Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-03 15:14:18    
China kudhibiti matumizi ya ardhi

cri

Katika miaka ya karibuni, uwekezaji wa mali zisizohamishika umekuwa ukiongezeka kwa kasi. Ongezeko hilo linaposukuma mbele maendeleo ya uchumi wa China, pia linaleta changamoto kwa utulivu wa uendeshaji wa uchumi kwa jumla. Changamoto kubwa ni kuwa miradi mingi inatumia ardhi kubwa, yakiwemo mashamba vijijini. Ofisa wa wizara ya ardhi na maliasili ya China alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari wa Redio China Kimataifa alisema, kuanzia mwaka 2006 China imeongeza nguvu ya kudhibiti matumizi ya ardhi yanayokwenda kinyume na sheria, na hatua hiyo imepata mafanikio katika kuzuia vitendo hivyo. Pia China imechukua hatua kulinda maslahi ya wakulima ambao mashamba yao yalitumiwa kwa ajili ya ujenzi wa miradi.

Kutokana na ongezeko kubwa la uchumi wa China, uwekezaji unapata maendeleo makubwa katika sehemu mbalimbali nchini China, na mashamba mengi yaliyoko kando ya miji yametumiwa kwa ujenzi wa viwanda na nyumba. Hali hiyo imesababisha kutokea kwa baadhi ya matatizo ya kiuchumi na kijamii. Ofisa wa idara ya utekelezaji wa sheria na usimamizi katika wizara ya ardhi na maliasili ya China Bw. Guo Baoping alisema,

"Matumizi ya ardhi yanayokwenda kinyume na sheria yanamaanisha kuwa watu wanatumia ardhi nyingi na kujenga maeneo ya kiuchumi bila ya kufuata sheria. Hivi sasa nchini China maeneo ya kiuchumi ni makubwa kuliko maeneo ya miji. Serikali za miji kadhaa zinatumia ardhi ovyo, vitendo hivyo vimeathiri vibaya maslahi ya wakulima na kusababisha hali isiyo na utulivu kwenye jamii."

Habari zinasema katika sehemu kadhaa mashamba mengi yalitumiwa kwa sababu mbalimbali, lakini wakulima waliopoteza mashamba yao walilipiwa fidia ndogo. Bw. Guo Baoping alisema hivi sasa China inafanya ukaguzi kuhusu uwezo wa maofisa wa serikali kwa mujibu wa ongezeko la uchumi na mapato ya fedha, hivyo baadhi ya maofisa walijenga maeneo makubwa ya kiuchumi au kuanzisha ujenzi wa miradi mingi ambayo ni marudio ya miradi mingine iliyojengwa.

Kama hali hiyo itaendelea, bila shaka itaathiri maendeleo mazuri ya uchumi na jamii ya China. Ni lazima China ichukue hatua kudhibiti matumizi ovyo ya ardhi. Katika miaka ya hivi karibuni udhibiti wa matumizi ya ardhi umekuwa sera muhimu ya usimamizi wa uchumi kwa ujumla, China imetoa sera nyingi ili kupunguza matumizi ya ardhi kwa ujenzi wa viwanda na nyumba, na kuadhibu matumizi ya ovyo ya mashamba. Naibu mkuu wa usimamizi wa ardhi wa China Bw. Gan Zangchun alipohojiwa na waandishi wa habari alisema,

"Ili kuimarisha na kuboresha usimamizi kwa ujumla, tunapendekeza itekelezwe sera ya ardhi kwenye usimamizi wa uchumi kwa ujumla. Zamani idhini ya matumizi ya ardhi ilitolewa na baraza la serikali, hivi sasa inatolewa na serikali za mikoa. Ni lazima idara za usimamizi wa ardhi za serikali kuu ya China ziimarishe uwezo wa usimamizi badala ya kushughulikia masuala madogo likiwemo kutoa idhini ya matumizi ya ardhi."

