Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-03 14:48:32    
Barua 0401

cri

Msikilizaji wetu Richard Wekesa Wekoyi wa sanduku la posta 1031 Bungoma Kenya ametuletea barua akisema kwa niaba ya wanachama wa Bwake Salamu Klabu ana furaha kubwa kututumia sote salamu na kututakia heri ya mwaka mpya wa 2007. Anasema wao huko Bungoma Kenya ni wazima na wanatushukuru kwa kazi yetu nzuri ambayo tunaendela kuifanya, na wanawashukuru wahusika wote ambao wanahakikisha kuona wasikilizaji wa Radio China kimataifa wanatumiwa bahasha zilizolipiwa stempu, anatumai kuwa tuendelea na moyo huo huo.

Anasema mwaka jana walishiriki katika shindano la chemsha bongo, lakini kwa bahati mbaya hakuna hata mmoja kati yao aliyeibuka mshindi, lakini hawajafa moyo bado wataendelea kushiriki wakiwa na matumaini ya kwamba huenda siku moja, mmoja kati yao ataibuka mshindi. Na mwisho ametuletea majina ya wasikilizaji kama wafuatao Edwin Wafula Kimalewa wa sanduku la posta 72, Chwele via Bungoma Kenya, Maurice Wetondo wa sanduku la posta 1600 Bungoma Kenya, na Protus Barasa Makila wa sanduku la posta 89 Bungeoma Kenya, anasema wasikilizaji hao wanataka kuwasilisha majina yao ili vyama vyao vya salamu viweze kutumiwa kadi za salamu.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Richard wekesa Wekoyi kwa barua yake, kama alivyosema na sisi tunawaunga mkono waendelee kushiriki kwenye shindano la chemsha bongo, kwani lipo kila mwaka. Pia Tunashukuru kwa salamu kutoka kwa wasikilizaji hao wapya na kuwatakia heri na baraka. Tunatumai kuwa baada ya kuanza mawasiliano tutaendelea kuwasiliana mara kwa mara.

Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai Falme za Kiarabu ametuletea barua pepe akisema ni furaha yake kubwa kupata nafasi hii nyingine ya kuwasiliana nasi, ikiwa pamoja na kueleza maoni yake juu ya maswala mbalimbali yanayohusu urafiki kati ya Radio China Kimataifa na wasikilizaji wake. Anasema angependa kusifu makala aliyosoma katika tovuti yetu ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, ambayo ilihusika na maelezo juu ya wakenya walivyosherehekea siku kuu ya mwaka mpya wa jadi wa China. Makala ambayo ilielezea jinsi gani wanafunzi wa Kenya walivyoshirikiana na wachina wanaoishi nchini humo katika maadhimisho ya sikukuu hiyo ya jadi, pamoja na kujifunza mengi juu ya harakati mbalimbali zinazojumuisha furaha ya kusherehekea siku hiyo adhimu kwa mamilioni ya wachina kote duniani.

Anasema kwa kweli tukio hilo ni ishara ya ushirikiano mpya wa karibu sana wa kitamaduni kati ya wakazi wa Jamhuri ya watu wa China na wakazi wa eneo la Afrika mashariki na kati. Kwani kwa maoni yake binafsi maingiliano haya ya karibu ya kitamaduni yanaweza kufungua njia nzuri zaidi ya maelewano kati ya jamii mbalimbali za kiafrika na zile za kichina. Bila shaka yoyote waafrika wana mengi ya kujifunza juu ya thamani ya utamaduni wa taifa kubwa kabisa lenye historia ndefu ya kitamaduni na kistaarabu duniani kama vile Jamhuri ya watu wa China kwa njia kama hiyo.

Anasema ni matumaini yake makubwa kwamba watu wa Jamii za Kichina pia watakuwa na hamu kubwa ya kujifunza na kuelewa vyema mila, desturi na tamaduni za jadi za jamii ya watu wa Afrika mashariki na kati, wakati kuongezeka kwa watalii na wafanyabiashara wa China wanaomiminika katika mataifa mbalimbali ya Kiafrika kunaweza kutoa nafasi nzuri zaidi ya kukuza maingiliano ya kitamaduni kati ya pande hizo mbili.

Tunamshukuru sana rafiki yetu Mbarouk Msabaha kwa barua yake ya kutuelezea mengi kutokana na usikivu wake wa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, pamoja na kusoma makala hiyo inayohusu wakenya waliosherekea mwaka mpya wa jadi wa China. Tunafurahi pia kuona wasikilizaji wetu sasa kupitia matangazo yetu, mnashuhudia kuimarika kwa maingiliano kati ya tamaduni za China na Afrika.

