Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-23 16:09:44    
Chuo cha Confucius katika Chuo kikuu cha Zimbabwe chafunguliwa rasmi

cri

Tarehe 16 mwezi machi Chuo cha Confucius katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe kilifanya sherehe ya kufunguliwa rasmi huko nchini Zimbabwe, waziri wa elimu ya juu wa Zimbabwe, balozi wa China nchini Zimbabwe, naibu mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Zimbabwe na watu mia moja hivi kutoka idara za utamaduni na elimu za Zimbabwe walihudhuria sherehe ya kufunguliwa kwa Chuo cha Confucius. Balozi wa China nchini Zimbabwe Bwana Yuan Nan alisema, China na Afrika zote ni machimbuko ya ustaarabu wa binadamu, katika karne ya 21 watu wenye aina hizo mbili za ustaarabu wanapaswa kuwasiliana zaidi. Akisema:

"China na Zimbabwe zinatakiwa kuimarisha mawasiliano zaidi ya kielimu na kiutamaduni kati ya vijana wa nchi hizo mbili, ili wawe daraja la kuzidisha maelewano kati ya wananchi wa nchi hizo mbili. Pia watakuwa nguvu ya kusukuma mbele uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Kuanzishwa kwa Chuo cha Confucius kutatoa nafasi nyingi zaidi kwa vijana wa Zimbabwe kujifunza lugha ya Kichina, bila shaka kitachangia mawasiliano ya kiutamaduni na kielimu kati ya nchi hizo mbili."

Balozi Yuan alisema, katika siku zijazo China itatoa udhamini kwa wanafunzi wengi zaidi wa Zimbabwe kuja kusoma nchini China, na kuwatuma watu wengi zaidi wanaojitolea wa China kwenda kufanya kazi nchini Zimbabwe. Waziri wa elimu ya juu wa Zimbabwe Bwana Stan Mudenge alisema:

"Kuanzishwa kwa Chuo cha Confucius katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe kutatoa fursa nyingi zaidi kwa watu wa Zimbabwe kupata elimu. Serikali za China na Zimbabwe zimekubali kuongeza zaidi kozi, mbali na somo la lugha ya Kichina na utamaduni wa China, pia kitaanzisha somo la sayansi ya kimaumbile, somo la uhandisi na masomo ya siasa na uchumi, ili kuzidisha maelewano kati ya wananchi wa China na Zimbabwe."

Bw. Mudenge alisema ni muhimu kwa watu wenye utamaduni tofauti kuwasiliana na kufahamiana. Hivi sasa watu wengi wa Zimbabwe wanakuja China kusoma na kufanya biashara, hivyo wanahitaji sana kujifunza Kichina na kufahamu utamaduni wa China. Lengo la Chuo cha Confucius nchini Zimbabwe ni kukidhi kadiri iwezekanavyo matakwa ya watu wa Zimbabwe ya kuifahamu China. Mkurugenzi wa ofisi inayoshughulikia mambo ya utamaduni ya ubalozi wa China nchini Zimbabwe Bi. Wu Jianhua alisema:

"Tunakifanya Chuo cha Confucius kama kituo cha utamaduni wa China, kitaeneza utamaduni wa China kama vile akyupancha, wushu , kuandaa mihadhara ya aina mbalimbali, kufanya shughuli za kiutamaduni, na kuonesha filamu za China. Chuo cha Confucius kitakuwa dirisha la watu wa Zimbabwe kufahamu mambo ya China."

Walimu wawili wa kwanza wa Chuo cha Confucius katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe ni walimu wanaojitolea. Bi Song Shuang ni mmoja wa walimu hao. Alisema:

"Naona furaha kubwa kupata nafasi hii ya kufundisha lugha ya Kichina katika Chuo cha Confucius. Jambo linalonishangaza ni kwamba, mafunzo ya lugha ya Kichina yanakaribishwa sana nchini Zimbabwe, mimi na mwenzangu tunafunidsha madarasa mawili kwa mbalimbali. Wanafunzi wengi wanaojifunza Kichina ni maofisa na wanakampuni."

Chuo cha Confucius katika Chuo Kikuu cha Zimbabwe kina wanafunzi 50, wamegawanyika katika darasa la mchana na darasa la usiku. Mwanafunzi Josephine Takundwa aliwahi kuja China, yeye anafanya biashara na China hivyo kujifunza lugha ya Kichina kutamsaidia sana katika biashara yake.

Mwandishi wetu wa habari hivi karibuni alitembelea Chuo cha Confucius kilichoanzishwa mwaka 2004 katika Chuo Kikuu cha Stellenbos, Afrika kusini. Mkuu wa Chuo hicho Bwana Martyn Davis alifahamisha kuwa hivi sasa Chuo cha Confucius katika Chuo Kikuu cha Stellenbos kina wanafunzi 97 kutoka sehemu mbalimbali. Wanafunzi hao wana imani tofauti za kidini na utamaduni tofauti, lakini upendo wao kwa utamaduni wa China umewajumuisha pamoja. Kwenye darasa la kujifunza lugha ya Kichina wanafunzi wote wanajifunza Kichina kwa makini, na wote wamepewa majina ya Kichina, mwanafunzi anayeitwa Jin Lai alisema:

"Mwaka huu natumaini kushiriki katika mashindano ya 'daraja la Kichina' ya wanafunzi wa vyuo vikuu duniani, nikipata matokeo mazuri, nitaweza kwenda China kwa niaba ya wagombea wa sehemu ya Afrika."

Mwalimu wa Kichina wa Chuo cha Confucius katika Chuo Kikuu cha Stellenbios Bi. Yu Aimei alisema,

"Wanafunzi wengi wanakuja hapa kujifunza Kichina kutokana na kupenda utamaduni wa China. Wanaona kuwa utamaduni wa China una historia ndefu na mambo mengi."

Mwezi Oktoba mwaka jana Chuo Kikuu cha Stellenbos kilifanya shughuli za mwezi wa utamaduni wa China, kufanya maonesho ya picha na video au filamu kuonesha mandhari nzuri ya kimaumbile, na kuwafahamisha wanafunzi wa chuo kikuu hicho hali ya China ilivyo na utamaduni wa makabila mengi ya China. Chuo cha Confucius pia kiliandaa mihadhara na shughuli za aina mbalimbali, kama vile kunywa chai ya kichina, kula chakula cha kichina, kuimba nyimbo za kichina, na kutazama filamu za kichina, ili kuwawezesha walimu na wanafunzi wa chuo hicho waone uzuri wa utamaduni wa China. Mkurugenzi wa Chuo cha Confucius Bwana Davis alisema:

"Ni vigumu sana kwa watu wenye lugha tofauti, utamaduni tofauti na kutowasiliana kujenga uaminifu kati yao. Hivyo chombo cha lugha na mawasiliano ya moja kwa moja ni msingi wa kujenga uaminifu kati ya binadamu."

Bw. Davis anapanga kufanya shughuli za kuadhimisha miaka 10 tangu uhusiano wa kibalozi kati ya China na Afrika kusini uanzishwe, ambazo ni pamoja na kuialika timu ya wanasoka wa China kwenda Afrika kusini kwenye michezo ya kirafiki na timu ya Afrika kusini.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-23