Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-27 15:11:44    
Barua 07/03/27

cri
Msikilizaji wetu Ras Franz Manko Ngogo wa klabu ya wasikilizaji wa CRI Kemogemba, Tarime Mkoani Mara nchini Tanzania, anasema anayo heshima na taadhima kutuarifu kuwa, idhaa ya Kiswahili hadi sasa imekuwa ni mtandao mkubwa wa usikivu na inapendwa na wasikilizaji wa Afrika ya mashariki. Hana budi kutoa shukrani zake mara dufu kwa kuwekewa saa nzima ya matangazo ya makala kutoka China kupitia Radio ya Kenya ya KBC ambayo inasikika vizuri huko Tarime na kusikilizwa hata na kina mama wa nyumbani ambao hawawezi kunasa masafa ya FM ambayo huhitaji radio za kisasa.

Kabla ya kuhitimisha barua yake Bwana Manko Ngogo anapenda kutoa pongezi kwa ubora wa vipindi vya Radio China Kimataifa vinavyotoa hamasa, hususani kipindi cha jumapili 26 mwezi Februari. Anakumbuka kuwa kipindi hicho cha daraja la urafiki kati ya China na Afrika kilielezea jinsi madaktari wa China wanavyoisadia Tanzania. Aliguswa sana aliposikia ustadi wanaoutumia madaktari wa China ambao hata wameweza kuwatibu viongozi wakubwa wa Tanzania ikiwa ni pamoja na Rais mstaafu wa Tanzania Ndugu Benjamini Mkapa.

Anapenda kutoa pongezi kwa madaktari wa China na anasema wanamkumbusha miaka ya 70 ambapo yeye mwenyewe alishuhudia huduma zao, wakati huo akiwa na umri wa miaka 10. Mwisho anamaliza barua yake kwa kuipongeza Radio China kimataifa kwa juhudi kubwa za kuwajulisha wasikilizaji mambo mbalimbali yanayotokea duniani na yanayotokea China na hata na hata barani Afrika.

. Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Franz Manko Ngogo kwa barua yake, Bwana Ngogo ni shabiki wa matangazo ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, kila mara anasikiliza kwa makini sana na hata alishiriki kwenye mashindano ya chemsha bongo kwa juhudi kubwa katika miaka mfululizo ya hivi karibuni, kila baada ya kushiriki chemsha bongo, anatuletea maelezo yake mazuri yanayotutia moyo. Hapa tunataka kumwambia kuwa, hivi karibuni tumemtumia barua pepe ya kumtaka atufahamishe mambo fulani, tafadhali tunamuomba ajitahidi kutujibu haraka.

Msikilizaji wetu Dominic Ndukis Mishoro wa S. L.B 1990 Kakamega nchini Kenya, anatoa salamu kwa wafanyakazi wote wa Idhaa ya Kiswahili ya radio Kimataifa, pia anapenda kutufahamisha kwamba yeye pamoja na wasikilizaji wenzake wanayapokea matangazo yetu vizuri sana nchini Kenya kupitia vituo vya matangazo vya KBC na kituo cha FM cha Radio China Kimataifa kilichopo Jijini Nairobi, ambacho ni kituo cha kwanza barani Afrika. Msikilizaji huyu anaiomba Radio China kimataifa iendelee kujenga vituo vingine vya FM katika sehemu mbalimbali duniani, anasema vituo hivyo vitazidi kudumisha mawasiliano na maelewano kati ya China na nchi mbalimbali.

Bwana Ndukis anasikitika kusema kuwa watu wa magharibi mwa Kenya hawayapati matangazo ya FM kwa sababu matangazo hayo kutoka kituo cha CRI Nairobi hayafikii huko, hivyo anaomba idara husika zilifanyie kazi tatizo hilo. Anaomba kama kuna uwezekano Radio China kimataifa ijenge vituo vya matangazo vya FM katika miji ya Eldoret, Kisumu na Kakamega ili wasikilizaji waweze kupata matangazo bora na usikivu mzuri

Kabla ya kuhitimisha barua yake, anaiomba Radio China kimataifa iongeze muda wa matangazo katika kipindi cha salamu zenu ili kuwezesha kadi nyingi zaidi za wasikilizaji zisomwe. Pia anaomba atumiwe kitabu chenye ratiba ya vipindi vya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa na chenye picha za watangazaji, anasema anawashukuru wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa kwa kazi nzuri pamoja na uhusiano mwema usio na ubaguzi. Anakamilisha barua yake kwa kuwapongeza wasikilizaji wote wa Radio China kimataifa, akisema wasivunjike moyo kwani Radio China kimataifa inawajali wasikilizaji wake wote.

