Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-17 16:20:01    
Barua 0415

cri

Msikilizaji wetu Philip Machuki wa Kijiji cha Nyankware Sanduku la posta 646 Kisii nchini Kenya anaanza barua yake kwa salamu nyingi kwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Anasema yeye lengo lake hasa ni kueleza machache aliyonayo kuhusiana na mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwezi Novemba mwaka jana. Anasema Mkutano huo ambao uliandaliwa vizuri na China umeonesha urafiki mkubwa kati ya China na nchi za Afrika. Si nchi nyingi zinazopenda kushirikiana na bara la Afrika, China imetoa mfano mzuri na juhudi zake za kusaidia kufufua uchumi wa nchi za Afrika zinastahili kupongezwa.

Bw Machuki pia anasema tangu China ianzishe uhusiano wa kibiashara na Kenya, imekuwa ikionesha mfano mzuri kwenye kutoa misaada, kwa sababu misaada inayotolewa sababu haina masharti, na wakenya wamepata fursa ya kununua bidhaa kwa bei nafuu sana kutoka China. Bwana Machuki pia anachukua fursa hii kuipongeza idhaa ya Kiswahili ya radio China kimataifa kwa kuandaa vipindi maalum kwa ajili ya mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, kupitia matangazo ya vipindi hivyo watu wengi walinufaika na kufahamu yote yaliyokuwa yanajiri katika mkutano huo.

Mwisho Bw. Machuki anamaliza barua yake kwa kusema shule anayosoma kuna wanafunzi zaidi ya 30 ambao wanapenda kushiriki katika chemsha bongo ya mwaka huu, hivyo wanaomba watumiwe bahasha na majarida kutoka China. Anasema anautakia urafiki kati ya China na Afrika udumu, na pia ametutakia wafanyakazi wa Radio China kimataifa na Wasikilizaji kila la heri.

Baada ya kuwasomea barua ya Msikilizaji Philip Machuki, sasa tuna barua kutoka kwa Bw Mogire machuki ambaye naye amaeanza kwa kutusalimu wafanyakazi wa Radio China kimataifa na Wasikilizaji wenzake, anasema yeye ni mzima na anaendelea kusikiliza matangazo yetu kupitia shirika la utangazaji la Kenya KBC. Anasema ilikuwa ni jambo la busara kuamua kurusha matangazo kupitia KBC. Kwani ni kwa kupitia matangazo ya Radio China kimataifa yanayosikika kwenye KBC, yeye na Wasikilizaji wengine wengi waliweza kufuatilia vizuri mkutano wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, mpaka ulipofungwa.

Anasema mikataba iliyosainiwa kati ya China na Afrika kwenye mkutano wa Beijing, itasaidia sana kuboresha maisha ya watu wa Afrika, nchini Kenya wanafurahia sana misaada ambayo itagharimiwa na serikali ya China ikiwemo ukarabati wa uwanja wa michezo wa kasarani. Heka heka za mwaka 2006 za kuzidisha ushirikiano kati ya China na Afrika zimedhihirisha kuwa China na nchi za Afrika ni ndugu na uhusiano wao ni wa kudumu. Ni matumaini yake kuwa Radio China kimataifa itaendelea na kasi ya kuwafahamisha wasikilizaji wake habari muhimu zitakazosaidia kujenga urafiki kati ya China na Afrika.

Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu hawa Philip Machuki na Mogire Machuki kwa barua zao, zilizotukumbusha heka heka za mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika. Tunafurahi kusikia kuwa matangazo yetu yaliweza kuwajulisha mengi kuhusu mkutano huo. Na Bw Philip, tunapenda kukumbusha kuwa Radio China kimataifa iko wazi kwa kila mtu, kwa hiyo hao rafiki unaosoma nao, wako huru kushiriki kwenye shindano la chemsha bongo, wasikilize matangazo yetu na kujibu kwa makini maswali, na kututumia majibu.

Mzee Athumani O. Matimbwa wa S.L.P 4608 Dar es salaam nchini Tanzania, anaanza barua yake kwa kuipongeza Radio China Kimataifa kwa kuwa daraja la urafiki kati ya China na mataifa ya Afrika, urafiki ambao unadumishwa kwa manufaa ya wananchi wote wa pande zote. Bw. Matimbwa anaendelea kusema, Radio China kimataifa inasikika nchini Tanzania na anawapongeza watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa.

