Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-10 14:36:03    
Barua 0408

cri

Msikilizaji wetu Mary David Ngadada wa Shule ya sekondari ya Jamhuri, iliyopo Dodoma nchini Tanzania anaanza barua yake kwa kusema yeye ni msichana mwenye umri wa miaka 20 na kwa sasa anasoma katika shule ya sekondari Jamhuri iliyopo mjini Dodoma. Anasema dhumuni la barua yake ni kuomba kuwa mmoja wa wanachama wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa, ikiwemo kushiriki katika vipindi mbalimbali kama vile kipindi cha michezo na matamasha kwa ujumla. Msikilizaji wetu huyu namaliza barua yake kwa kuwatakia wafanyakazi wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa heri na fanaka katika shughuli za kila siku ikiwemo ya kuelimisha jamii.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Mary David Ngadada kwa barua yake, na tunamkaribisha kwa mikono miwili kuwa mwanachama wa idhaa yetu ya Kiswahili, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo kwa vipindi vyetu.

Msikilizaji wetu Seif Said Soud wa S.L.B 559 Shinyanga nchini Tanzania anaanza barua yake kwa kutoa salamu nyingi za mwaka mpya wa 2007 kwa wafanyakazi wote wa idhaa ya kswahili ya CRI, yeye ni mzima na anaendelea na ujenzi wa taifa lake Tanzania. Anasema lengo la barua yake ni kutufahamisha kuwa yeye bado ni mwanachama hai wa idhaa ya kiswahili wa Radio China Kimataifa, pia anaomba atumiwe kalenda ya mwaka 2007 na zawadi nyingine kama zipo. Mwisho Bw. Seif anamalizia barua yake kwa kuitakia idhaa ya kiswahili ya CRI kila la kheri katika mwaka mpya wa 2007 izidi kuwapatia wasikilizaji habari na mambo mengine mengi ya kimataifa.

Tunamshukuru Bwana Seif kwa barua yake na maoni yake kwa vipindi vya idhaa yetu ya Kiswahili, tunaahidi kuwa tutaendelea na juhudi za kuwafurahisha zaidi wasikilizaji wetu, na bila shaka hatutamsahau kama tukiwa na zawadi nyingine kwa ajili ya wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Fred Wakoli Liambila wa S.L.B 13, Webuye nchini Kenya ametuletea barua akitutaka tupokee salamu, yeye ni mzima na pamoja na wasikilizaji wengine nchini Kenya wanaendelea kufurahia matangazo na vipindi mbalimbali kupitia idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Anasema idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa inawafunza na kuwajulisha matukio mengi yanatokea ulimwenguni. Baadhi ya habari ambazo yeye pamoja na wasikilizaji wenzake wamezifurahia ni pamoja na habari za kisiwa marufu cha Taiwan ambacho kinawapa moyo wa kuitembelea China hata kwa dakika chache na kuifahamu zaidi. Bw Fred pia anaombi ambalo aonaona lingemsaidia kuifahamu China, yeye anapenda kutumiwa majarida mbalimbali yatakayo msaidia kujifunza mengi kuhusu China, kwa mfano jarida la utamaduni, urafiki wa China na Afrika. Mwisho anaomba kituo cha FM cha Nairobi kiboreshwe ili wasikilizaji wote wapate uhundo wake.

Tunamshukuru msikilizaji wetu Bwana Fred kwa barua yake ya kutuelezea hali ya wasikilizaji wetu huko Kenya ya kusikiliza matangazo ya idhaa yetu ya Kiswahili, hii imetutia moyo sana. Tunatumai kuwa kutokana na juhudi za wasikilizaji na wafanyakazi wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China tutaweza kuboresha matangazo yetu.

Msikilizaji wetu Harun Ochieng' Opere wa S.L.P 40 Sawagongo nchini Kenya ametuletea barua ambayo kwanza kabisa anachukua nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kumuwezesha na kumpa uhai hata ameweza kuandika na kupokea barua kutoka idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Anatoa pongezi na shukrani kwa watangazaji na wafanyakazi wote wa idhaa ya ya kiswahili ya CRI kwa kazi ya kuwaelimisha na kuwapasha watu habari kuhusu matukio mbalimbali kote duniani.

Msikilizaji wetu pia anaishukuru idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa kumtumia kadi za salamu ambazo zilikuwa zimelipiwa gharama za posta, na kwa mara ya kwanza aliweza kuwasalimia jamaa na marafiki kupitia idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa, anasema kwa kweli alifurahi sana.

Bwana Harun pia anashukuru kwa vijitabu viwili na maua maridadi ya kupendeza aliyopokea, vyote kwa pamoja vilimfurahisha yeye pamoja na jamaa na marafiki zake, "ama kwa hakika ana shukuru sana", ndivyo anavyosema msikilizaji wetu huyu. Anasema atafurahi sana kama atapata nafasi ya kuja kuitembelea China. Anatumaini kuwa siku moja atapata nafasi na bahati ya kuitembelea China, na anaomba Mwenyezi Mungu awape nguvu wafanyakazi na wasikilizaji wote wa Idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa ili iweze kupepea na kuyafikia mataifa yote ya ulimwenguni.

Tunamshukuru msikilizaji wetu Harun Ochieng' Opere kwa barua yake na tunafurahia nia yake ya kujitahidi kupata nafasi ya kuja China kutembelea. Ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo yake. Tunafarijika kusikia kuwa amefurahia zawadi tulizomtumia, na ni matumaini yetu pia kuwa tutaendelea kudumisha mawasiliano kati yetu.

