Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-04 15:58:36    
Wakazi wenye matatizo ya kiuchumi wa mji wa Dalian wananufaika na utaratibu wa misaada ya matibabu

cri

 Misaada ya matibabu ni sehemu muhimu katika utaratibu wa misaada ya kijamii. Kutokana na sababu mbalimbali baadhi ya watu wenye matatizo makubwa ya kiuchumi, hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu, wala kushiriki kwenye bima ya matibabu. Kwa watu kama hao misaada ya matibabu imekuwa ni matumaini yao pekee. Dalian ni mji wa bandari ulioko kaskazini mashariki mwa China, uchumi wake una maendeleo mazuri. Kuanzia mwaka huu, serikali ya mji huo itatumia fedha nyingi katika kueneza huduma za misaada ya matibabu kwa wakazi wote wenye matatizo ya kiuchumi mjini humo.

Bw. Zhang Fengling mwenye umri wa miaka 51 ni mfanyakazi ambaye hajaajiriwa, na alipatwa na saratani ya damu miaka 7 iliyopita. Bw Zhang ametumia zaidi ya Yuan laki tatu kwa ajili ya matibabu yake, ambazo ni akiba yote ya familia yake iliyokuwa benki, pamoja na misaada kutoka kwa jamaa na marafiki zake. Gharama kubwa za matibabu zimekuwa mzigo mkubwa kwa familia yake. Kutokana na kukosa fedha za kutosha, Bw. Zhang Fengling alisimamisha kupatiwa matibabu kwa muda mrefu. Lakini sera ya misaada ya matibabu kwa wakazi maskini iliyotolewa mwaka huu na serikali ya mji wa Dalian imempatia fursa ya kupata matibabu tena. Alisema:

"zamani kila mara nilipokwenda hospitali, mke wangu na dada yangu waliitisha mkutano wa familia ili kuchangisha fedha. Hivi sasa serikali inatoa kadi za misaada ya matibabu, hatua hiyo imepunguza mzigo kwa familia yangu."

Kadi ya misaada ya matibabu ni kitambulisho cha misaada ya matibabu kilichotolewa na serikali ya mji wa Dalian kwa wakazi maskini. Kwa mujibu wa kanuni husika, wakazi wenye pato chini ya kiwango cha maisha ya msingi, ambao hawashiriki kwenye bima ya matibabu, wana haki kamili ya kupewa msaada wa matibabu. Wakazi wanaotimiza masharti hayo wanapewa Yuan 100 kwa mwaka kwa ajili ya matibabu, na kama wakilazwa hospitali, kwa wastani wanapewa ruzuku ya matibabu ya Yuan 4300, na ili kutekeleza sera hiyo, serikali ya mji wa Dalian kila mwaka inatenga Yuan milioni 55 kwa ajili ya utaratibu huo. Bi. Xu Hongmei ni mmoja kati wa watu wa kundi la kwanza la wakazi walionufaika na sera hiyo. Alisema:

"familia kama ya kwetu zenye pato la chini hazimudu gharama za matibabu, sera hiyo inatunufaisha moja kwa moja katika matibabu."

Mpaka sasa, kwa jumla wakazi elfu 67 wa mji huo wananufaika na sera hiyo, wengi kati yao hawakutoa ombi la misaada hiyo hata bila wao kujua. Mkurugenzi wa kamati ya mtaa wa Malan wa mji huo, anaoishi Bi. Zhang Fengling, Bi. Guo Xiaoxuan alisema:

"tulithibitisha familia mojamoja kati ya familia zaidi ya elfu moja zenye matatizo ya kiuchumi zinazoishi katika mtaa huo, na orodha ya zile zisizoshiriki kwenye bima ya matibabu inatumwa kwa idara ya mambo ya kiraia ya mji huo na kuongezwa kwenye orodha ya familia zinazopewa misaada ya matibabu. Si kwamba wao wanaenda kuomba misaada kwa serikali, bali ni serikali inayowatafuta na kuwapatia msaada.

Tofauti na utaratibu wa zamani wa kutoa misaada, sera hiyo inatoa misaada kabla, na wala si baada ya watu kupatwa na matatizo. Hivi sasa data kuhusu wakazi wanaohitaji misaada zimekusanywa kwenye mfumo wa kompyuta wa idara ya matibabu ya mji huo, wagonjwa wanaweza kupata matibabu au kununua dawa katika mamia ya hospitali na maduka ya dawa yaliyoko mjini Dalian kwa kutumia kadi ya matibabu iliyotolewa na serikali. Naibu mkurugenzi wa kituo cha usimamizi wa bima ya matibabu ya wafanyakazi wa Dalian Bw. Sun Xiangjun alisema:

"sera hiyo inaweza kupunguza gharama, na pia inarahisisha utaratibu wa wagonjwa kupata matibabu. Hivi sasa ni rahisi sana kwa wakazi hao kupata matibabu."

Utekelezaji wa sera hiyo mjini Dalian pia unakaribishwa na hospitali, kwa kuwa sera hiyo inasaidia kupunguza migogoro kati ya madaktari na wagonjwa. Naibu mkuu wa hospitali ya urafiki ya Dalian Bw. Zhang Zhonglu alisema,

"zamani wagonjwa maskini waliposubiri kupewa misaada au kulipa gharama za matibabu, mara kwa mara walikuwa wanakosa raha. Hali hiyo pia ilikuwa ni sababu moja ya kuwepo kwa uhusiano wa utatanishi kati ya madaktari na wagonjwa. Hivi sasa sera hiyo inawanufanisha watu wengi wenye matatizo ya kiuchumi, pia inapunguza kwa kiasi kikubwa migogoro kati ya wagonjwa na madaktari."

Bw. Zhang Zhonglu alisema, kutokana na uongozi wa serikali, hospitali za Dalian pia zimetoa sera mbalimbali za nafuu kwa wakazi maskini. Kwa mfano, wagonjwa wenye matatizo ya kiuchumi wanapunguziwa gharama kwa asilimia 30 katika upimaji wa kimatibabu na upasuaji mkubwa.