Habari zinasema kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Novemba mwaka 2006, China imechunguza matukio elfu 77.4 za matumizi haramu ya ardhi, kupunguza matumizi ovyo ya ardhi zenye eneo la mita za mraba elfu 10, na kuwaadhibu maofisa waliokiuka sheria. Wizara ya ardhi na maliasili ya China imeongeza nguvu kudhibiti matumizi ya ardhi kwa ujenzi, na kutaka miradi yote ya ujenzi ambayo itatumia mashamba ipitishwe na wataalamu. Naibu waziri wa ardhi na maliasili ya China Bw. Li Yuansheng alisema, hivi sasa matumizi ovyo ya ardhi yanazuiliwa vizuri.

"China inaendelea kusimamisha ujenzi wa maeneo ya kiuchumi. Idara za usimamizi wa ardhi za ngazi mbalimbali zinafanya juhudi kukagua miradi mipya, zimegundua miradi mingi ambayo inatumia ardhi ovyo, na zimezuia ongezeko kubwa la kupita kiasi la uwekezaji kwenye mali zisizohamishika."

Wakati China inapoimarisha ukaguzi wa matumizi ya ardhi, pia inasukuma mbele mageuzi ya utaratibu wa matumizi ya ardhi kwa kulipia, kuendelea kuimarisha usimamizi wa mapato kutokana na matumizi ya ardhi, kutoza malipo ya matumizi ya ardhi, na kutumia mapato hayo kuendeleza kilimo.

Bw. Li Yuansheng alisema China inapochunguza matukio ya matumizi haramu ya ardhi, pia inalinda maslahi ya wakulima ambao mashamba yao yalitumiwa katika ujenzi wa miradi iliyojengwa.

"Tumeongeza fidia kwa wakulima ambao mashamba yao yalitumiwa na miradi, na kuwasaidia wakulima hao kushiriki kwenye huduma za jamii. Kwenye msingi wa kuhakikisha maisha ya wakulima hao hayawi mabaya zaidi, na maisha yao yatakuwa na uhakikisho katika muda mrefu, tumechukua hatua nyingi katika kukamilisha utaratibu wa kutumia mashamba, kutoa fidia, na kuwasaidia wakulima hao kutafuta ajira mpya na kutatua mgogoro unaosababisha na matumizi ya mashamba."

Habari zinasema katika sehemu nyingi nchini China, wakulima wengi ambao mashamba yao yalitumiwa kwenye ujenzi wa miradi wamejiunga na mfumo wa huduma za jamii ambazo maisha yao yanaweza kuzitegemea. Wakati huo China inatoa mafunzo bure kwa wakulima hao ili waweze kutafuta ajira mjini. Katika kijiji cha Longhe mjini Jiangyin mkoani Jiangsu, mkulima Bw. Hui Jianping anaweza kupata Yuan 150 kwa mwezi ambazo ni fidia inayotolewa na serikali kwa wakulima waliopoteza mashamba. Katika siku zijazo fedha hizo zitaongezeka zaidi. Bw. Hui anaridhika na fedha hizo, alisema,

"Nitaweza kupata Yuan 200 kwa mwezi nitakapofika umri wa miaka 60, fedha hizo ni karibu sawa na mshahara wa fanyakazi staafu wa mijini, hili ni jambo ambalo sikuwahi kutarajia hapo zamani."

Habari zinasema China inakamilisha utaratibu wa ukaguzi wa ardhi ya taifa, idara za ukaguzi wa ardhi zimeanzishwa katika sehemu 9 muhimu ikiwemo miji ya Beijing na Shanghai, ili kuendelea kudhibiti matumizi ya ardhi kwa ujenzi na kuhifadhi mashamba vijijini. Idara hizo zitafanya ukaguzi kuhusu utekelezaji wa hifadhi ya mashamba na malipo ya matumizi ya ardhi kwa ajili ya ujenzi wa viwanda katika miji mbalimbali. Wakati huo huo, China itaendelea kutekeleza kwa makini utaratibu wa kukagua kazi za maofisa katika usimamizi wa ardhi, ambao kazi za kugundua na kuzuia matumizi haramu ya ardhi ni sehemu muhimu ya ukaguzi wa kazi za. Serikali ya China itawaadhibu maofisa ambao hawatazuia matumizi haramu ya ardhi na kusababisha athari mbaya, na wale hawatachunguza au kuficha matumizi haramu ya ardhi.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-03