Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-26 19:52:33    
Ban Ki-moon na Rice watembelea Palestina na Israel kwa wakati mmoja kuhimiza mazungumzo ya amani

cri

Tarehe 25 katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-moon na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice walioko ziarani kwenye sehemu ya mashariki ya kati kwa mbalimbali walitembelea Palestina, na kufanya mazungumzo na viongozi wa Israel. Vyombo vya habari vimeona kuwa, lengo la watu hao wawili kutembelea Palestina na Israel ni kuhimiza mazungumzo ya amani kati ya pande hizo mbili. Lakini kutokana na kuwa viongozi wa Palestina na Israel wanachukua msimamo tofauti kuhusu suala la kuwaachia huru wafungwa, hivyo matokeo ya juhudi zao bado ni vigumu kukadiriwa.

Palestina ni kituo cha kwanza cha ziara ya katibu mkuu Ban Ki-moon katika sehemu ya mashariki ya kati, tarehe 25 alifanya mazungumzo na mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bwana Mahmoud Abbas huko Ramallah. Baadaye Bi Rice aliyemaliza ziara yake nchini Misri alifika Ramallah kufanya mazungumzo na Bw. Abbas. Halafu Bw. Ban Ki-moon na Bi. Rice walifanya mazungumzo mafupi mjini Jerusalem. Kutokana na mpango uliowekwa, viongozi hao wawili tarehe 26 kwa nyakati tofauti watafanya mazungumzo na waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert.

Watu hao wawili wote wanatumai kutafuta njia ya kuhimiza mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel kwenye hali mpya ya kuundwa kwa serikali ya muungano wa kitaifa ya Palestina na nchi za kiarabu kuandaa mkutano wa wakuu ili kujadili hali mpya ya mchakato wa amani ya Palestina na Israel.

Bw. Ban Ki-moon na Bi. Rice wanapojitahidi kusukuma mbele mchakato wa amani ya mashariki ya kati, pia wanakiri kuwa ni vigumu kupata maendeleo yaliyo dhahiri kwa hivi sasa. Serikali mpya ya Palestina haiwezi kutimiza masharti matatu yaliyotolewa na pande nne husika kuhusu suala la mashariki ya kati, yaani kuitambua Israel, kuacha matumizi ya mabavu na kutambua mikataba iliyosainiwa kati ya Palestina na Israel, waziri mkuu wa Israel Bw. Olmert ameeleza kidhahiri kususia serikali mpya ya muungano wa kitaifa ya Palestina, na kukataa kufanya mazungumzo ya aina yoyote kati yake na Palestina. Hivyo Bw. Ban Ki-moon amesema kuwa, wakati wa kufanya mazungumzo na maofisa wa kundi la HAMAS bado haujawadia. Naye Bi. Rice amekiri kuwa hivi sasa wakati wa kutimiza amani kwenye mashariki ya kati bado haujafika.

Lakini wakati Bw. Ban Ki-moon na Bi. Rice kujitahidi kusukuma mbele mazungumzo kati ya Palestina na Israel, pande hizo mbili zimeanza tena kulumbana. Bw. Olmert tarehe 25 kwenye mkutano wa kawaida wa baraza la mawaziri alimlaani Bw. Abbas kwa kuvunja ahadi alizotoa kwa Israel, hasa ahadi yake ya kumwachia huru askari wa jeshi la Israel aliyetekwa nyara na kundi la Hamas Bwana Gilad Shalit kabla ya kuundwa kwa serikali mpya wa Palestina. Bw. Olmert alisema kitendo cha Abbas hakitasaidia kuhimiza mazungumzo kati ya Israel na mamlaka ya utawala wa Palestina. Ofisa wa Palestina alisema kuwa Bw. Abbas siku zote zilizopita hakutoa ahadi namna hiyo, alikubali tu kujitahidi kufanikisha kuachiwa huru kwa Bw. Shalit. Siku hiyo hiyo Bw. Abbas alisema Israel inapaswa kuzingatia kuwaachia huru wapalestina waliofungwa. Waziri wa habari wa Palestina alimlaani Bw. Olmert kwa kuielekeza kwa makosa jumuiya ya kimataifa na watu wa Israel. Alisema Israel inawajibika kwa askari Shalit kuchelewa kuachiwa huru, kwa sababu Israel haikuzingatia kwa makini pendekezo la Palestina la kubadilishana wafungwa. Malumbano kati ya viongozi wa Palestina na Israel bila shaka yametia mashaka juhudi za Bw Ban Ki-moon na Bi. Rice za kusukuma mbele mchakato wa amani ya pande hizo mbili.