Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-13 18:30:10    
Je, Korea ya Kaskazini inaweza kufunga miundo mbinu ya nyuklia ya Yongbyon kwa wakati?

cri

Tarehe 14 Aprili ni siku ya mwisho kwa Korea ya Kaskazini kufunga miundo mbinu ya nyuklia ya Yongbyon. Hii ni siku iliyowekwa katika makubaliano ya duru la tano la mazungumzo ya pande sita, kuweza au kutoweza kwa Korea ya Kaskazini kufunga miundo mbinu hiyo kwa wakati uliopangwa ni suala linalofuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa.

Kwa mujibu wa makubaliano yaliyopitishwa tarehe 13 Februari katika duru la tano la mazungumzo ya pande sita, Korea ya Kaskazini inapaswa kufunga miundo mbinu yake ya nyuklia kwenye kinu cha Yongbyon katika muda wa siku 60 yaani siku ya mwisho ni tarehe 14 Aprili. Kufunga miundo mbinu ni hatua ya kwanza kwa Korea ya Kaskazini kuacha kabisa mpango wa nyuklia. Lakini Korea ya Kaskazini inapotekeleza hatua hiyo ya kwanza, suala la kuzuiliwa kwa fedha zake katika benki ya Macau limekuwa kikwazo. Marekani haikutimiza ahadi yake ya kukwamua fedha hizo ndani ya siku 30, na Korea ya Kaskazini inashikilia msimamo wa kutoshiriki tena kwenye mazungumzo ya pande sita kabla ya kupata fedha zake, kwa hiyo mazungumzo yaliyopangwa kufanyika tarehe 19 Machi yalikwama.

Tarehe 10 Aprili Wizara ya Fedha ya Marekani na serikali ya mkoa wa utawala maalum wa Macau wa China zilitangaza kuwa dola milioni 25 za Kimarekani za Korea ya Kaskazini zilizozuiliwa katika benki ya Macau zitarudishwa kwa Korea ya Kaskazini. Lakini Korea ya Kaskazini haikujibu lolote kuhusu suala hilo ambalo ni sharti la kwanza kwa nchi hiyo kutekeleza hatua ya kwanza ya kufunga miundo mbinu ya nyuklia. Kabla ya hapo, kiongozi wa ujumbe wa Korea ya kusini unaohudhuria mazungumzo ya pande 6 Bwana Chun Yung Woo alizitaka pande mbalimbali zidumishe uvumilivu. Na tarehe 12 alisema huko Seoul kuwa, Korea ya kaskazini haitaki kukiuka waraka wa pamoja wa tarehe 13 Februali wa pande 6 zilizohudhuria mazungumzo kuhusu suala la nyuklia la peninsula ya Korea, hivyo hakuna haja ya kujali sana kikomo cha siku ya utekelezaji wa waraka wa pamoja. Na kiongozi wa ujumbe wa Marekani Bwana Christopher Hill tarehe 12 alipofanya ziara nchini Korea ya kusini alisema, hivi sasa bado kuna uwezekano wa kuchukua hatua kwa Korea ya kaskazini katika siku mbili za mwisho. Shirika la habari la AP limesema, Bwana Hill alisema, atafanya ziara mjini Beijing tarehe 13, na anapenda kukutana na kiongozi wa ujumbe wa Korea ya kaskazini mjini Beijing.

Hivi karibuni mkuu wa jimbo la New Mexico la Marekani Bw. Bill Richardson na mshauri mwandamizi wa rais wa Marekani kuhusu masuala ya Korea Bw. Victor Cha walifanya ziara ya siku nne nchini Korea ya Kaskazini na tarehe 11 walifanya ziara Korea ya Kusini, Bw. Victor Cha huko Seoul alipozungumza na waandishi wa habari alisema, alipokuwa ziarani nchini Korea ya Kaskazini alitangaza uamuzi wa Marekani wa kukwamua fedha za Korea ya Kaskazini zilizozuiliwa, lakini Korea ya Kaskazini haikutaja siku ya mwisho ya kufunga miundo mbinu ya nyuklia. Bw. Bill Richardson alisema, Korea ya Kaskazini imewahi kusema kuwa itaanza kufunga miundo mbinu ya nyuklia ndani ya muda wa saa 24 baada ya kupata fedha zake na kuruhusu wakaguzi wa kimataifa kwenda Korea ya Kaskazini.

Na msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bwana Qin Gang tarehe 12 alipozungumzia suala kuhusu kuondolewa kizuizi kwa fedha za Korea ya kaskazini alisema, China inaona taarifa iliyotolewa na serikali ya mkoa wa utawala maalum wa Makau, pia iliona taarifa iliyotolewa na wizara ya fedha ya Marekani kabla ya hapo, na inafanya mawasiliano na pande zinazohusika, na ina matumaini kuwa suala kuhusu fedha za Korea ya kaskazini litatuliwa mapema iwezekanavyo.

Vyombo vya habari vimesema dalili mbalimbali zinaonesha kuwa, Korea ya kaskazini kufunga miundo mbinu ya nyuklia ya Yongbyon kwa wakati, bado ni jambo linalostahili kutarajiwa.