Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-23 16:33:46    
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa afanya ziara ya ghafla mjini Baghdad

cri

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon tarehe 22 aliwasili ghafla mjini Baghdad kwa ziara ya siku moja nchini Iraq. Hii ni mara ya kwanza kwa katibu mkuu huyo kuitembelea Iraq. Wachambuzi wanaona kuwa sababu ya Bw. Ban Ki-moon kufanya safari yake ya kwanza katika Mashariki ya Kati nchini Iraq yenye hali mbaya ya usalama ni kwa ajili ya kuonesha kuzingatia suala la Iraq na kuunga mkono serikali ya sasa ya Iraq na kuutaka Umoja wa Mataifa ufanye kazi kubwa zaidi katika suala la Iraq.

       

Baada ya kuwasili mjini Baghdad, Bw. Ban Ki-moon alifanya mazungumzo na waziri mkuu wa Iraq Nouri Al-Maliki nyumbani kwa waziri mkuu katika eneo la kijani mjini humo. Habari zinasema Bw. Ban Ki-moon na Bw. Nouri Al-Maliki walizungumzia hasa mpango wa ukarabati wa Iraq wa "mkataba wa kimataifa wa Iraq" ambao ulianzishwa kwa pamoja na Umoja wa Mataifa na serikali ya Iraq. Kutokana na mpango huo, serikali ya Iraq inashughulikia kuimarisha uundaji wa jeshi na kukamilisha kazi za utungaji wa sheria na jumuiya ya kimataifa inayoelekezwa na Umoja wa Mataifa inaongeza misaada ya kisiasa, kiuchumi na kiufundi kwa Iraq. Mpango huo umeelekeza malengo ya kila mwaka ya maendeleo ya uchumi ya Iraq kwa miaka mitano ijayo. Bw. Ban Ki-moon aliuchukulia mpango huo kama ni chombo cha kuiwezesha Iraq kutoa uwezo wake ambao bado haujatumika na kuitaka jumuiya ya kimataifa iunge mkono kwa nguvu mpango huo mpya wa ukarabati wa Iraq.

Baada ya mazungumzo hayo, Bw. Ban Ki-moon alieleza kuwa amefanya mazungumzo mazuri na Bw. Nouri Al-Maliki na kuahidi kuendelea kuiunga mkono serikali ya Maliki. Bw. Maliki alieleza kuwa ana imani na mustakabali wa Iraq na uwezo wa serikali ya Iraq kushughulikia mambo ya usalama. Naye Bw. Ban alisema si muda mrefu baadaye ataweza kuona Iraq yenye ustawi na usalama zaidi. Bw. Maliki alisema anaona kuwa ziara ya Bw. Ban imeonesha kuwa Iraq imerejesha uwezo wa kuwapokea viongozi wakubwa duniani, kwani imepiga hatua kubwa kwa kuelekea utulivu. Lakini wakati mkutano na waandishi habari ukiwa unaendelea, mlipuko mkubwa ulitokea mita 50 karibu na ukumbi wa mkutano huo na magari mawili yaliteketezwa. Bw. Ban Ki-moon aliposikia mlipuko huo, alijificha nyuma ya jukwaa la ukumbi. Kwa bahati nzuri Bw. Ban na Bw. Maliki hawakuumia. Ingawa mkutano huo uliendelea baada ya mlipuko, lakini ulimalizika kwa haraka. Ofisa wa usalama wa Iraq alieleza kuwa mlipuko huo ulikuwa ni shambulizi la roketi. Sasa haijulikani kama shambulizi hilo lilimlenga Bw. Ban Ki-moon. Lakini mlipuko huo unaonesha kuwa kwa katibu mkuu mpya Ban Ki-moon anayetaka kutatua matatizo makubwa ya Iraq na kuweka heshima yake, atakabiliwa na shida nyingi zaidi kuliko mambo anayotarajia.

Habari zinasema katibu mkuu huyo pia atazitembelea Misri, Israel, Palestina, Jordan, Saudi Arabia na Lebanon kwa mpango uliowekwa baada ya ziara hiyo nchini Iraq. Katika kipindi hicho, tarehe 28 atahudhuria mkutano wa wakuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu utakaofanyika huko Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia na kufanya majadiliano na viongozi wa nchi hizo kuhusu hali ya Lebanon na Iraq, hata sehemu nzima ya Mashariki ya kati.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-23