|
Mapambano ya kisilaha yalitokea tarehe 21 huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, na kusababisha vifo na majeruhi 17. Hayo ni mapambano makali kabisa kutokea jeshi la kundi la mahakama za kiislamu la Somalia lishindwe na kukimbia mji wa Mogadishu. Mapambano hayo yamefanya hali mbaya ya usalama nchini Somalia kuwa mbaya zaidi.
Alfajiri ya siku hiyo, kikosi cha pamoja cha jeshi la serikali la Somalia na askari wa Ethiopia kilipoingia kwenye sehemu ya katikati ya mji wa Mogadishu kilikutana na watu waliofunika nyuso zao wakiwa na bunduki na kupambana nao. Baada ya mapambano hayo, watu wenye silaha walikokota miili ya askari mmoja wa jeshi la serikali la Somalia na askari mmoja wa Ethiopia kwenye mtaa mwingine na kuichoma moto. Kutokana na takwimu zisizokamilika, mapambano hayo yalisababisha vifo vya watu 7 na wengine 10 kujeruhiwa.
Mnamo miezi kadhaa iliyopita, matukio ya mashambulizi yanatokea karibu kila siku nchini Somalia. Serikali ya mpito ya Somalia ilitangaza kutekeleza mpango wa usalama wa mwezi mmoja, lakini mpango huo haukupata mafanikio. Hasa baada ya tarehe 12 mwezi huu, bunge la mpito la Somalia liliidhinisha serikali ya mpito kurudi mjini Mogadishu kutoka Baidoa, mji Mogadishu uliingia katika mapambano mfululizo. Hadi sasa mapambano yanayaoendelea yamesababisha vifo vya raia kumi kadhaa wakiwemo watoto. Vyombo vya habari vinaona kuwa lengo la mapambano hayo ni kuweka vizuizi kwa serikali ya mpito ya Somalia kurudi katika mji mkuu. Msemaji wa rais wa Somalia pia aliainisha kuwa washambuliaji walijaribu kutumia mashambulizi hayo kuonesha kuwa serikali ya mpito haina uwezo wa kudhibiti hali ya mji mkuu.
Tangu mwaka 1991, kwa muda mrefu Somalia imekuwa katika mapambano kati ya mabwana wa vita. Mwaka 2004, serikali ya mpito ya Somalia iliundwa mjini Nairobi na baadaye ilihamia nchini Somalia, lakini kutokana na kukosa jeshi lenye askari wengi, serikali ya mpito haikuweza kudhibiti nchi. Mwezi Juni mwaka jana, jeshi la muungano wa mahakama za kiislamu la Somalia liliuteka mji mkuu Mogadishu na serikali ya mpito ya Somalia ililazimishwa kuhamia mjini Baidoa, kilomita 250 kaskazini magharibi ya mji wa Mogadishu. Mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka jana, kutokana na msaada wa jeshi la Ethiopia, jeshi la Somalia lilirejesha sehemu kubwa ya nchi hiyo ukiwemo mji wa Mogadishu, lakini watu wenye silaha wa kundi la mahakama za kiislamu walieleza kuwa wataanzisha vita vya msituni kama vya Iraq. Baada ya tarehe 23 mwezi Januari mwaka huu Ethiopia ilipotangaza kuondoa jeshi lake kutoka nchini Somalia, hali ya usalama ya mji wa Mogadishu ilibadilika ghafla na kuwa mbaya.
Ili kuisaidia serikali ya mpito ya Somalia kutuliza hali ya nchi hiyo, Umoja wa Afrika ulikabidhiwa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jukumu la kutumia jeshi la kulinda amani lenye askari 8000 nchini Somalia. Lakini jeshi hilo halijaundwa hadi hivi sasa. Askari 200 wa jeshi la kulinda amani la Uganda walioko mjini Mogadishu pia wana upungufu wa zana mbalimbali.
Kuanzia mwezi Februari mwaka huu, wakazi elfu 40 mjini Mogadishu walikimbia makazi yao. Serikali ya mpito ya Somalia ina mpango wa kuitisha mkutano wa maafikiano ya kitaifa tarehe 16 mwezi Aprili, ambapo serikali ya mpito itafanya mazungumzo na majeshi mbalimbali ya madhehebu na kujadili njia za kutuliza hali ya nchini humo. Hali ya Somalia inazidi kufuatiliwa na jumuiya ya kimataifa siku hadi siku.
Idhaa ya kiswahili 2007-03-22
|