Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran tarehe 9 alikagua miundombinu ya nyuklia iliyoko katika Natanz, kisha kwenye mkutano wa kusherehekea mafanikio ya shughuli za nyuklia alisema, Iran imekuwa na uwezo wa kuzalisha nishati ya nyuklia, na kusema kwamba tokea hapo Iran "imejiunga na klabu ya nyuklia". Kauli hiyo mara ilisababisha mshituko mkubwa kwa jumuiya ya kimataifa.
Bw. Mahmoud Ahmadinejad akiwa mbele ya maofisa waandamizi na waandishi wa habari alisema, "Maadui wanatumia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama ni chombo cha kuzuia Iran isipate maendeleo, lakini tokea leo Iran imekuwa moja ya nchi zenye uwezo wa kuzalisha nishati ya nyuklia duniani." Alisisitiza kwamba Iran inaendelea kuwa wazi kwa nchi za magharibi kuhusu mazungumzo ya suala la nyuklia.
Mwenyekiti wa kamati ya mambo ya kimataifa katika baraza la chini la Russia Bw. Konstantin Kosachev tarehe 9 huko Moscow alisema kauli ya rais Mahmoud Ahmadinejad ni uchokozi kwa jumuiya ya kimataifa.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-moon siku hiyo aliitaka Iran irejee kwenye mazungumzo na kusisitiza kuwa "ni muhimu sana" kwa nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, Iran, ifuate azimio la Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa ikulu ya Marekani Bw. Sean McCormack siku hiyo pia alisema, kitendo cha Iran cha kuinua uwezo wa kuzalisha nishati ya nyuklia ni kitendo kukiuka azimio la Baraza la Usalama, kitendo chake kinaonesha kuwa vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama kwa Iran ni "sahihi".
Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani ambayo ni nchi mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya imesema, mpango wa nyuklia wa Iran "unaelekea kwenye makosa".
Wizara ya mambo ya nje ya Uingereza ambayo imemaliza hivi punde tu mgogoro wa kidiplomasia na Iran, iliitaka jumuiya ya kimataifa ifanye juhudi za pamoja ili kuhakikisha Iran haipati silaha za nyuklia.
Kabla ya hapo wachambuzi walikadiria kuwa pengine kwenye mkutano huo Bw Ahmadinejad alitangaza kuwa Iran imefanikiwa kufunga mashinepewa 3,000 za kusafisha uranium, lakini siku hiyo hakutaja idadi gani ya mashinepewa zilifungwa katika sehemu ya Natanz.
Vyombo vya habari vimegundua kwamba hii ni mara ya kwanza kwa Iran kuthibitisha imekwisha funga mashinepewa tokea Iran ilipotangaza kuwa itafunga mashinepewa 3,000 miezi kadhaa iliyopita. Katika siku hiyo Mahmoud Ahmadinejad kwenye hotuba yake alisema, Iran siku zote inachukua msimamo wa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki na iliwahi kuruhusu watu wa shirika hilo kufanya ukaguzi nchini Iran. Lakini alipogusia azimio la Baraza la Usalama la kuiwekea vikwazo Iran, alizionya nchi za magharibi zisiilazimishe Iran "ifikirie upya" sera yake kuhusu suala la nyuklia. Lakini ni sababu gani Iran imetangaza kuwa imejiunga na "klabu ya nyuklia"?
Kwanza azimio la Namba 1747 la Baraza la Usalama lililopitishwa tarehe 24 Machi kuhusu suala la nyuklia la Iran lilisema suala la nyuklia la Iran liendelee kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo, lakini limeongeza ukali wake dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran. Lakini Iran inasisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia unalenga matumizi ya amani na itaendelea kushughulika na kazi ya kusafisha uranium.
Wachambuzi wanaona kuwa kauli ya Bw Mahmoud Ahmadinejad ina nia ya kuitangazia jumuiya ya kimataifa kwamba upinzani wa nchi za magharibi na vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama havifui dafu kwa mpango wa nyuklia wa Iran.
Pili, wachambuzi wanaona kuwa Iran inajaribu kupata hali ya "maji yaliyomwagika" ili kujipatia hadhi katika mazungumzo. Iran inaona kuwa mpango wake wa nyuklia ukiendelea haraka zaidi vitu vitakavyobakizwa vitakuwa vingi katika mazungumzo. Kabla ya hapo, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleezza Rice alisema haondoi uwezekano wa kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Iran kwenye mkutano wa kimataifa wa mawaziri utakaofanyika tarehe 3 na 4 katika mji wa Sharm-el-Sheikh nchini Misri. Sababu ya Iran kuchagua wakati huu kutangaza uwezo wake huo hakika inalenga kujipatia hadhi yake katika mazungumzo hayo.
Idhaa ya kiswahili 2007-04-10
|