  
Tarehe 23 Machi askari 15 wanamaji wa Uingereza walikamatwa na Iran kwa sababu ya kuingia eneo la bahari ya Iran bila idhini. Baada ya juhudi nyingi za vuta nikuvute, mwishowe tarehe 5 Aprili askari hao wanamaji waliachiliwa huru na kurudi nyumbani.
Askari hao wanamaji walipanda ndege ya Uingereza siku hiyo asubuni kutoka Tehran. Kabla ya kuondoka walihojiwa na kituo cha televisheni cha Iran, licha ya wao kutoa shukrani kwa kutendewa vema waliona furaha kubwa ya kurudi nyumbani na kujiunga na jamaa zao.
"Tunaelewa kwamba watu wa Iran wanaona wameonewa kutokana na sisi kuingia ndani ya eneo la bahari yao. Lakini ninachotaka kusema ni kuwa kwa vyovyote vile hatuna nia ya kuwaudhi watu wa Iran na kuihujumu mamlaka ya Iran. Ninatumai tukio hilo litasaidia kuboresha uhusiano kati ya Uingereza na Iran."
Bi. Faye Turney ni askari pekee mwanamke kati ya wanamaji hao, na ni wa kwanza kukiri kwamba waliingia ndani ya eneo la bahari ya Iran kwenye kituo cha televisheni cha Iran. Awali, baada ya kituo cha televisheni cha Iran kutangaza video yake, serikali ya Iran iliahidi kuwa itamwachia huru ndani ya siku mbili. Lakini kutokana na Uingereza kujaribu kuishinikiza Iran kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa, Iran ilighairi ahadi yake ya kumwachia huru. Tarehe 5 askari huyo aliyekuwa amevaa hijabu alisema tena mbele ya kamera ya video.
"Sasa nimetulia, naona furaha sana kuweza kurudi nyumbani. Hapa tunatendewa vema, lakini natamani zaidi kurudi nyumbani kujiunga na jamaa zangu. Naomba msamaha kwa kitendo chetu, na nawashukuru kwa wema wenu na kutuachia huru."
Majuma mawili tokea walipokamatwa yalikuwa giza kwa wanamaji hao. Taarifa ya serikali ya kuwaachia huru kwa ghafla iliwafurahisha na hata hawakuamini masikio yao. Mama wa askari mwanamaji, Adam Sperry alisema kwa msisimko,
"Waliniambia habari hiyo kwa simu, lakini sikuamini kama ni kweli, niliona hawataachiwa huru kabla ya wiki ijayo au muda mrefu zaidi."
Baba wa askari Chris Coe alisema,
"Sawa kabisa! Tuliposikia habari hiyo sote tulirukaruka kwa furaha."
Kuachiwa huru kwa wanamaji hao 15 kunamaanisha kumalizika kwa mgogoro wa kidiplomasia kati ya Uingereza na Iran. Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair siku hiyo alisema Uingereza ilikuwa na msimamo thabiti katika muda wote ilipowasiliana na Iran. Alisema,
"Tulifanya juhudi nyingi kuliko watu walivyofikiri ili kuwaokoa wanamaji hao mapema. Naahidi kwamba pande zote mbili hazikuwa na makubaliano yoyote ya kichini chini."
Lakini baadhi ya magazeti ya Uingereza yalionesha mashaka kuhusu kauli hiyo ya Bw. Tony Blair. Baadhi yanasema, serikali ya Uingereza iliikabidhi kichini chini Iran barua ya kuomba msamaha, na mengine yanasema, kuachiwa huru kwa wanamaji hao kunahusiana na kuachiwa huru hivi karibuni kwa ofisa mmoja wa Iran aliyetiwa mbaroni nchini Iraq. Zaidi ya hayo, katika sakata hilo, kuna masuala kadhaa ambayo watu wanayafuatilia, kwamba kwa nini wanamaji hao wa Uingereza walikamatwa kirahisi hivi? Kwa nini wanamaji hao walishirikiana vizuri hivi na Iran katika propaganda? Na kwa nini Iran inaweza kufanikiwa kuiaibisha serikali ya Uingereza kupitia propaganda? Kuweza au kutoweza kupata majibu ya masuala hayo kutaathiri sana maendeleo ya uhudiano wa kidiplomasia kati ya Uingereza na Iran.
Idhaa ya kiswahili 2007-04-06
|