Msikilizaji wetu Joan Nabwile Khisa Kong'an wa S.L.P 441 Bungoma nchini Kenya, ametuletea barua akisema anachukua fursa hii kuwashukuru wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili ya radio China Kimataifa kwa juhudi kubwa ambazo walizifanya mwaka 2006 na anawahimiza wote kuendelea na juhudi hizo kwa mwaka 2007. Anasema kwa hakika anafurahia sana matangazo ya Rado China kimataifa, ambayo yamemsaidia kujifunza mambo mengi sana, na kila siku amekuwa akipiga hatua za kimaendeleo. Baada ya kuwaambia rafiki zake kuhusu kipindi cha Safari nchini China walifurahi sana na wao pia wako tayari kutuandikia barua kuuliza maswali mbalimbali na kushiriki na wasikilizaji wengine wa Radio China kimataifa. Mwisho anamalizia barua yake kwa kuomba kutumiwa fulana ambayo imeandikwa "Radio China Kimataifa"

Msikilizaji wetu Ali Hamis Kimani wa S.L.B 34 Ndori Nchini Kenya, anaanza barua yake kwa salaam na anasema ni matumaini yake kuwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya CRI ni wazima wakiendelea kuchapa kazi, yeye na familia yake ni wazima wakiendelea kuitegea sikio radio China Kimataifa. Anasema dhumuni la barua yake ni kutoa pongezi kwa kazi nzuri ya idhaa ya kiwahili ya CRI iliyofanya kwa mwaka wote wa 2006 na anatumaini kazi hiyo nzuri itaendelea kwa mwaka 2007 bila ubaguzi hasa katika mashindano ya chemsha bongo.

Mbali na pongezi hizo Bwana Ali Hamisi pia anatoa shukrani zake za dhati kwa kutumiwa mara kwa mara kadi za salamu na picha za wanyama na ndege wanaopatikana nchini China, anasema anafurahia sana picha za wanyama. Anamalizia barua kwa kukumbusha kuwa, kwa sasa amebadilisha anuani yake.

Tunamshukuru kwa dhati kwa pongezi zake kwa kazi ya idhaa yetu ya Kiswahili, ni matumaini yetu kuwa atajitahidi kushiriki mashindano ya chemsha bongo ya Radio China Kimataifa mwaka huu yatakayofanyika siku chache baadaye, ili kupata ujuzi mwingi zaidi kuhusu China.

Msikilizaji wetu Benson Barasa Wabwire wa S.L.B 2319 Bungoma nchini Kenya katika barua yake anatoa ombi pamoja na kutoa pongezi kwa idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa. Ombi lake ni kuwa, ili kupanua na kuongeza wasikilizaji wengi kijijini kwake na katika sehemu za karibu anaomba atumiwe kadi nyingi za salamu kwa sababu wenzake pia wanataka kutuma salam kwa wapendwa wao wengi wanaoishi sehemu mbalimbali duniani.

Na pongezi zake zinakuja kwam idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa kumchagua Bw Ayub Mutanda kutembelea nchini China ambapo aliona mambo mengi ya ajabu, na lililomfurahisha zaidi ni kusikia sauti yake kupitia idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Na kuonyesha furaha isiyo kifani, bwana Ayub Mutanda alimpatia zawadi kutoka radio China kimataifa. Anamalizia barua yake kwa kuomba kutumiwa kadi nyingi za salam kwa sababu wameanzisha klabu ya salamu.

Msikilizaji wetu Mutanda Ayub wa S.L.P 172 Bungoma nchini Kenya kwenye barua yake ameanza kwa salamu kutoka maktaba ya jamii ya Kanduyi mjini Bungoma. Anasema yeye ni mzima ana anaendelea vyema kuyategea sikio matangazo ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa bila kukosa hata siku moja, na anasema kwa kweli uungaji mkono wa idhaa ya Kiswahili ya CRI unazidi kuzaa matunda.

Anasema mpaka sasa watu wengi hawaamini kama kweli alipata bahati ya tuzo maalum ya kuitembelea China, lakini cha msingi kwake kwa sasa anazingatia ujuzi na maarifa aliyopata akiwa nchini China. Safari yake nchini imemuwezesha kupata bahati ya kupata marafiki kutoka nchi mbalimbali duniani zikiwemo Vietnam, Brazil, Afghanstan, Marekani, Tanzania, Thailand, Sri lanka, New Zealand, Canada, Russia na nchi nyingine kadha wa kadha. Na marafiki zake wote wamshawasiliana na kupongezana kwa ushirikiano mzuri waliokuwa nao wakati wakiwa Beijing katika sherehe za kutimiza miaka 65 ya Radio China Kimataifa.

Baada ya safari yake nchini China Bw.Mutanda alipata bahati ya kupata mtoto wa kike ambaye ni mrembo ambapo ameamua kumpa jina la "Du Chen Bahati" ambayo ni majina ya mama Chen na Bi Du Shunfang ambao walikuwa wahariri wa kwanza wa Radio China Kimataifa kufika mjini Kisii. Kama ilivyo kawaida msikilizaji wetu huyo anaiomba idhaa ya Kiswahili ya CRI izidi kuendelea vyema kujali maslahi ya wasikilizaji kama ilivyo desturi.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu huyo Mtanda Ayub Shariff kwa barua yake iliyotuelezea mengi, hapa tunapongeza yeye kupata mtoto mmoja, na kumshukuru yeye amempa mtoto wake jina la Du Chen Bahati kwa kukumbuka ziara yetu mjini Kisii. Tuna imani kuwa mawasiliano na urafiki kati yetu utadumu daima.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-10