Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-11 19:25:50    
Umoja wa Mataifa wasema kuongezeka kwa joto duniani kutaleta maafa makubwa kwa binadamu

cri

Shirika husika la Umoja wa Mataifa tarehe 10 mwezi Aprili lilitoa taarifa ikieleza athari zitakazoletwa moja kwa moja kwa maisha ya binadamu katika siku za baadaye kutokana na hali ya hewa duniani kubadilika kuwa joto. Taarifa inasema kama hali ya hewa duniani itaendelea kuongezeka kuwa joto zaidi, basi katika miongo kadhaa ijayo binadamu watakabiliwa na maafa makubwa.

Kamati maalumu ya mabadiliko ya hali ya hewa kati ya serikali za nchi mbalimbali ya Umoja wa Mataifa tarehe 6 huko Brussels ilitoa taarifa ya tathmini kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa ya duniani, taarifa hiyo yenye kurasa 1,572 ilitayarishwa na wanasayansi 441. Taarifa iliyotolewa tarehe 10 ni muhtasari tu wa taarifa iliyotolewa na kamati hiyo maalumu, ikiweka mkazo wa kunukuu sehemu kuhusu athari zinazoletwa na kuongezeka kwa joto duniani kwa maisha ya binadamu. Taarifa hiyo imefafanua kuhusu hali ya siku za baadaye ya baadhi ya maeneo makubwa yakiwemo ya Asia, Afrika, Oceania na nchi za visiwa zilizoko kwenye Pasifiki ya kusini.

Moja ya matokeo ya moja kwa moja yatakayotokana na kuongezeka kwa joto duniani ni kusababisha kupungua kwa mavuno ya chakula na kutishia moja kwa moja maisha ya binadamu, hususan kwa bara la Asia lenye idadi kubwa sana ya watu. Taarifa hiyo inasema endapo joto duniani litaongezeka kwa nyuzi 3.6, basi hadi mwaka 2050 uzalishaji mpunga nchini China utapungua kwa kati ya 5% na 12%, wakati mavumo ya ngano ya Bangladesh yatapungua kwa theluthi moja. Inakadiriwa kuwa idadi ya watu wenye njaa duniani itafikia milioni 50 ifikapo mwaka 2020, idadi hiyo ya watu itafikia milioni 132 katika miaka 30 ijayo, na kufikia milioni 266 mwaka 2080. Mbali na njaa, kutakuwa na tatizo lingine la upungufu wa maji ya kunywa. Taarifa imesema kutokana na kupungua kwa barafu kwenye mlima Himalaya, nchini India, watu milioni 100 watakabiliwa na upungufu wa maji.

Kutokana na kukabiliwa na mkumbo unaosababishwa na kuongezeka kwa joto duniani, bara la Afrika lililoko nyuma kimaendeleo ni dhaifu zaidi katika kupambana na mkumbo huo. Taarifa inasema hadi kufikia mwishoni mwa karne hii, kiasi cha watu bilioni 1.8 barani Afrika watakosa maji safi ya kunywa, ambapo kati ya 25% na 40% ya wanyama watatoweka duniani, hii itaathiri vibaya uchumi wa nchi za Afrika zinazochukulia utalii kuwa nguzo ya uchumi. Sambamba na kuongezeka kwa joto, maradhi mengi ya sehemu ya joto duniani yataenea, ambapo watu milioni 80 wataambukizwa ugonjwa wa malaria. Aidha hasara ya kiuchumi inayoletwa na kuongezeka kwa joto duniani kwa nchi za pwani barani Afrika itafikia kiasi cha 14% ya jumla ya thamani ya uzalishaji mali ya nchini ya nchi hizo.

Kwa nchi za Australia na New Zealand, ambazo ziko kwenye bara la Oceania, hali mbaya ya hewa ya huko itakayosababishwa na kuongezeka kwa joto duniani ni ukame, maafa ya moto, mafuriko ya maji, maporomoko ya udongo kwenye milima na kuwa na joto kupita kiasi.

Mafanikio mapya ya utafiti wa sayansi waliyoyapata watafiti wa chuo kikuu kimoja cha mjini Sydney Australia, ni kudungua uhusiano kati ya carbon dioxide na kiasi cha unga unaotoka kwenye maua (mbelewele) ulioko katika hewa, ikiwa hewa inakuwa joto zaidi, kiasi cha unga wa maua kilichoko katika hewa pia kinaongezeka, hali ambayo inaleta matatizo kwa wagonjwa wenye matatizo ya kupumua(asthma).

Taarifa hiyo inataka nchi zote duniani zichukue hatua mara moja kupunguza utoaji wa carbon dioxide, kulinda mazingira ya dunia na kuweka sera za kufuata njia ya maendeleo endelevu.