Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-02 15:22:24    
Mwigizaji mashuhuri wa tamthilia ya kuchekesha Huang Hong

cri

Mwigizaji wa tamthilia ya kuchekesha Bw. Huang Hong anajulikana sana kwa sababu ya kuzingatia sana haki na maslahi ya wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini, na anasifiwa kuwa ni "msemaji wa wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini".

Kuanzia tarehe 3 hadi 15 Machi mkutano wa kila mwaka wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China ulikuwa ukifanyika mjini Beijing. Wajumbe wa baraza hilo wote ni wataalamu katika sekta mbalimbali, wao wanashiriki kwenye mambo ya kisiasa kwa kuishauri. Mjumbe wa baraza hilo Bw. Huang Hong mwenye umri wa miaka 47, kwenye mkutano huo alitoa pendekezo la "wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini wapatiwe mfumo wa uhakikisho wa kijamii". Pendekezo hilo lilipotolewa tu mara lilifuatiliwa sana na vyombo vya habari. Pendekezo hilo linahusiana na hadhi ya wakulima, mishahara yao, bima na maisha yao ya utamaduni katika miji.

"Tamthilia nilizoigiza karibu zote zinaeleza mambo ya watu wadogo katika jamii. Nilifahamu matatizo yao nilipokusanya habari miongoni mwao katika maeneo ya ujenzi. Naona wakulima hao wanaofanya kazi za vibarua mijini wanazidi kuwa kundi muhimu katika jamii, na katika sekta za ujenzi, mikahawa na viwanda wakulima hao wanachukua zaidi ya nusu ya wafanyakazi wote wa sekta hizo. Hapo kabla nilionesha tu mambo yao katika michezo ya sanaa lakini sasa nikiwa mjumbe wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa inanipasa nibebe majukumu mengine."

Tamthilia za kuchekesha alizoigiza zinavutia kwa maana yake kubwa ya undani. Yeye ni hodari kuonesha matatizo ya kijamii kwa kuonesha mambo ya makabwera.

Maisha ya mijini na ya vijijini ya tofauti kubwa, baada ya wakulima kuingia mijini wanakumbwa na matatizo na mambo mengi ambayo ni mageni kwao. Tamthilia za Huang Hong zinaonesha maisha yao ya furaha na yenye chungu, na watazamaji wanasikitishwa baada ya kucheka. Bw. Huang Hong alipotaja tamthilia zake alisema,

"Michezo ya sanaa ni lazima ioneshe hisia zako za kweli, hatuelewi sana maisha ya wakulima wanaoishi vijijini, lakini maisha ya wakulima wanaofanya kazi mjini walioko pembezoni mwangu, kama yaya na walinzi wa sehemu ya makazi nayaelewa sana. Mambo yao yanayokugusa moyo usiyaache yapite. Naona wakulima hao kutoka vijijini wanavutia sana kwa sababu watu hao hawana unafiki na ni wakarimu na hawana ubinafsi. Unapozungumza nao unafurahia uwazi wao na wakijaribu kukuficha kitu wanaonekana wazi papo hapo, unaweza kufahamu kila kitu mioyoni mwao. Kwa hiyo watu kama hao wanaponigusa moyo ni lazima nishike kalamu kuwaandikia katika tamthilia yangu."

Bw. Huang Hong licha ya kuandika na kuigiza tamthilia za kuchekesha, naye pia aliwahi kuhariri na kuigiza katika filamu yake ya "Baba Mmoja na Watoto Ishirini na Tano". Filamu hiyo imetengenezwa kwa mujibu wa hadithi ya kweli, inaeleza kuwa mhusika mkuu Zhao Guang alikuwa mtoto yatima na alilelewa na kuwa mtu mzima kutokana na msaada wa wenyeji wenzake. Kutokana na juhudi zake, baadaye alitajirika. Alipodadisiwa na waandishi wa habari aliahidi kuwa atakuwa baba wa watoto wote yatima, kwa hiyo watoto 25 yatima walihamia nyumbani kwake na tokea hapo maisha yake yalibadilika kabisa. Filamu hiyo inamweleza mkulima mmoja mwenye hulka ya uaminifu na wema, na kutokana na kujaa vituko vya kuchekesha filamu hiyo inavutia sana. Mwaka 2002 filamu hiyo ilipata tuzo katika mashindano ya filamu nchini China na ilipata tuzo katika maonesho ya 17 ya kimataifa ya filamu nchini Iran.

Tokea mwaka 2000 hali ya wakulima wanaofanya kazi mijini imeanza kufuatiliwa siku hadi siku nchini China. Katika sherehe ya sikukuu ya mwaka mpya wa China, Huang Hong aliigiza katika tamthilia ya kuchekesha iitwayo "ukarabati". Mkulima anayemfanyia mwenye nyumba ukarabati alisababisha mambo mengi ya ajabu ya kuchekesha katika kazi yake, mwishoni mwa tamthilia hiyo mkulima huyo kwa sauti kubwa alimwomba mwajiri wake "mishahara ya wakulima mijini isidaiwe!" Watazamaji wakayapigia sana makofi maneno hayo, kwa sababu tatizo la kudaiwa kwa mishahara ya wakulima wanaofanya kazi mijini lilikuwa kubwa wakati huo. Bwa. Huang Hong alisema,

"Naona kitu muhimu ni kuwaletea watazamaji kichekesho cha maana, na nini unachotaka kuwafahamisha kupitia tamthilia yako. Naona wasanii hodari ni lazima wawe na majukumu kwa jamii."

Bw. Huang Hong alisema tamthilia zake zote huoneshwa miongoni mwa wakulima wanaofanya kazi mijini kabla ya kuoneshwa rasmi, kama watazamaji hao wakicheka inamaanisha kuwa tamthilia yenyewe imefanikiwa.

Hivi karibuni Bw. Huang Hong ametunga tamthilia moja ya televisheni, anataka kuonesha vya kutosha maisha halisi ya wakulima hao wa mijini na kueleza kuwa, watu hao ni watu wsioweza kukosekana katika ustawi wa miji nchini China na mchango wao haufutiki.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-02