katika sekta ya matibabu ya nchini China na kote duniani.

Hospitali ya usingaji ya Beijing ilianzishwa mwaka 1958. Mwanzoni hospitali hiyo ilikuwa ni zahanati ndogo yenye madaktari 7, baada ya maendeleo ya miaka 50, hivi sasa hospitali hiyo imekuwa hospitali kubwa kabisa ya usingaji ya kimatibabu nchini China, na asilimia 40 ya madaktari wa hospitali hiyo wana upofu. Ingawa madaktari hao hawawezi kuona, lakini wana hisia maalum ya kugusa pamoja na uwezo mkubwa wa kukumbuka mambo, wanatumia mikono yao kuondoa maumivu kwa wagonjwa. Kila asubuhi, wagonjwa wengi husubiri kwenye misururu katika mlango wa hospitali hiyo. Bi. Jin Jing mwenye umri wa miaka 40 hivi anafanya kazi ya uhariri katika kampuni moja mjini Beijing, yeye alipatwa tatizo la mfupa wa shingo kutokana na kufanya kazi mezani kwa muda mrefu kila siku. Kutokana na ushauri wa rafiki yake, Bi. Jin Jing alikwenda kupata matibabu ya usingaji kwenye hospitali hiyo. Alisema:

"tunakuja kwenye hospitali hii kutokana na sifa yake. Hii ni mara yangu ya tatu kupata matibabu hapa, kwa kweli nimejisikia vizuri zaidi baada ya usingaji. Madaktari wa hospitali hiyo wote wana maarifa na wanafanya kazi kwa makini. Kwa ujumla nimeanza kupona hatua kwa hatua baada ya kupewa matibabu hayo."

Kutokana na mageuzi ya kijamii na utaratibu wa maisha kuwa wenye pilikapilika nyingi, watu wengi hasa vijana, wameanza kupatwa magonjwa ya mfupa ya shingo au ya kiuno, pamoja na kuwa watu wanapendelea zaidi matibabu ya asili, hivyo matibabu ya usingaji yanakaribishwa na wagonjwa. Mkuu wa hospitali ya usingaji ya Beijing Bw. Lai Wei alisema, kutokana na sababu mbalimbali, upungufu wa watu wenye utaalamu huo umetokea katika maendeleo ya hospitali hiyo. Sherehe hiyo ya kukaribisha walimu iliandaliwa kwa ajili ya kurithisha utaalamu wa madaktari wazee. Bw. Lai Wei alisema:

"wataalamu hao wazee wenye ustadi maalum na maarifa mengi ni hazina kubwa ya hospitali hiyo. Lakini kutokana na hali ya afya na umri wa wazee hao, tumetambua kuwa tunakabiliwa na kazi kubwa ya kurithisha utaalamu wa wataalamu hao. Tukiweza kuurithisha, si kama tu tutatoa mchango kwa maendeleo endelevu ya hospitali hiyo, bali pia itasaidia kuhimiza maendeleo ya kazi ya matibabu ya usingaji."

Bw. Lai Wei alisema matibabu ya usingaji ni matibabu yenye utendaji halisi, mbali na mahitaji ya ufahamu wa nadharia mbalimbali, bali pia yanahitaji uzoefu mwingi wa utendaji wa kimatibabu. Njia ya jadi ya walimu kufundisha wanafunzi hatua kwa hatua inasaidia kurithisha matibabu hayo vizuri zaidi.

Madaktari vijana hodari waliochaguliwa na hospitali hiyo wote wana ufahamu kamili wa nadharia husika na uzoefu kiasi wa kimatibabu. Kutokana na mpango wa hospitali hiyo, watafuatana na wataalamu hao wazee na kujifunza kwa miaka mitatu. Wakati wa kutoa matibabu kwa wagonjwa, wakikumbana magonjwa sugu, wanafunzi wanaweza kuomba msaada kutoka kwa walimu wao, kila siku kuna muda maalum kwa walimu kufundisha wanafunzi hatua kwa hatua.

Daktari Ma Yuzhong wa hospitali hiyo mwenye upofu, ana umri wa miaka 36, alipokuwa na umri wa miaka 23, alijifunza usingaji katika chuo kikuu cha Changchun, na alianza kufanya kazi kwenye hospitali ya usingaji ya Beijing mwaka huohuo. Hivi sasa anasomea shahada ya pili kwenye idara ya akyupancha katika chuo kikuu cha matibabu ya kichina cha Beijing.

Bw. Ma Yuzhong alisema anaona fahari kuwa mwanafunzi wa mzee Shi Ruihua. Alisema tangu aanze kujifunza kutoka kwa mzee Shi Ruihua, amepata maendeleo makubwa, na ataendelea kufanya juhudi ili kuweza kurithi utaalamu wa mwalimu wake. Bw. Ma Yuzhong alisema:

"mwalimu ananifundisha mkono kwa mkono, nikiwa na maswali ninamwuliza moja kwa moja, njia hii ni nzuri sana, na nimepata maendeleo makubwa. nashukuru hospitali kutupatia fursa hiyo, tutatumia fursa hii muhimu kujifunza na kurithi maarifa ya wataalamu hao wazee."

Mkuu wa hospitali ya usingaji ya Beijing Bw. Lai Wei alisema, hospitali hiyo imetenga Yuan milioni moja ili kusaidia kurithisha vizuri zaidi maarifa ya wataalamu wazee. Katika muda wa miaka miwili, hospitali hiyo imeanda vitabu na VCD kadhaa kuhusu uzoefu wao wa miaka ya 50 wa matibabu ya usingaji, ili kuwasaidia madaktari vijana wajifunze na kueneza maarifa ya wataalamu hao kwenye jamii.