|
Balozi mpya wa Marekani nchini Iraq Bw. Ryan Crocker tarehe 29 aliapishwa chini ya ulinzi mkali mjini Baghdad. Katika siku hiyo hiyo katika sehemu ya Khalis, kaskazini ya Baghdad, ilitokea milipuko mingi na kusababisha vifo vya watu 107 na wengine zaidi ya 130 kujeruhiwa. Wachambuzi wanaona kuwa ingawa usemi ambao "mwaka 2007 ni mwaka wa kuamua vita vya Iraq" unakubaliwa na watu wengi, lakini ni vigumu kusema kama balozi huyo ataweza kusaidia chochote kuibadilisha hali mbaya nchini Iraq.
Bw. Ryan Crocker ana umri wa miaka 57, ni mwanadiplomasia mzoefu. Alianza kuwa balozi wa Marekani nchini Pakistan mwaka 2004. Baada ya Marekani kuiteka Iraq alikuwa ni mtu anayeshughulikia mawasiliano kati ya serikali ya Marekani na serikali ya muda ya Iraq. Rais George Bush anaona kuwa yeye anafahamu zaidi utamaduni na lugha ya kanda hiyo, akiwa pamoja na uzoefu wa zaidi ya miaka 30, mtu huyo anafaa zaidi kuwa balozi nchini Iraq.
Kwenye sherehe ya kuapishwa, Bw. Crocker alisisitiza kuwa hivi sasa suala la usalama nchini Iraq ni suala kuu linaloikabili Marekani, magaidi na watu wenye silaha wanaendelea kuutishia usalama wa Baghdad na nchi nzima ya Iraq, na hii ni changamoto ya kihistoria. Ameitaka serikali ya muda ya Iraq ichukue hatua zote za lazima kuleta umoja wa taifa la Iraq.
Siku ya kuapishwa kwa Bw. Crocker pia ni siku mbaya kabisa ya umwagaji damu katika muda wa karibuni uliopita nchini Iraq. Katika siku hiyo ya tarehe 29, mabomu mengi ya kujiua yalilipuka katika mji wa Baghdad na kwenye soko moja la mji wa Khalis, kaskazini ya Baghdad, na kusababisha watu zaidi ya 200 kupoteza maisha na kujeruhiwa. Hii inaonesha kuwa migogoro kati ya madhehebu ya kidini bado inaendelea na kuongezeka, na haina dalili yoyote kupungua, majeshi ya muungano yanayoongozwa na Marekani sasa yako mbioni kushughulika na matukio hayo.
Zaidi ya hali hiyo, Bw. Crocker anakabiliwa na changamoto za aina tatu.
Kwanza, namna ya kushughulikia uhusiano kati yake na madhehebu ya Shia na Suni ni tatizo gumu. Katika muda mrefu uliopita serikali ya Marekani ilikuwa inatumia sera za aina mbili za ukali na upole kwa madhehebu ya Suni na Shia, lakini haikuwa na dawa yoyote kutuliza migogoro kati ya madhehebu hizo mbili.
Pili, nchi za Mashariki ya Kati zinazidi kupiga kelele za kutaka Marekani iondoe jeshi lake kutoka Iraq. Tarehe 28 mfalme wa Saudi Arabia kwenye mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika alizitaka nchi za Kiarabu ziungane pamoja na kuzuia nguvu za nje kudhibiti mustakabali wa kanda hiyo. Saudi Arabia ni nchi mshirika muhimu wa Marekani katika kanda ya Mashariki ya Kati, kauli ya mfalme huyo inaonesha kuwa Marekani imetengwa zaidi kutokana na kuwepo kwa jeshi la Marekani nchini Iraq. Kwa hiyo namna ya kufanya uhusiano uwe mzuri kati ya Marekani na nchi jirani za Iraq, hasa Iran, pia ni tatizo gumu linalomkabili Bw. Crocker.
Tatu, shinikizo nchini Marekani la kutaka kuondoa jeshi kutoka Iraq limekuwa likiongezeka siku hadi siku. Gazeti la USA Today tarehe 27 lilitangaza uchunguzi wake kuhusu maoni ya raia kwamba 56% ya Wamarekani wanaona ni kosa la Marekani kuanzisha vita dhidi ya Iraq, kiasi hicho kimeongezeka kwa 33% ikilinganishwa na miaka minne iliyopita, na 60% ya watu wa Marekani wanaunga mkono bunge la Marekani kuweka ratiba ya kuondoa jeshi la Marekani. Baraza la juu la bunge la nchi hiyo linalodhibitiwa na Chama cha Democrat tarehe 29 lilipitisha sheria ya kutenga fedha kwa ajili ya jeshi la Marekani ikiwemo ratiba ya kuondoa jeshi hilo. Pamoja na kukubali kutenga dola za Kimarekani bilioni 120 sheria hiyo pia inataka jeshi la Marekani liwe limeondolewa kabisa nchini Iraq tarehe 31 Machi mwaka 2008. Sheria hiyo ilipitishwa na baraza la chini la bunge la Marekani, lakini haitatekelezwa mpaka rais aidhinishe. Hata hivyo, hali hiyo inaonesha kuwa shinikizo la kutaka Marekani iondoe jeshi lake kutoka Iraq linazidi kuongezeka kila kukicha, na ugumu wa kazi ya balozi mpya Bw. Crocker utazidi kuwa mkubwa.
Idhaa ya kiswahili 2007-03-30
|