Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-03 15:02:13    
Mkutano wa ngazi ya juu kuhusu usalama wa afya duniani wafanyika nchini Singapore

cri

Tarehe 7 Aprili ni "siku ya afya duniani", kauli mbiu ya siku hiyo mwaka huu ni "usalama wa afya duniani". Ili kueneza kauli mbiu hiyo, Shirika la Afya Duniani WHO pamoja na serikali ya Singapore tarehe mbili zilifanya mkutano wa ngazi ya juu kuhusu usalama wa afya duniani huko Singapore. Kwenye mkutao huo washiriki walizungumzia tishio kubwa la usalama wa afya linaloikabili dunia na kuona kwamba nchi zote zinapaswa kuimarisha ushirikiano na kuchukua hatua za pamoja ili kukabiliana na tishio hilo.

Wajumbe kutoka Shirika la Afya Duniani WHO, mawaziri wa afya, maofisa wa serikali na wajumbe wa mashirika husika zaidi ya 200 kutoka Malaysia, Cambodia, Laos, Brunei, Myanmar na Vietnam walihudhuria mkutano huo. Waziri mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong kwenye ufunguzi alisema, ingawa sayansi na teknolojia zinaendelea siku hadi siku, lakini maafa yanayosababishwa na magonjwa bado hayatabiriki. Hata hivyo, alisema kama ushirikiano ukiimarishwa na kujiandaa vya kutosha, tunaweza kupunguza athari za maafa hayo. Katibu mkuu wa Shirika la Afya Duniani Bi. Margaret Chan kwenye mkutano huo alisema, njia za jadi zinazotumika katika baadhi ya nchi hazifai tena kwa mabadiliko mapya yanayotokea duniani. Kwa hiyo wakati dunia yetu inapokabiliwa na hatari, kila nchi ni lazima ichukue hatua za kujikinga, na magonjwa makubwa yanapokuwa tishio kubwa Shirika la Afya Duniani itaendelea kutoa tahadhari kama lilivyofanya zamani kwa nchi zote na kubadilishana teknolojia za kujikinga na maofisa wa afya wa kila nchi, na kutoa ushirikiano na msaada ili kuwanusuru watu wa kila taifa.

Mkutano huo ulifanyika katika mazingira ambayo usalama wa afya duniani umekuwa unazidi kuhatarishwa. Magonjwa ya UKIMWI na homa ya mafua ya ndege yanaenea kwa kasi na yamekuwa tatizo linalofuatiliwa sana na kila nchi. Alisema, maafa ya kimaumbile na matumizi ya silaha kali pia yanaweza kuhatarisha afya ya binadamu. Moja ya mada zilizozungumzwa kwenye mkutano huo ni namna ya kuunganisha sera za mambo ya nje pamoja na usalama wa afya duniani. Waziri wa mambo ya nje wa Norway Bw. Jonas Gahr Store anaona kuwa utandawazi unazifanya nchi kutegemeana, kwa hiyo utatuzi wa usalama wa afya unahitaji kuzingatiwa kwa mkakati na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa. Mada nyingine kwenye mkutano huo ni "Taratibu za Afya Duniani" zitakazotekelezwa kuanzia tarehe 15 Julai mwaka huu. Taratibu hizo mpya zitasaidia nchi na sehemu mbalimbali kupambana na magonjwa ya kuambukiza katika sekta za mawasiliano na biashara. Kwa mujibu wa taratibu hizo, usimamizi wa afya utaimarishwa katika meli na ndege, mbali na viwanja vya ndege na forodha. Na taratibu hizo zimesisitiza uchunguzi, utabiri na kuchukua hatua za haraka wakati usalama wa afya ya umma inapokuwa hatarini.

Washiriki wa mkutano huo pia walijadili ushirikiano wa teknolojia mpya kati ya mashirika ya afya ya kimataifa, kwa mfano, kuanzisha mtandao wa internet wa kikanda au dunia nzima, nchi zote ziweze kunufaika na teknolojia za kisasa, kuimarisha tahadhari na hali ya maambukizi. Ili kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa, washiriki wameona ni muhimu kudhihirisha wazi hali ya afya ya umma na kuimarisha imani kati ya mataifa. Ofisa wa Singapore alitumia mfano wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Sars, alieleza umuhimu wa kupasha habari na kuwasiliana kwa wakati na nchi nyingine na Shirika la Afya Duniani WHO, kwa kufanya hivyo maambukizi yanaweza kudhibitiwa haraka.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-03