Msikilizaji wetu Mutanda Ayubu Shariff wa Bongoma Kenya ametuletea barua pepe akisema, ana furaha wakati huu kuweza kutuma salama zake pamoja na zile za wasikilizaji wenzake kutoka eneo la Bungoma Kenya. Na wakati huu angependa kuwafahamisha kwa njia ya barua pepe jinsi sherehe ilivyoweza kufanyika katika kijiji cha Lwanda Kaskazini mwa mji wa Bongoma, Kenya. Anasema kabla ya hapo anataka kuishukuru Idhaa ya Kiswahili kwa kuwafahamisha maana ya sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China, bila kusahau mwandishi wa habari Bwana Xie Yi wa CRI aliyeko Nairobi Kenya ambaye aliwatia moyo na kuwapa pongezi tele kwa njia ya simu na kusema amefurahia sana maandalizi hayo.

Bwana Shariff alisema, siku hiyo takriban wasikilizaji 50 walialikwa kwenye sherehe ya kuadhimisha siku kuu ya mwaka mpya wa jadi wa China tarehe 18 Februali, 2007, na zaidi ya wasikilizaji 30 waliweza kuhudhuria na wengine kutuma pongeza zao bila kusahau mamia ya watu wapendao kushangilia mchezo, ambapo waliandaliwa michezo, majadiliano, uchaguzi, vinywaji, ukaribishaji wa wageni na maktaba ndogo kufunguliwa huko Nalondo.

Hata kama sherehe ilichelewa kuanza ilikuwa ya mafanikio mema kwani lengo la mkutano liliweza kutimizwa. Karibu timu zote zilifika kwenye uwanja kwa wakati unaotakiwa. Ingawa juhudi za kupiga picha za wachezaji hazikufanikiwa, lakini mchezo wa kandanda ulichezwa vizuri sana kati ya shule za sekondari Lwanda FC na Bulondo FC, ambapo timu ya Bulondo ililazwa na Lwanda FC mabao matatu kwa moja. Wanashukuru sana mwalimu mkuu wa Lwanda Bi. Mildred Masibo na mwenzake Bwana Nelson Majimbo kwa kuwaruhusu wanafunzi wao kushiriki bila malipo na mchezo huo uliweza kuorodheshwa kwa mashindano ya shule za sekondari eneo hilo ambayo itaendelea baada ya wiki mbili.

Pia anasema mbali na michezo hiyo wasikilizaji wote waliohudhuria walipewa muda wa kujieleza na kutoa mapendekezo mbalimbali kuhusu kuimarisha usikivu wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, pamoja na maoni ya mara kwa mara kuhusu kuanzisha miradi ya maendeleo kwa wanachama haswa kufungua akaunti na kadhalika..

Hata hivyo wanachama walitumia fursa hii kufanya uchaguzi wao wa viongozi katika wilaya ya kaskazini ya Bungoma. Uchaguzi ulifanyika bila shida yoyote ukisimamiwa na Bwana David Wanya ambaye ni mfanyabiashara sokoni Kitale. Bwana Mutanda Ayubu alichaguliwa kama mwenyekiti bila kupingwa. Naibu mwenyekiti ni Kennedy Nyongesa wa Yayashop. Katibu mkuu ni Paul Sirengo, Katibu mtendaji wa Peter Yamame, mtunza hazina ni Jendeka Goldah Vuyiyi na karani ni Lewis Munyasia. Na wote waliahidi kujadiliana na vyama vingine bila ubaguzi wowote.

Labda tatizo ni kuwa kwenye sherehe yao kulikuwa na upungufu kidogo, kwani chakula na vinywaji vilikuwa vya wageni pekee. Na matumaini ya wanachama kuandaa chakula cha kichina hayakutimia kwani hakukuwa na hata mmoja kati yao aliyekuwa na ujuzi wa upishi wa kichina. Kwa hivyo ilikuwa tu vinywaji soda ya kawaida, maji na sambusa kadiri iliyotengenezwa kwa umbo la pembe tatu kwa kupikwa au kukaangwa kwa mafuta..

Bwana Shariff pia anasema kuwa anapenda kutoa shukurani zake kwa Bwana Lewis Juma Munyasia kwa kujitolea na kutoa chumba ambacho kwa sasa ni Mkataba ndogo katika kijiji cha Nalondo kilicho mbali kidogo na mji wa Bungoma Kenya, licha ya shughuli hizi zote baadhi ya wasikilizaji walikwua na radio zao wakifuatilia mambo vile yalivyo huko China..

Tunamshukuru sana Bwana Mutanda Ayubu Shariff kwa barua yake ya kutuelezea jinsi yeye na wenzake walivyofanya shughuli ya kusherehekea siku ya mwaka mpya wa jadi wa China, maelezo yake yametutia moyo sana, tunawashukuru wote walioshiriki kwenye shughuli hiyo. Ni matumaini yetu kuwa tutadumisha mawasiliano na urafiki kati yetu.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-03