Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-03-29 15:49:17    
Mbinu ya kuongeza mapato ya wakulima wa China

cri

Maelezo ya leo yanamhusu mkulima mmoja anayejulikana kwa jina kaka Niu, Niu maana yake ya Kichina ni ng'ombe, ambaye anaishi huko Shuangxi, kitongoji cha mji wa Hangzhou, mji maarufu wa utalii uliopo mashariki mwa China. Katika miaka ya hivi karibuni, shughuli za utalii kwenye maskani ya kijana huyo zimeendelezwa sana, ambapo yeye na wakulima wenzake wamepata mbinu mpya ya kuongeza mapato.

Huko Shuangxi misitu ya mianzi inaonekana kila mahali. Kuna mito midogo yenye maji safi na hewa safi, sehemu hiyo inajulikana kwa kuwa na mandhari nzuri. Nyumba ya kijana huyo iko Shuangxi, na kazi yake ni kuendesha mkokoteni unaovutwa na ng'ombe kwa watalii. Kila asubuhi anachunga ng'ombe akiendesha gari moja jeupe, ambalo alinunua kwa pesa alizochuma kutokana na kuendesha mkokoteni huo. Bwana huyo anajivunia uhodari wake wa kufuga ng'ombe. Alisema "Liu, liu, liu. Natamka hivyo kama nikitaka ng'ombe aelekee upande wa kulia. Ng'ombe wangu anaweza kukimbia kwa kasi kama farasi, pia anaweza kwenda polepole kama wazee. Ana ngozi laini. Angalia, unaonaje ngozi yake?"

Kaka Niu ni mkulima, jina lake ni Zhang Ronggen. Alipewa jina la Kaka Niu na jamaa na wanakijiji wenzake kutokana na uhodari wake katika kufuga ng'ombe. Tangu zamani watu wa China walikuwa wanatumia sana ng'ombe katika shughuli za kilimo. Lakini katika miaka ya hivi karibuni kutokana na maendeleo ya kiuchumi na kisayansi, wakulima wa China wanatumia zaidi mitambo mbalimbali ya kilimo, na kilimo cha jadi cha kutumia maksai kinapotea hatua kwa hatua. Kaka NIu akiwa na wasiwasi na ng'ombe, aliona watu waliokuja kutalii kwenye maskani yake wanaongezeka siku hadi siku, wazo moja likamjia kuwa, shughuli za utalii huenda itakuwa ni mbinu nzuri ya kuongeza mapato.

Hapo baadaye kampuni moja ya utalii ilianzishwa kwenye maskani ya kijana huyo. Mtalii mmoja kutoka mji wa Shanghai Bibi Zhou Wen alivutiwa na mandhari ya Shuangxi, akisema "Hapa hakuna majengo ya kisasa, ni mandhari ya asili tu, pia kuna mito, napapenda sana."

Shuangxi ina sifa za kijiogrofia ya kuwa karibu na miji mikubwa ya Hangzhou na Shanghai, kwa hiyo ina msingi mzuri wa kuendeleza shughuli za utalii. Mbali na mandhari nzuri, shuangxi pia ni mji mdogo wenye historia zaidi ya miaka elfu moja na una mabaki ya kiutamaduni. Sifa hizo zinawavutia watalii wengi. Lakini katika kanda hiyo pia kuna miji midogo mingine inayofanana na Shuangxi, lakini je mji huo unawezaje kuwavutia watalii wengi zaidi?

Kampuni ya utalii ya Shuangxi iliwahamasisha wafanyakazi wake wachemshe bongo na kutafuta mbinu maalumu. Wakati huo huo kijana huyo alikumbuka maneno aliyosema mtalii mmoja kutoka Shanghai. "Mtalii mmoja wa Shanghai alikuja akisema, nimewahi kupanda gari na ndege isipokuwa mkokoteni unaovutwa na ng'ombe, kwa hiyo nataka kujaribu kupanda mkokoteni unaovutwa na ng'ombe."

