Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran tarehe 4 alitangaza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika huko Tehran kuwa, Iran imeamua kuwasamehe na kuwaachia huru askari 15 wa jeshi la maji la Uingereza waliozuiliwa nchini humo kuanzia tarehe 23 Machi. Vyombo vya habari vinaona kuwa, tukio hilo limeweza kutatuliwa kwa njia ya amani ni kutokana na sababu mbalimbali.
Tarehe 23 Machi Iran iliwazuia askari 15 wa jeshi la maji la Uingereza kwenye eneo la maji la ghuba ya Uajemi ambalo siku zote linagombewa na Iran na Iraq. Kwa kuwa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liliamua kupiga kura kuhusu mswada wa azimio jipya kuhusu suala la nyuklia la Iran tarehe 24 Machi, na jeshi la Marekani nchini Iran liliwahi kuwazuia wairan watano mwezi Januari mwaka huu, hivyo vyombo vya habari vilidhani kuwa, matukio hayo mawili yanahusiana, Iran inawazuia askari wa Uingereza kwa kujaribu kutoa ishara kuhusu msimamo wake imara, pia kuonesha uwezo wake wa kujipatia hali ya uwiano katika mapambano kati yake na nchi za magharibi, pia inataka kujua jibu la pande husika. Sasa tukio hilo lililodumu kwa siku 13 limetatuliwa kwa njia ya amani, hasa kutokana na sababu mbalimbali kama zifuatazo:
Kwanza katika tukio hilo, Iran siku zote ilikuwa ina uwezo wa kudhibiti hali ya mambo. Baada ya tukio hilo kutokea, Iran ilisisitiza mara kwa mara kuwa, lengo lake la kuwahoji askari wa jeshi la Uingereza waliozuiliwa, ni kutaka kufanya uchunguzi kuhusu kama askari hao waliingia kwenye eneo la maji la Iran au la. Lakini kutokana maendeleo ya hali ya mambo, mwishowe Iran ililichukulia tukio hilo kuwa ni tukio lililosababishwa na uelewa wa makosa, na kulitatua bila kuchukua hatua yoyote.
Pili, msimamo wa Uingereza iliyohusika na tukio hilo ulibadilika hatua kwa hatua. Ingawa rafiki yake na mshirika wake Marekani ilionesha msimamo mkali na kusema hatua ya Iran ya kuwashikilia askari wa jeshi la Uingereza haisameheki, lakini Uingereza ilipoona juhudi zake za kutafuta msaada wa Jumuiya ya Kimataifa haziwezi kufanikiwa, iliacha msimamo wake mkali wa mwanzo, na ikashikilia kuwa ni lazima ifanye mazungumzo ya kidiplomasia ili kutatua tatizo.
Aidha Marekani na Iran pia zilifanya mawasiliano fulani. Mjumbe wa Iran tarehe 4 aliruhusiwa kukutana na maofisa watano wa Iran wanaozuiliwa na jeshi la Marekani nchini Iraq. Ingawa kila upande ulisisitiza kuwa mkutano huo hauhusiani na tukio la "askari wa jeshi la maji la Uingereza", lakini ni dhahiri kuwa, mkutano huo hakika ulisaidia kwenye utatuzi wa tukio la "askari wa jeshi la maji la Uingereza".
Wachambuzi wanaona kuwa, ingawa tukio hilo limetatuliwa kwa njia ya amani, lakini katika kipindi cha siku zijazo tukio hilo bado litaleta athari kwa uhusiano kati ya Iran na nchi za magharibi.
Kidiplomasia, Iran iliwazuia askari wa jeshi la maji la Uingereza, kutoa onyo mara kwa mara halafu kudai kufanya mazungumzo, siku zote ilikuwa inadhibiti tukio, kijuujuu iliiadhibu Uingereza ambayo ni mtiifu wa Marekani, lakini kwa kweli uhusiano wa uaminifu ulio dhaifu kati ya Iran na Uingereza ambayo ni nchi kubwa katika Umoja wa Ulaya umerudi nyuma zaidi. Iran itakabiliwa na taabu kubwa zaidi katika kujiunga tena na jumuiya ya kimataifa na kupata heshima duniani.
Kiuchumi, tukio hilo limesababisha hali ya sehemu ya ghuba izidi kuwa mbaya, ambalo litaleta athari mbaya kwa Iran kuvutia uwekezaji na kufanya ushirikiano wa nishati na nchi nyingine. Vyombo vya habari vimeonesha kuwa, baada ya tukio hilo, suala la nyuklia la Iran litaibuka tena baada ya kuwekwa kando kwa muda, ambapo Iran na nchi za magharibi zitaendelea na mapambano kuhusu suala hilo.
|