Tarehe 12 Aprili, waziri mkuu wa China Bw Wen Jiabao ambaye yuko ziarani Japan alitoa hotuba kuhusu "urafiki na ushirikiano" kwa wabunge zaidi ya 400 kwenye ukumbi wa baraza la chini la bunge la Japan. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa China kutoa hotuba kwenye bunge la Japan katika miaka 22 iliyopita.
Leo nimepata fursa ya kutoa hotuba kwenye bunge la Japan, na nafurahi kukutana na wabunge wa baraza la chini na la juu ya bunge la Japan. Nachukua fursa hii kuwatakia heri na baraka wabunge waliopo hapa na wananchi wa Japan, pia kuwashukuru kwa dhati tena kutoa heshima kubwa kwa marafiki wa sekta mbalimbali wa Japan waliotoa mchango mkubwa kwa ajili ya urafiki kati ya China na Japan katika miaka mingi iliyopita.
Waziri mkuu wa Japan Bw Shinzo Abe na waziri wa mambo ya nje pia walisikiliza hotuba ya Bw Wen Jiabao. Katika hotuba yake, Bw Wen Jiabao amesema, ili kuimarisha urafiki na ushirikiano, China na Japan zinatakiwa kurithi na kuenzi urafiki wa jadi ulioanzia tangu enzi na dahari. Kwenye mawasiliano kati ya nchi hizo mbili ya zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita, China na Japan zilifundishana na kuigana, na kusukuma mbele maendeleo ya kila upande. Hizo ndizo historia na mila za jadi na mali za ustaarabu zinazomilikiwa na pande mbili kwa pamoja, ambazo zinastahili kuthaminiwa.
Waziri mkuu Bw Wen Jiabao amedhihirisha kuwa, ili kuimarisha urafiki na ushirikiano, ni lazima kujumlisha na kukumbuka mafunzo ya historia katika miaka ile ya msiba. Vita vya kuivamia China vilivyoanzishwa na Japan viliwafanya wananchi wa China kukumbwa na balaa kubwa, pia viliwaletea msiba na huzuni nyingi wananchi wa Japan. Akisema:
Kusisitiza kukumbuka mafunzo ya historia siyo kuendelea na uhasama, bali ni kwa ajili ya kufungua vizuri siku za mbele. Tokea uhusiano wa kibalozi kati ya China na Japan uwe wa kawaida, serikali ya Japan na viongozi wa Japan wameeleza msimamo wao mara kwa mara kuhusu masuala ya historia, ambapo walikiri hadharani uvamizi wa Japan, wakijikosoa kwa kina na kuomba radhi kutoka kwa nchi zilizokumbwa na balaa hilo. Serikali ya China na wananchi wake walisifu hali hiyo. Tuna matumaini ya dhati kuwa, upande wa Japan utachukua hatua halisi kuonesha msimamo wao na kutimiza ahadi zao. China na Japan zikishirikiana zitapata manufaa ya pamoja, na zikipambana zitapata madhara ya pamoja. Kutimiza urafiki wa vizazi kwa vizazi kati ya wananchi wa China na Japan kunalingana na mkondo wa historia na matumaini ya wananchi wa nchi hizo mbili, pia ni matarajio ya dhati ya nchi za Asia na jumuiya ya kimataifa.
Bwana Wen Jiabao amesema katika hali mpya ya historia, China na Japan zina maslahi ya pamoja yanayozidi kuwa makubwa siku hadi siku, na zinakabiliwa na changamoto kubwa ambazo zinapaswa kushirikiana kukabiliana nazo. China na Japan kujenga ushirikiano wa kimkakati na wa kunufaishana kunafuata mkondo na nia ya wananchi. Bwana Wen Jiabao alisema:
Nyaraka tatu za kisiasa ikiwemo pamoja na "Taarifa ya pamoja ya China na Japan" ni majumuisho ya kisiasa, kisheria na kihalisi ya uhusiano wa zamani kati ya nchi hizo mbili, na kupanga mpango kuhusu siku za usoni za uhusiano wa nchi hizo mbili, hili ni jiwe la msingi la uhusiano kati ya China na Japan. Bila kujali zinakutana na hali ya namna gani, kama pande hizo mbili zinaweza kufuata kwa makini kanuni mbalimbali zilizothibitishwa kwenye nyaraka hizo tatu za kisiasa, basi uhusiano kati ya nchi hizo mbili utaweza kusonga mbele bila matatizo.
Bwana Wen Jiabao alipozungumza suala la Taiwan alisema, suala la Taiwan linahusiana na maslahi makuu ya taifa la China. China itafanya juhudi kadiri iwezavyo ili kutatua suala hilo kwa njia ya amani, lakini kamwe haitaruhusu shughuli za kuifanya Taiwan ijitenge na taifa la China, hivyo inaitaka Japan ifuate ahadi yake na kushughulikia suala hilo kwa tahadhari.
Katika hotuba yake, waziri mkuu Wen Jiabao amesisitiza tena msimamo wa China wa kufuata njia ya maendeleo ya amani.
|