Vyombo vya habari vya Cote d'Ivoire tarehe 8 viliikariri tume ya Umoja wa Mataifa nchini humo ikisema, jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa na jeshi la Ufaransa yataondoka Cote d'Ivoire kuanzia tarehe 16 mwezi huu. Siku moja kabla ya hapo, serikali ya mpito ya Cote d'Ivoire iliyoongozwa na waziri mkuu mpya Bw. Guillaume Soro iliundwa. Maendeleo hayo yameonesha kuwa, serikali ya Cote d'Ivoire na makundi ya upinzani yameanza kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwanzoni mwa mwezi Machi, na kuonesha kuwa hali ya nchi hiyo imeelekea kuwa tulivu hatua kwa hatua.
Katika miaka ya mwishoni mwa 80 ya karne iliyopita, kutokana na kushuka kwa bei za kahawa na Cocoa kwenye soko la kimataifa, uchumi wa Cote d'Ivoire ulididimia. Wakati huo huo ili kugombea raslimali za kiuchumi, uhusiano kati ya wahamiaji kutoka nje na wakazi wazaliwa huko ulikuwa wasiwasi hadi kuzusha mgogoro wa kijamii. Mwezi Septemba mwaka 2002, Cote d'Ivoire ilikumbwa na jaribio la mapinduzi na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe, wanamgambo wa makundi ya upinzani walidhibiti sehemu ya kaskazini mwa nchi hiyo hatua kwa hatua, na kukabiliana na jeshi la serikali lililodhibiti sehemu ya kusini. Kutokana na usuluhishi wa jumuiya ya kimataifa, mwezi Januari mwaka 2003 vyama vikubwa vya kisiasa na makundi ya upinzani yalisaini makubaliano ya Marcoussis nchini Ufaransa, na kuanzisha mchakato wa amani. Lakini katika mchakato wa kutekeleza makubaliano hayo vyama mbalimbali vya nchi hiyo viliendelea na malumbano bila kusita na kusababisha kuahirishwa mara kwa mara kwa mpango wa kunyang'anya silaha na uchaguzi mkuu wa urais. Kutokana na azimio lililotolewa na baraza la usalama, kipindi cha mpito cha Cote d'Ivoire kitamalizika kabla ya mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, serikali ya mpito lazima ifanye uchaguzi mkuu kabla ya hapo, kuunda serikali mpya, na kutokomeza msukosuko wa kisiasa uliodumu kwa zaidi ya miaka minne.
Mwezi Februari mwaka huu rais Laurent Gbagbo wa nchi hiyo alifanya mazungumzo ya moja kwa moja na kiongozi wa upinzani Bwana Guillaume Soro, ambao walisaini makubaliano ya amani tarehe 4 mwezi Machi. Kutokana na makubaliano hayo pande hizo mbili zilikubali kuunda serikali mpya na kufuta hatua kwa hatua sehemu ya amani iliyosimamiwa na wanajeshi wa nchi za nje, kurejesha shughuli za kuthibitisha vitambulisho vya uraia na kunyang'anya silaha, na kuunda jeshi la umoja ili kufanya maandalizi kwa ajili ya uchaguzi mkuu.
Jambo linalofurahisha ni kwamba, serikali ya Cote d'Ivoire na makundi ya upinzani yameanza kutekeleza mambo yaliyopo kwenye makubaliano. Tarehe 29 Machi kiongozi wa upinzani Bwana Soro aliteuliwa kuwa waziri mkuu ambaye aliapishwa madaraka tarehe 4 Aprili. Serikali mpya ya mpito iliundwa Tarehe 7 Aprili, mawaziri 32 wapya waliteuliwa na rais Gbagbo. Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na Ufaransa nchini Cote d'Ivoire wameamua kuondoka Cote d'Ivoire hatua kwa hatua kuanzia tarehe 16 mwezi huu, na sehemu ya amani itaondolewa. Hayo yameonesha mustakabali mzuri katika kutimiza amani nchini humo.
Lakini mchakato wa amani ya Cote d'Ivoire bado unakabiliwa na matatizo mengi, kama vile madaraka ya waziri mkuu mpya Bw Guillame Soro bado hayajaelezwa wazi, kazi za kuthibitisha vitambulisho vya uraia, kunyang'anya silaha na kuunda jeshi la muungano bado hazijaanza kutekelezwa, pamoja na migongano mingi ya kijamii iliyobaki kutokana na vurugu zilizodumu kwa miaka mingi .
|