Tarehe 2 mwezi Aprili mwaka 1989, kamati kuu ya kundi la ukombozi wa Palestina ilifanya mkutano huko Tunisia, Bw. Yasser Arafat ambaye ni mwenyekiti wa kamati kuu ya kundi la ukombozi wa Palestina, kamanda mkuu wa jeshi la nguvu ya mapinduzi alichaguliwa kuwa Rais wa Palestina.
Bw. Yaser Arafat alizaliwa Jerusalem, jina lake kamili ni Rahman Abdul Rauf Arafat al-Qwdwa al-Hussein. Bw. Arafat alipokuwa mtoto, mwalimu wake alimpa jina la "Yasser" ili kumkumbuka rafiki yake aliyefariki dunia. Baada ya vita vya pili vya dunia, mabadiliko makubwa yalitokea katika sehemu ya mashariki ya kati, wanasiasa wengi walitokea na wengine walitoweka katika ulingo wa kisiasa kwa nyakati mbalimbali. Lakini katika miaka mingi iliyopita, Bw. Arafat aliendelea kuwepo katika ulingo wa kisiasa. Tangu alipokuwa kijana, Yasser Arafat alikuwa mwanamapinduzi, alishiriki kwenye shughuli za kupinga uzayuni pamoja na baba yake. Baada ya kuundwa kwa Israel, familia yake ilihamia kwenye sehemu ya Gaza, huko Gaza alitambua maisha ya wakimbizi wa kiarabu. Mwaka 1959, Bw. Arafat alishiriki kwenye shughuli za kupinga uvamizi wa jeshi la Israel na kuwa mwanzilishi mmoja wa kundi la Fattah.
Mwaka 1969, Bw. Arafat aliapishwa kuwa mwenyekiti wa kundi la ukombozi wa Palestina, aliwaongoza wapalestina kupambana na jeshi la Israel. Hivyo Israel ilimuona Bw Yasser Arafat kuwa adui kubwa, serikali ya Israel ilikuwa inatekeleza mipango mingi ili kumwondoa Bw Arafat. Lakini Yasser Arafat alikuwa ni mtu mwenye akili sana, alichukua hatua mbalimbali zenye mafanikio na kufaulu kukwepa mashambulizi mengi ya Israel. Kwa Bw. Arafat, si kama tu hatari ilitoka kwa Israel, bali pia ilitoka kwa nchi nyingine. Mwaka 1970 Palestina na Jordan zilipambana, jeshi la Jordan lililishinda jeshi la ukombozi wa Palestina, hali ya Arafat ilikuwa mbaya sana. Wakati huo huo, Rais wa Misri Bw. Naser aliitaka Jordan ihakikishe usalama wa Arafat na kutuma ndege maalumu mjini Amman. Lakini Jordan ilipinga ombi la Rais Naser, na ikataka kumwua Bw Arafat. Kutokana na hali hiyo ya hatari, Bw. Yasser Arafat alivaa nguo za Kuwait, na kujifanya balozi wa Kuwait, na kufanikiwa kuingia kwenye ubalozi wa Misri ulioko Amman na kuondoka kwa ndege maalumu.
Bw. Arafat alikuwa na uwezo mkubwa wa kutoa hotuba. Wapalestina walimpenda, hata katika nchi nyingine za kiarabu zilimheshimu sana. Bw. Arafat alijitolea katika maisha yote kwa kazi ya ukombozi wa Palestina. Bwana Arafat alifariki tarehe 10 mwezi Novemba mwaka 2004 nchini Ufaransa.
Tarehe 6 mwezi Aprili mwaka 1994, ndege ya rais iliangushwa, marais wa Burundi na Rwanda walikufa
Tarehe 6 mwezi Aprili mwaka 1994, Rais wa Rwanda Bw. Juvenal Habyarimana na Rais wa Burundi Bw. Cyprian Ntaryamira walimaliza mkutano wa kikanda kuhusu kuondoa migogoro ya kikabila na kurudi Kigali, mji mkuu wa Rwanda kwa ndege moja, usiku wa siku hiyo ndege ilipofika Kigali ilitunguliwa kwa roketi na kuanguka, marais wa nchi hizi mbili pamoja na watu walioambatana nao walikufa kwenye tukio hilo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania
Siku chache zilizopita mwenyekiti wa umoja wa wanawake wa Tanzania Bi. Anna Abdallah na ujumbe wake wa watu sita walikuwepo nchini China kwa ziara ya mafunzo, ziara iliyoanza tarehe 19 hadi tarehe 29 mwezi march. Katika ziara hiyo Bi Anna Abdalah alipata nafasi ya kuongea na Radio China Kimataifa ambapo alieleza kuhusu uhusiano uliopo kati ya wanawake wa China na Tanzania.
