Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-09 15:24:01    
Hakelu lililojengwa likining'inia

cri

Katika kipindi hiki kwa leo, nitawafahamisha hekalu lililojengwa kwenye genge la mlima, hekalu hilo linajulikana kwa jina la Xuankongsi, maana yake katika Kichina ni hekalu linaloelea angani, na liko kwenye bonde moja wilayani Hunyuan. Milima iliyoko kwenye pande mbili za bonde hilo ina urefu wa mita mia moja hivi, hekalu la Xuankong liko kwenye sehemu inayoingia ndani kidogo katikati ya genge la mlima, hekalu hilo liko kwenye urefu wa mita 50 hivi kutoka ardhi ya chini, hekalu hilo linaonekana limebandikwa kwenye genge la mlima. Kwa kuwa hekalu hilo lilijengwa kwenye sehemu inayoingia ndani kwenye genge la mlima, mvua na jua haviwezi kuathiri hekalu hilo, hivyo ingawa hekalu hilo lilijengwa zamani za kale, lakini bado liko imara kwenye genge la mlima.

Sehemu muhimu ya hekalu la Xuankong ilijengwa kwa mbao. Ukubwa wa hekalu hilo ni mita za mraba 152.5, ambao ni pungufu ya nusu ya kiwanja cha mpira wa kikapu. Kuna jumla ya vyumba 40 ndani ya hekalu hilo, ukiangalia kutoka mbali, hekalu hilo limejengwa juu ya nguzo kumi kadhaa, jiwe kubwa lililotokeza kwa nje juu ya hekalu, linaonekana kama litaanguka chini mara moja.

Watalii wa nchini na kutoka nchi za nje waliolitembelea hekalu hilo, wote wanashangazwa na hekalu hilo, majengo mbalimbali ya hekalu hilo yameunganishwa na njia zilizotandazwa mbao, ambazo ni nyembamba zilizojengwa moja kwa moja kwenye genge la mlima kiasi cha kuweza tu kuruhusu mtu mmoja kupita. Mtu akiingia kwenye njia hizo hutembea taratibu na kwa uangalifu mkubwa, akihofia kuwa, akikanyaga kwa nguvu, hekalu zima litabomoka. Mwongoza watalii bibi Lin Yu alikuwa amepita muda mfupi uliopita kwenye njia hiyo nyembamba, na bado alikuwa na wasiwasi mkubwa, alisema,

"Tuko juu kwa juu, najisikia kama naelea angani."

Kuna msemo mmoja katika wilaya ya Hunyuan unaosema, "Hekalu la Xuankong liko angani likiwa limening'inizwa kwa manyoya matatu ya mkiani mwa farasi." Mkia wa farasi uliotajwa hapo unafananishwa nguzo ya mti, kwani hekalu limejengwa juu ya nguzo, hekalu limejengwa juu ya nguzo 30, ambazo zimesimamishwa juu ya jiwe kubwa la mlima. Watalii wanapofika kwenye hekalu la Xuankong hudhani kuwa, hekalu hilo limesukumwa na nguzo hizo za mti. Lakini mtafiti anayefanya kazi katika hekalu la Xuankong Bw. Sun Yi alikanusha wazo hilo, alieleza: 

"Ukweli ni kuwa, nguzo hizo zinazosimama hazibebi uzito wowote, uzito wote wa hekalu hilo unabebwa na nguzo zilizolala chini ya hekalu, ambazo upande mmoja wa nguzo hizo zimeingizwa kwenye mawe ya mlima, huu ndio umaalumu wa hekalu la Xuankong."

Nguzo hizo zimezolala chini hekalu zinaonekana kama zimeota kwa kulala kwa upande kutoka kwenye mawe ya mlima, hekalu la Xuankong liko juu ya nguzo hizo 27 zilizolala upande wa chini yake. Bw. Sun Yi alisema, sehemu zinazobeba uzito kwenye miti hiyo zilipatikana baada ya kupigwa hesabu kwa makini na mafundi wa kale. Baadhi ya miti hiyo inabeba uzito, na baadhi ya mingine ilitumika katika kurekebisha urefu wa majengo ya hekalu.

