|
Kuanzia tarehe 27 jeshi la baharini la Marekani lilianza kufanya luteka katika Ghuba ya Uajemi. Hiyo ni luteka kabambe kabisa katika Ghuba hiyo tokea vita vya Iraq zianze mwaka 2003. Kutokana na kuwa mazoezi hayo yanafanyika katika wakati nyeti ambapo Iran imewakamata askari wa Uingereza na pande mbili kati ya Iran na Uingereza haziafikiani, luteka hiyo inafuatiliwa sana.
Tarehe 27 manowari mbili za kubeba ndege pamoja na ndege zaidi ya mia moja na askari zaidi ya elfu kumi walishiriki kwenye luteka hiyo.
Kutokana na kuwa ni siku tano zimepita tokea Iran iwakamate askari wa Uingereza, luteka hiyo inafanyika karibu na eneo la bahari ya Iran kwa maili 12 tu, na luteka hiyo inalenga kupiga manowari na ndege za "adui" pamoja na nyambizi zenye makombora, vyombo vya habari vinaona kuwa hii ni "ishara fulani" ya jeshi la Marekani kwa Iran. Lakini tarehe 27 amiri jeshi wa luteka hiyo Bw. Kevin Aandahl alikataa ubashiri huo, alisema, luteka hiyo haina uhusiano wowote na tukio la askari wa Uingereza kukamatwa, na Marekani haina nia ya kuitishia Iran, na lengo la luteka hiyo ni "kwa ajili ya kulinda utulivu na usalama wa kanda hiyo". Lakini alionya kuwa kama kanda hiyo ikikumbwa na hali ya wasiwasi, hakika wasiwasi huo unasababishwa na Iran.
Jambo linalostahili kutiliwa maanani ni kuwa manowari pekee ya Ufaransa yenye kubeba ndege ya Charles de Gaulle hivi karibuni pia iliingia kimya kimya kwenye sehemu ya Ghuba na kujiunga na nguvu za kijesi za Marekani na kufanya manowari kwenye sehemu hiyo ziwe nne.
Vyombo vya habari vinasema, ingawa nguvu za kijeshi za Marekani na Ufaransa zimeungana na Uingereza imetangaza kuwa itaunda kikosi cha dharura kuwaokoa askari wake katika wakati unaofaa, lakini hali hiyo haimaanishi kuwa hakika vita vitatokea katika sehemu ya Ghuba ya Uajemi.
Kwanza, msukosuko kama huo wa kidiplomasia kati ya Iran na Uingereza umewahi kutokea miaka mitatu iliyopita wakati rais wa Iran Bw. Mohammad Khatami alipokuwa madarakani. Wakati huo Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zilifanya mazungumzo na serikali ya Khatami, na mazungumzo hayo yalipata mafanikio bila ya kuufanya msukosuko uwe mbaya, na askari wanane wa Uingereza waliokamatwa waliachiliwa huru. Kuhusu msukosuko wa sasa ingawa tarehe 27 waziri mkuu wa Uingereza Bw. Blair alisema kama Iran haitawaachia huru askari wake baada ya mazungumzo, Uingereza itachukua "hatua nyingine". Lakini kauli hiyo ni kama tishio tu la kidiplomasia na wala haimaanishi kuwa kweli Uingereza itaanzisha vita dhidi ya Iran. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza tarehe 27 pia alisisitiza kuwa kutatua suala la wanamaji wa Uingereza waliokamatwa kuna manufaa kwa pande zote mbili.
Pili, kushiriki kwenye nguvu za kijeshi za Marekani katika sehemu ya Ghuba ya Uajemi hakumaanishi kuwa Ufaransa itafuata sera kali za Marekani. Kutokana jinsi Ufaransa inavyopinga vita dhidi ya Iraq, watu wanaelewa kuwa wakati Ufaransa inaposhirikiana na Marekani haitapoteza uhuru wake. Kwa hiyo Ufaransa haitashiriki kwenye operesheni ya kijeshi dhidi ya Iran.
Tatu, wachambuzi wanaona kuwa hivi sasa Marekani imeweka askari wake laki 1.73 katika sehemu ya Ghuba, idadi hiyo ni karibu sawa na idadi ya askari kabla ya kuanza kwa vita dhidi ya Iraq, lakini hivi sasa Marekani bado haijapata kisingizio cha kuanzisha vita dhidi ya Iran.
Nne, nia ya Iran kuwakamata askari wa Uingereza ambayo ni nchi rafiki wa Marekani sio kutaka kuanzisha vita, kwa nje suala hilo linaonesha kama Iran inagongana na Uingereza, lakini kwa undani ni kuwa Iran inapambana na Marekani, na inatoa ishara kuwa kuiwekea vikwazo hakutasaidia kitu, na katika suala la nyuklia Iran ina hatua zake dhidi ya vikwazo.
Kwa ufupi, hivi sasa Iran iko kwenye njia panda, kuweza au kutoweza kutatua suala la kuwakamata wanamaji 15 wa Uingereza kunategemea jinsi kila upande utakavyorekebisha msimamo kufuatia hali itakavyokuwa, lakini Marekani na Uingereza hazina nia ya kuanzisha vita dhidi ya Iran.
Idhaa ya kiswahili 2007-03-28
|