Kuhusu uhusiano kati wanawake wa China na Tanzania Bi Anna alisema, "Ushirikiano kati ya wanawake wa China na Tanzania ulianza mara tu baada ya uhuru wa Tanzania na tangu wakati huo hadi hivi sasa tumeshafanya mambo mbalimbali" Zamani ushirikiano kati wanawake wa China na Tanzania ulitilia mkazo zaidi namna ya kuwasaidia kuwasomesha wasichana wa kitanzania hasa katika maeneo ambayo ilikuwa vigumu kwa wasichana wa kitanzania kupata nafasi ya kusomea, kwa mfano taaluma ya udaktari. Kwa kupitia ushirikiano wasichana wengi walipata nafasi ya kuja nchini China kwa masomo na walisaidiwa kujiandaa ili kuweza kushika madaraka mbalimbali nchini mwao. Wakati huo serikali ya China ilikuwa inatoa nafasi za masomo kwa Watanzania wake kwa waume lakini licha ya nafasi hizo umoja wa wanawake wenyewe ulipewa nafasi zake maalum kwa ajili ya wanawake.
Bi Anna amesema kuwa umoja wa wanawake wa china umekuwa ukiwasaidia sana wanawake wa Tanzania, kwa mfano waliwahi kuvisaidia vikundi vya wanawake vya ushonaji masaada wa vyerehani, wamewahi kusaidia uboreshaji wa shughuli za mikono ya kina mama.
Mwaka 2006 shirikisho la wanawake wa China lilituma ujumbe nchini Tanzania ambapo pia walituleta vifaa mbalimbali vikiwemo vifaa vya ofisi kama computer na printer zake, mashine za kurudufu na baiskeli ambapo baiskeli ziligawiwa kwa makatibu wa umoja wa wanawake wa kila wilaya. Katika ziara hiyo tuliwatembeza katika matawi yetu ambapo waliona shughuli mbalimbali zinazofanywa na umoja wetu, na baada ya ziara waliona kuna umuhimu wa kuzidisha zaidi ushirikiano ambapo pia walitualika kuzuru nchini China.
Pia tuliwatembeza katika shule za chekechea zilizopo katika jamii za kimasai huko Arusha ambapo tuliwaonesha jinsi serikali inavyowahamasisha vijana kuanza shule ambapo katika jamii nyingi za kimasai za wafugaji, hili limekuwa tatizo gumu hasa kwa watoto wa kike. Na katika ziara yetu wametupa vifaa mbalimbali vya shule ya chekechea kama vile mipira, kalamu, vifutio na vifaa vya kutengenezea madawati, na vifaa hivyo watavisafirisha wenyewe.
Akieleza ni mambo gani ambayo wamejifunza katika ziara yao nchini China, Bi Anna Abdalah alisema kuwa, wamejifunza sana kuhusu wanawake wajasiriamali jinsi wanavyofanya shughuli zao, kwa sababu wanawake wajasiriamali wa Tanzania wanafanya shughuli ndogondogo tofauti na ilivyo China ingawa wapo wengine ambao wanafanya biashara za kati au za juu wakisafiri kuja China kununua bidhaa au kwenda Dubai. Na jambo la msingi kabisa walilojifunza ni jinsi ya kuwaunganisha wajasiriamali hao, ili wawe na umoja mkubwa, ili kama mtu anataka kuagiza bidhaa kutoka China isiwepo haja ya kuja China kununua bidhaa bali mjasiria mali anaweza kutumia mawasiliano ya internet au kuwasiliana na wajasiriamali wa china ili kuweza biashara nzuri kabisa.
Katika ziara hiyo ambapo pia walitembelea viwanda vya wanawake waliosaidiwa na shirikisho la wanawake wa China, waliomba msaada wa kuwasaidia wanawake wa Tanzania wanaotengeneza bidhaa ndogondogo ili ziwe na ubora utakaozifanya zipate masoko kwa urahisi.
Alimalizia kwa kusema, wanawake wajasiriamali wa China wameonesha nia ya kwenda kuwekeza nchini Tanzania ambapo wamewaomba kuwekeza katika shughuli zinazofanywa na wanawake.
Idhaa ya kiswahili 2007-04-06
|