Maadamu miti hiyo imelala chini kama maboriti, je, ni kwanini nguzo zile kumi kadhaa zimezimamishwa wima? Kuna hadithi moja inayosema, zamani hekalu la Xuankong lilipoanza kujengwa, nguzo zilizosimamishwa wima chini ya hekalu zilikuwa nene sana, lakini zile nguzo nene zilifanya hekalu lionekane kama halijajengwa angani, hivyo mtawa mzee wa hekalu aliamua kuondoa nguzo zile zilizosimama chini ya hekalu. Lakini hakutarajia kuwa, baada ya nguzo zile kuondolewa, watalii wasingethubutu kupanda kwenye hekalu la Xuankong. Hivyo mtawa yule mzee alisimamisha nguzo nyingine ndogo kabisa zikifanya kazi kama mapambo. Ingawa hiyo ni hadithi, lakini hali halisi ni kuwa, nguzo zile zinazosimama wima chini ya hekalu la Xuankong hazifanyi kazi yoyote, na hazibebi uzito wa hekalu. Bw. Luo Zhewen ambaye ni mtaalamu wa majengo ya kale wa idara ya vitu vya kiutamaduni ya China, amefanya utafiti kuhusu majengo ya hekalu la Xuankong kwa miaka zaidi ya 20, alisema mbinu ya usanifu wa majengo maalumu ya hekalu la Xunakong ni za kuiga mbinu ya ndege anavyojenga kiota, alisema:

"Sehemu zenye kujitokeza kwa nje, au zenye mabadiliko, kama mafundi wakiziunganisha kwa maboriti au kwa madaraja, inakuwa ni sanaa ya muunganisho kati ya mlima na majengo, sanaa hiyo ni yenye thamani kubwa."

Umaalumu mkubwa wa majengo ya hekalu la Xuankong ni usanifu mwafaka kabisa. Hii inaonekana wakati wa kujenga majengo ya hekalu, mafundi walizingatia sana mazingira maalumu ya kijiografia ya huko, kwa hiyo majengo mbalimbali ya hekalu hilo yanaendana na mazingira yake. Kwa mfano moja ya majengo yaliyo makubwa zaidi ya hekalu la Xuankong ni jengo la Sanguan, ambalo mbele yake ni nyumba moja ya mbao, na nyuma yake yamechimbwa mapango mengi ya mawe, hivyo hekalu likaonekana kubwa na pana zaidi. Ingawa hekalu la Xuankong siyo kubwa, lakini ndani yake zimewekwa sanamu nyingi za mabudha zikiwemo za shaba, chuma, za udongo wa mfinyanzi na za mawe. Kwa kuwa hekalu lenyewe siyo kubwa, hivyo maumbo ya sanamu za hekalu hilo pia ni madogo, hata hivyo sanamu za mabudha zinaonekana zinafanana, zinaonekana zenye hisia mbalimbali na ni zenye thamani kubwa ya kisanaa.

Mbali na usanifu wa majengo usio wa kawaida, hekalu la Xuankong ni hakelu pekee ambalo mabudha wa dini tatu wanaabudiwa kwa pamoja nchni China, ambao ni wa dini za kibudha, kidao na Confucius. Kusema kwa makini, falsafa ya ki-confucius siyo dini, lakini watu wa baadhi ya sehemu nchini China wanaichukulia falsafa ya Confucius kuwa dini yao. Katika ukumbi wa dini tatu ulioko sehemu ya juu kabisa ya hekalu la Xuankong, Sakyamuni, Lao?tzu na Confucius wanakaa pamoja. Kiongozi wa awamu ya kwanza ya idara ya usimamizi wa hekalu la Xuankong Bw. Zhang Jianyang alisema,

"Watalii wa nchini na wa nchi za nje wote wanataka kutembelea hekalu la Xuankong, tena wote wanapanda juu hadi kwenye ukumbi wenye sanamu za mabudha wakuu wa dini hizo tatu, ni China tu ambayo imeweza kufanya viongozi wa dini tatu wakae pamoja, hilo ni wazo zuri lisilo la kawaida."

Hekalu la Xuankong ni hekalu lililojengwa miaka elfu moja iliyopita, ambalo limeunganisha pamoja elimu ya ujenzi wa uhandisi, elimu ya uzuri na dini. Habari zinasema hivi sasa hekalu la Xuankong linatembelewa na watalii karibu elfu kumi kwa siku. Mandhari ya kipekee na sanaa nzuri ajabu ya ujenzi wa majengo vimewavitia na kuwafurahisha mno watalii wa nchini na wa nchi za nje. Endapo umevutiwa na hekalu la Xuankong, basi tunakukaribisha ufike kwenye mjini wa Datong mkoani Sanxi ili ushuhudie wewe mwenyewe.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-09