Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-16 14:51:58    
Ni kwa nini mazungumzo kati ya viongozi wa Palestina na Israel hayakuhusisha masuala nyeti?

cri

Waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert na mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas tarehe 15 walifanya mazungumzo huko Jerusalem. Hayo ni mazungumzo ya kwanza kati yao tangu utaratibu wa viongozi hao wawili kukutana kila baada ya kipindi fulani uanzishwe. Katika mazungumzo hayo, walijadiliana kuhusu suala la usalama na kuzidi kupunguza vikwazo dhidi ya maisha ya Wapalestina, lakini mazungumzo hayakuhusisha masuala makuu nyeti kama vile mamlaka ya Jerusalem, hali ya wakimbizi wa Palestina kurudi nyumbani na mipaka ya mwisho kati ya Palestina na Israel, kwa sababu Bw. Olmert hataki kujadili masuala hayo.

Wachambuzi wanasema Israel siku zote inasisitiza kuwa, masuala hayo makuu hayatazungumzwa hadi Palestina itakapokubali masharti matatu yaliyotolewa na pande 4 zinazohusika na suala la Mashariki ya Kati, yaani kutambua nchi ya Israel, kuacha matumizi ya mabavu na kupokea makubaliano yaliyofikiwa zamani na pande hizo mbili. Lakini kutokana na mwongozo uliotangazwa na serikali ya mungano wa taifa ya Palestina iliyoundwa mwezi uliopita, serikali hiyo inashikilia msimamo wa kutoitambua Israel na kuendelea na mapambano ya kimabavu dhidi ya Israel kwani inaona hii ni haki halali ya Wapalestina.

Sababu nyingine ya Israel kutojadili masuala makuu na Palestina, ni "pendekezo la amani la nchi za kiarabu". Mkutano wa wakuu wa Umoja wa nchi za kiarabu uliofanyika mwezi uliopita ulitoa dhana ya kuzindua tena "pendekezo la amani la nchi za kiarabu" lililotolewa mwaka 2002. Baada ya mkutano huo, pande husika zilikuwa na mjadala mwingine na kupendekeza kuunda kamati moja ya utekelezaji wa pendekezo hilo kwenye mkutano wa mawaziri wa Umoja wa nchi za kiarabu utakaofanyika tarehe 18 mwezi Aprili. Kamati hiyo itafanya mazungumzo na Israel ili kutimiza lengo la kubadilishana amani kwa ardhi. Serikali ya Israel imesema ingependa kutafiti dhana hiyo, kwani kati ya nchi za kiarabu si Palestina peke yake itakayohusika na mazungumzo hayo. Hata hivyo Israel bado haijaamua kukubaliana na dhana hiyo.

Kwa sasa upande wa Palestina nao hauko tayari kujadili masuala makuu na Israel. Kabla ya Bw. Abbas kwenda Jerusalem, maofisa walioambatana naye walidokeza kuwa kwenye mazungumzo hayo upande wa Palestina utazingatia masuala ya usalama na misaada ya kiuchumi. Tangu serikali ya mungano wa taifa ya Palestina iundwe, nchi za magharibi hazijarejesha misaada ya moja kwa moja, kwa kuwa sera ya serikali hiyo hailingani na matakwa ya pande 4 zinazohusika na suala la Mashariki ya Kati. Huko Palestina kiwango cha maisha ya watu kinazidi kushuka, watumishi wanafanya migomo mara kwa mara kulalamika kushindwa kupata mishahara. Mbali na hayo mapambano ndani ya Palestina yamepungua baada ya kuundwa kwa serikali hiyo, lakini bado hayajamalizika kabisa. Kutokana na hali hiyo, Bw. Abbas anataka sana kupata ushirikiano wa Israel ili kupunguza msukosuko wa hivi sasa.

Kwa hiyo pande mbili za Palestina na Israel zote zimetambua kuwa, ni afadhali kupata ufumbuzi wa matatizo halisi badala ya kupoteza wakati katika kujadiliana masuala nyeti ambayo hayawezi kutatuliwa mara moja kwa hivi sasa. Baada ya mazungumzo hayo, pande hizo mbili za Palestina na Israel zote zilisema hayo ni mazungumzo mazuri, kwa sababu yanasaidia kuanzisha uaminifu kati ya viongozi wa Palestina na Israel.

2007-04-16