Msikilizaji wetu Kuleba Robert Kadidi Musiba wa S.L.B 4, Namanyere-Nkasi mkoani Rukwa nchini Tanzania, anatumaini kwamba wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa ni wazima na wanaendelea vyema na kazi ya upashanaji habari. Yeye huko nchini Tanzania ni mzima na anaendelea na shughuli zake za kila siku huku akiitegea sikio idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa.

Anasema lengo la barua yake ni kutoa shukrani kwa barua aliyoipata tuliyomwandikia tarehe 30/05/ 2006 na anatushukuru sana kwa kumkumbuka. Anasikitika kuwa kwa kipindi kirefu hajawasiliana na sisi kwa kuwa alikuwa nje ya makazi yake kwa muda mrefu hivyo ilikuwa vigumu kwake kupata barua. Bwana Musiba anasema kutokana na matangazo yetu kutosikika vizuri kwa baadhi ya nyakati huko aliko, angependa kutumiwa makala zinazohusu mashindano ya chemsha bongo ili aweze kwenda sambamba na wasikilizaji wenzake ambao wanapata matangazo vizuri kila siku.Mwisho anatutakia kazi njema wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya radio china Kimataifa.

Tunamshukuru sana Bwana Kuleba Robert Kadidi Musiba kwa barua yake na moyo wake wa dhati. Kuhusu matangazo yetu ambayo bado hayawezi kusikika vizuri katika sehemu fulani fulani nchini Tanzania, tunaendelea na juhudi zetu, tunaomba wasikilizaji wetu watuelewe na kuvumilia, kwani sisi wafanyakazi tunafanya juhudi, lakini matokeo ya haraka hayawezi kuamuliwa na sisi, sisi tunafanya juhudi kadiri tuwezavyo.

Msikilizaji wetu mwingine Bw Kennedy Nehemeiah wa S.L.B 636 Bungoma nchini Kenya, yeye ametuandikia barua akiomba kuwa mwanachama wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa.

Tunakukaribisha sana Bwana Nehemeiah katika idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Ni matumaini yetu kuwa utaendelea kusikiliza vizuri matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali yatakayosaidia kuboresha vipindi vyetu.

Msikilizaji wetu Mniko Paul wa S.L.B 5034 Dar es salaam nchini Tanzania, ametuandikia barua akianza kwa salamu kwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio china Kimataifa. Anaishukuru sana idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kwa juhudi zake katika kuwasiliana na wasikilizaji wake wote bila ubaguzi, yeye binafsi anatoa pongezi kwa Radio China kuhakikisha kuwa kila mwanachama anapata kile anachotarajia kutoka kwenye matangazo yetu. Anasema Chemsha Bongo za Radio China kimataifa kwa wasikilizaji zinawafanya wawe makini katika kufuatilia vipindi vyote. Anapenda kutoa ushauri kuwa, kadri matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa yanavyozidi kuboreshwa, anaomba hata vituo vya matangazo katika nchi mbalimbali pia vingeongezwa na hata muda wa matangazo nao pia ungeongezwa. Mwisho atashukuru sana kama atapata nafasi ya kuitembelea China siku moja.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Mniko Paul kwa barua yake, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo, ingawa nafasi za kuchaguliwa kuwa msikilizaji mshindi atakayekuja kuitembelea China ni chache, lakini tunaamini kuwa mmoja mmoja kati ya wasikilizaji wetu hakika watapata bahati ya kuchaguliwa.

Msikilizaji wetu Joel Ngoko wa S.L.B 1246 Kisii Nchini Kenya, anatoa salamu nyingi kwa watangazaji wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, anasema bado anaendelea kuyapata vizuri matangazo yetu kupitia KBC. Anasema alikuwa na matumaini makubwa ya kushinda katika shindano la chemsha bongo lakini kwa bahati mbaya hakufanikiwa, lakini bado hajakata tamaa na ataendelea kushiriki katika chemsha bongo nyingine ili aweze kupata nafasi ya kuitembelea China nchi anayoipenda, ambayo uchumi wale unakuwa kwa kasi na yenye urafiki wa jadi na Afrika. Ni matumaini yake kuwa siku moja atashinda chemsha bongo na atapata nafasi ya kuzuru nchini China pamoja na kisiwa chake cha Taiwan ili aweze kukaa na marafiki wa kichina walau kwa wiki moja.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-27