Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-22 19:46:47    
Kuzuia mashambulizi ya aibu kumeorodheshwa kwenye somo la elimu ya usalama la shule za msingi na sekondari nchini China

cri

Msichana Hui Lan mwenye umri wa miaka 11 ni mwanafunzi wa shule ya msingi ya mjini Nanchang. Kama walivyokuwa watoto wengine wengi wa rika lake, yeye hafahamu maana ya mashambulizi ya aibu, lakini hivi sasa suala hilo limefuatiliwa zaidi na wazazi wa watoto, jamii na serikali nchini China.

Mwongozo wa maelekezo ya elimu ya usalama wa umma kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari uliotolewa hivi karibuni na wizara ya elimu ya China kwa mara ya kwanza umeorodhesha udhalilishaji wa kijinsia, maafa ya kimaumbile na vitendo vya kimabavu shuleni kuwa mambo ya elimu ya usalama wa umma kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, shule hizo zimeagizwa kuwafundisha wanafunzi namna ya kujiokoa na kujilinda wakati wakikumbwa na matukio ya dharura.

Mwongozo huo unasema wanafunzi wa shule za msingi kutoka darasa la 4 hadi 6 wanatakiwa kufahamu njia ya kawaida ya kukabiliana na maovu, matishio na mashambulizi ya kijinsia, wanafunzi wa sekondari ya chini wanatakiwa kufahamu ustadi wa kimsingi wa kupambana na matukio hayo ya dharura, ambapo wanafunzi wa sekondari ya juu wanatakiwa kufahamu namna ya kujikinga dhidi ya udhalilishaji wa kijinsia.

Nchini China watu hukwepa kuzungumza hadharani suala kuhusu kufanya mapenzi, walimu na wazazi wa watoto hushindwa kuwaambia watoto mambo kuhusu mashambulizi ya aibu. Lakini wataalamu wa saikolojia wamedhihirisha kuwa, kuwaelimisha watoto namna ya kuzuia kudhalilishwa kijinsia ni jambo muhimu sana. Naibu mkurugenzi wa kituo cha msaada wa kisheria na utafiti kwa watoto na vijana cha China Bi. Zhang Xuemei alisema, hivi sasa matukio ya watoto kukumbwa na mashambulizi ya aibu yanatokea mara kwa mara.

Mkuu wa shirika la kuzuia unyanyasaji na kuwapuuza watoto la Shangxi Bwana Ning Huangxia alisema katika miaka mitano iliyopita, shirikisho la wanawake la Shangxi peke yake lilipokea malalamiko zaidi ya 50 kuhusu watoto wa kike kushambuliwa na wanaume, baadhi ya matukio yaliwahusu watoto wa kike kumi kadhaa. Alisema kutolewa kwa mwongozo huo kuna umuhimu mkubwa.

Mzazi wa mwanafunzi mmoja wa Beijing alisema, yeye husoma habari kuhusu watoto kushambuliwa kwa aibu kwenye vyombo vya habari, lakini hajui namna ya kumfahamisha mtoto wake kuhusu mashambulizi ya aibu na kuimarisha mwamko wa kujilinda. Kuwepo kwa somo maalum kuhusu namna ya kuzuia mashambulizi ya aibu shuleni kutawasaidia watoto wafahamu zaidi hatari zilizopo ili wajikinge.

Hivi sasa fani mbalimbali za kijamii nchini China zimeanza kufuatilia hali ya mashambulizi ya aibu kwa watoto. Uchunguzi uliofanywa kwenye mtandao wa Internet kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wa mijini umeonesha kuwa, zaidi ya nusu ya wanafunzi hawafahamu kitu chochote kuhusu udhalilishaji wa kijinsia, na wanafunzi wengi hawaelewi maana halisi ya mashambulizi ya aibu kwa watoto, wengine wanadhani ni wanafunzi wa kike tu wanaweza kukumbwa na mashambulizi ya aibu, na wengine wakaona kuwa mashambulizi ya aibu kwa watoto hufanywa na watu wasiowafahamu.

Lengo la kuweka somo la usalama ni kuwawezesha wanafunzi wawe na mtizamo sahihi kuhusu afya, usalama na maisha. Sheria ya kuwalinda watoto ya China imeweka kifungu cha kupiga marufuku mashambulizi ya aibu dhidi ya watoto. Katika miaka ya karibuni idara husika zimeanzisha tovuti maalum kuhusu elimu ya usalama na mawasiliano ya habari, kuunda mashirika ya aina mbalimbali ya kiraia au ya kiserikali ili kueneza ujuzi kuhusu namna ya kuzuia mashambulizi ya aibu kwa watoto na kuwapa matibabu ya kisaikolojia watoto wanaokumbwa na mashambulizi ya aibu.