|
Mkutano wa 19 wa siku mbili wa wakuu wa nchi wa Umoja wa Nchi za Kiarabu unaofanyika kwa siku mbili ulianza tarehe 28 mwezi Machi huko Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia, viongozi wa nchi za kiarabu wanaoshiriki kwenye mkutano huo wameahidi kutatua migogoro ya sehemu ya mashariki ya kati kwa njia ya kidiplomasia.
Wakuu wa nchi, viongozi wa serikali au wawakilishi wao kutoka nchi wanachama 22 wa Umoja wa Nchi za Kiarabu pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon na mwakilishi wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia sera za kidiplomasia na usalama Bw. Javier Solana walishiriki kwenye mkutano wa siku hiyo. Ajenda muhimu za mkutano huo wa wakuu ni pamoja na mchakato wa amani wa mashariki ya kati, mgogoro kati ya Palestina na Israel, hali ya Iraq, mgogoro wa kisiasa nchini Lebanon na suala la Darfur la Sudan. Washiriki wa mkutano wanatumai kuwa wataweza kuondoa tofauti kati yao, kusuluhisha maoni na misimamo yao, na kukabiliana na tishio na changamoto dhidi ya usalama wa sehemu ya mashariki ya kati.
Kuhusu mchakato wa amani ya mashariki ya kati, viongozi wa nchi za kiarabu wanaoshiriki kwenye mkutano siku hiyo walipitisha azimio likithibitisha ahadi zote walizotoa katika "pendekezo la amani la waarabu" lililopitishwa na mkutano wa wakuu wa nchi za kiarabu uliofanyika mwaka 2002 huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon, azimio linatoa wito tena kutaka serikali na watu wa Israel kukubali pendekezo hilo, kutumia nafasi hiyo na kuanza upya kwa mazungumzo ya moja kwa moja. Mkutano huo pia umeamua kuanzisha vikundi kadhaa kuwasiliana kwa nyakati na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, baraza usalama la Umoja wa Mataifa "pande nne kuhusu suala la mashariki ya kati" ambazo ni Marekani, Umoja wa Ulaya, Russia na Umoja wa Mataifa ili kutafuta uwezekano wa kurejesha mazungumzo ya amani.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon alipotoa hotuba kwenye ufunguzi wa mkutano siku hiyo, alipongeza sana "pendekezo la amani la waarabu". Alisema pendekezo hilo ni moja ya nguzo za mchakato wa amani ya mashariki ya kati, na limeonesha kuwa, nchi za kiarabu zinatafuta kwa makini njia ya kuleta amani na utulivu wa sehemu ya mashariki ya kati. Katibu mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu Bw. Amr Moussa katika hotuba aliyotoa siku hiyo, aliihimiza Israel ikubali "pendekezo la amani la nchi za kiarabu" linalokusudia kuzindua upya mchakato wa amani ya sehemu ya mashariki ya kati.
Kuhusu suala la Palestina na Israel, viongozi wa nchi za kiarabu wanaoshiriki kwenye mkutano huo wametaka kuondoa haraka iwezekanavyo vikwazo vya kiuchumi na kisiasa dhidi ya watu wa Palestina. Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia, ambayo ni nchi inayoandaa mkutano huo, akitoa hotuba kwenye ufunguzi wa mkutano alisema ni lazima kuondoa haraka iwezekanavyo vikwazo visivyo vya haki dhidi ya watu wa Palestina. Kwani mchakato wa amani ya mashariki ya kati hauwezi kuhimizwa bila kuondokana na ukandamizaji na matumizi ya nguvu. Waziri mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa wa Palestina ambaye pia ni kiongozi wa kundi la upinzani la Hamas Ismail Haniya ametaka mkutano wa wakuu wa nchi za kiarabu usilegeze masharti kwa Israel kuhusu suala la haki ya wakimbizi wa Palestina ya kurejea nyumbani.
|