Huduma za safari ya mikokoteni inayokokotwa na ng'ombe haziwezi kupatikana bila kuwepo Kaka Niu. Kwa hiyo kampuni ya utalii ilikodi ng'ombe wake na kumwalika ajiunge na kampuni hiyo. Kaka huyo aliacha shughuli za kilimo na kuanza kujishughulisha na kuendesha mkokoteni unaovutwa na ng'ombe kwa ajili ya watalii. Ng'ombe walipewa kazi mpya, na kaka huyo mwenye ng'ombe na wakulima wenzake wenye ng'ombe pia walipata ajira mpya. Watalii wakifika Shuangxi, wanaacha magari na mabasi na kupanda mikokoteni inayovutwa na ng'ombe na kushuhudia maisha ya vijijini kwenye njia nyembamba za vijijini.

Kupanda mikokoteni inayovutwa na ng'ombe kunawavutia watalii wengi siku hadi siku. Meneja mkuu wa kampuni hiyo ya utalii Bw. Wang Banglin alisema "Mwaka 2000 tulipoanza kutoa huduma hiyo, ni watalii elfu kumi kadhaa tu walishiriki kwenye safari za kupanda mikokoteni inayovutwa na ng'ombe mwaka huo. Hivi sasa safari hizo zinawavutia watalii kati ya laki 6 na laki 7 kwa mwaka."

Kutokana na kuchapa kazi kwa miaka kadhaa, Kaka Niu alipata akiba kwa kiasi fulani, akanunua gari moja jeupe kwa kutumia fedha hizo, na maisha yake yakabadilika kabisa.

Wanakijiji wenzake wengi pia walipata uwezo baada ya kuanza kujishughulisha na utalii. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na ongezeko la idadi ya watalii, kampuni ya utalii ya Shuangxi pia inapanuka siku hadi siku. Wanakijiji wengi walioshuhudia mafanikio ya kaka huyo mwenye ng'ombe, pia walijiunga na kampuni ya utalii na kujishughulisha na kuendesha mikokoteni inayovutwa na ng'ombe, jambo ambalo liliongeza mapato yao.

Wakulima kadhaa walieleza kufurahia. Mkulima mmoja alisema  "Mwanzoni tulipojishughulisha na sekta ya utalii, kulikuwa na watalii wachache sana, ilikuwa nadra kuja kwetu kwa mabasi makubwa ya utalii, wakati ambapo tulifurahi sana tukiona magari madogo kuja. Hivi sasa mabasi mengi yanakuja, hali ambayo tulikuwa hatuitarajii."

Mkulima mwingine alisema  "Kama tungekuwa tunafanya shughuli za kilimo tu, tusingeweza kuchuma pasa nyingi namna hii."

Maendeleo ya sekta ya utalii yameongeza uwezo wa wakazi wa Shuangxi, ambapo familia nyingi zimejenga nyumba mpya nzuri. Hivi karibuni ujenzi wa mtaa mmoja wa makazi huko Shuangxi ulikamilika, na Kaka Niu alinunua nyumba kwenye mtaa huo. Nyumba hiyo ni kubwa na nzuri inayofanana na nyumba za mijini, na kwenye mtaa huo wa makazi pia kuna bustani. Hapo awali kijana huyo alikuwa maskini kiasi kwamba aliwahi hata kuishi kwenye zizi la ng'ombe, alikuwa hatarajii kuwa siku moja atamiliki nyumba hiyo.

Baada ya gari na nyumba, kijana huyo alianza kufikiria kuanzisha shughuli zake mwenyewe. Hivi karibuni alianza kufanya biashara ya maua, akipanda maua na miche ya miti kwenye mashamba yake na kuyauza sokoni. Kutokana na maendeleo ya sekta ya utalii, maua yanahitajika sana kwenye mahoteli, sehemu za vituvio vya utalii na mitaa ya makazi huko Shuangxi, kwa hiyo kijana huyo anaona biashara ya maua ina mustakabali mzuri na kuamua kujishughulisha na biashara hiyo.

Alisema "Wenzangu wanapenda kununua , ninauza maua kwenye masoko mbalimbali, pia nimetekeleza miradi kadhaa midogo ya ujenzi wa bustani."

Katika miaka ya hivi karibuni, kijana huyo aliyekuwa mfuga ng'ombe ameshuhudia mambo mengi ambayo hapo awali hakuyatarajia. Sekta ya utali si kama tu ilimpatia nafasi ya ajira, bali pia alimfanya mkulima huyo awe na shughuli zake mwenyewe.

Idhaa ya kiswahili 2007-03-29