Chansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye yuko ziarani huko Mashariki ya Kati, tarehe mosi Aprili alisema Umoja wa Ulaya unapenda kuzisaidia pande mbili za Palestina na Israel katika juhudi za kuleta amani. Wachambuzi wanaona kuwa ziara hiyo ya Chansela wa Ujerumani, nchi ambayo ni mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya ina lengo la kuimarisha nguvu ya ushawishi ya umoja huo kwenye mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel, lakini ziara hiyo haikupata mafanikio halisi.
Katika wiki iliyopita waziri wa mambo ya nje wa Marekani na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa walitembelea Mashariki ya Kati kwa nyakati tofauti, wakati huo huo wakuu wa nchi za kiarabu walikutana huko Riyadh, mji mkuu wa Saudi Arabia na mada kuu ya mkutano wao ilikuwa suala la amani katika kanda ya Mashariki ya Kati. Shughuli hizo za kidiplomasia zimeleta mambo mawili, moja ni kuanzisha utaratibu wa kukutana kwa viongozi wa Palestina na Israel kila baada ya muda fulani, lingine ni kujadili kuzindua tena pendekezo la amani lililotolewa na nchi za kiarabu mwaka 2002. Kutokana na hali hiyo ziara ya Chansela Merkel ilifuatiliwa sana, kwani nchi yake sasa inauwakilisha Umoja wa Ulaya.
Siku ambayo Bibi Merkel alipoondoka Ujerumani, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya walikutana huko Bremen, Ujerumani, wakiamua kuwa umoja huo utaendelea na jitihada ili kusukuma mbele mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati. Wachambuzi wanaona kuwa kwenye ziara hiyo, kauli zilizotolewa na Chansela Merkel zinalingana na msimamo huo wa Umoja wa Ulaya. Kwamba kwa upande mmoja alisisitiza kuwa, Umoja wa Ulaya unaahidi kuhakikisha usalama wa Israel na kujitahidi kufanikisha kuachiwa huru kwa askari wa Israel aliyetekwa nyara, na kwa upande mwingine aliitaka Palestina ifuate masharti matatu yaliyotolewa na pande 4 zinazohusika na suala la Mashariki ya Kati, masharti hayo ni pamoja na kuitambua Israel, kuacha matumizi ya nguvu na kutambua makubaliano ya amani yaliyofikiwa hapo awali kati ya Palestina na Israel.
Kuhusu msimamo wa Umoja wa Ulaya uliowasilishwa na Bibi Merkel kwenye ziara hiyo, viongozi wa Palestina na Israel wameitikia kwa juhudi. Rais wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas tarehe mosi Aprili alitoa wito kwa Israel kuchukua hatua za kuitikia pendekezo la amani la nchi za kiarabu na kurejesha kwa haraka mazungumzo kati ya Palestina na Israel. Na siku hiyo hiyo, waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert pia alisema anapenda kuwaalika wakuu wa nchi za kiarabu kufanya mkutano wa amani wa kanda hiyo, wakibadilishana maoni kuhusu migogoro ya kanda hiyo na kusukuma mbele mchakato wa amani.
Hata hivyo wachambuzi wanasema pamoja na kutokea kwa hali fulani ya kufurahisha kati ya Palestina na Israel, tofauti za kimsingi kati ya pande hizo mbili bado zipo na kuna njia ndefu kabla ya kutatuliwa kwa masuala mengi halisi. Bibi Merkel alipoizuru Palestina, alikuwa na mazungumzo na Bw. Abbas tu ili kuepusha kuikasirisha Israel. Kwa upande wa Hamas, kundi hilo linaendelea kusisitiza msimamo wa kukataa kuitambulia Israel, na msimamo huo hakika haulingani na matakwa ya Umoja wa Ulaya. Kutokana na hali hii, ni vigumu kukubalika kwa ombi la Bw. Abbas la kutaka Umoja wa Ulaya uondoe vikwazo dhidi ya Palestina. Ndiyo maana wachambuzi kadhaa wanaona ziara hiyo ya Chansela Merkel haikuleta mafanikio halisi, lakini pande husika zinatakiwa kutumia ipasavyo mazingira mazuri ya sasa, kuendelea na jitihada za kusukuma mbele mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati.
|