Bw Matimbwa anasema wakati tulipokuwa tunaukaribisha mwaka wa 2007, Marekani na washirika wake bado walikuwa wanaendeleza ukaliaji kwenye mataifa mengine huku umoja wa mataifa ukiwa umekaa kimya. Waisrael na wapalestina wanaendelea kuishi katika hali ya uhasama. Anasema mikataba ya kiujanja ujanja inafanyika wananchi wa Palestina wanaendelea kuangamizwa kila siku, anauliza ni kwa nini dunia haisimamishi umwagaji damu huko mashariki ya kati??

Kwenye barua yake nyingine Bw Matimbwa anasema analipongeza jarida la daraja la urafiki ambalo liliwawezesha kufahamu mengi, wasikilizaji wanasubiri kwa hamu toleo lingine. Anasema pia atashukuru sana kama siku moja atapata nafasi ya kwenda kwenye msikiti mmoja mkubwa wa hapa China. Pia Bwana Matimbwa anasema amesema wenye kitabu kinachoitwa "Uislamu nchini China" na kufahamu kuwa kuna msikiti wa Dong si wenye mkataba hapa Beijing. Anafahamu kuwa kwenye mkataba ya msikiti huo, kumehifadhiwa kitabu kitakatifu cha dini ya kiislamu ambacho kilichukuliwa kwenye jumba la kifalme la enzi ya Qing.

Pia anasema kwenye kitabu hicho "uislamu nchini China" amesoma kuhusu mwalimu mmoja wa kabila la Wahui la China alisaidiwa na Ma Lian Yuan na Ma Qi hua kuchonga maneno ya Quran kwenye mianzi, huko mkoani Yunnan, Na baadaye waliwaajiri watu 30 hodari wa kuchonga Quran yenye juzuu 30. Pia amefahamu kuwa hapa China kuna ushonaji wa mitindo ya Kiarabu, na vitu vilivyoshonwa pia vinaweza kupatikana kwenye maktaba ya Dong si.

Anaomba kama kuna siku watangazaji wa Idhaa ya Kiswahili wakitembelea msikiti huo, basi tumtumie anuani ya msikiti, duka lake la vitabu, madrasa yake. Anasema kuwa amefahamu yote haya kwa kuwa yeye amekuwa msomaji mkubwa wa majira ya China ya tokea miaka ya 70.

Tunamshukuru sana Msikilizaji wetu mzee Matimbwa kwa ufuatiliaji wake mkubwa wa matangazo yetu na hata majarida yetu. Barua yake imetuonesha ufuatiliaji wake wa muda mrefu wa matangazo yetu, hali ya dini nchini China, na hata hali ya mambo inavyoendelea katika sehemu mbalimbali duniani kupitia matangazo yetu. Si watu wengi wanaoweza kukumbuka mambo ambayo idhaa yetu iliyafanya kwenye miaka ya sabini, lakini kupitia barua yako tumetambua kuwa hata mambo ya muda mrefu uliopita bado yapo kwenye kumbukumbu za wasikilizaji wetu, Tunafurahi na kushukuru sana.

Bibi Jendeka Goldah Vuyiya wa Sanduku la Posta 172 Bungoma nchini Kenya, ametuandikia barua akisema anatushukuru sana kwa kuendelea kuwasiliana naye. Anasema yeye anazidi kuiombea baraka idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa katika mwaka huu wa 2007. Kutokana na yale aliyoambiwa na Bw Mutanda Ayub Sharif aliyetembelea ofisi zetu, anafahamu kuwa kuna pilikapilika nyingi sana za kazi. Anawashukuru viongozi wa Radio China kwa kumuwezesha Mutanda kutembelea China, kwa sababu toka utotoni walikuwa wanafahamu kuwa kuna nchi inayoitwa China, lakini hawakufahamu kama kuna siku bahati itatokea na wataweza kutembelea China, lakini bahati ilimfikia Bw Mutanda.

Pia Bibi Jendeka anasema wanamshukuru Bw Mutanda kwa kuwahimiza kusikiliza matangazo yetu, na wanamheshimu sana huko Mkoani wa magharibi kutokana na juhudi zake. Jambo lingine ambalo hapendi kulisahau ni zawadi kama T-shirt yenye maandishi ya Radio China kimataifa na kalenda ya mwaka 2007, anashukuru sana kwa zawadi hizo. Anasema maswali kuhusu chemsha bongo alikwishapata, na sasa anaendelea kusikiliza matangazo yetu ili aweze kupata majibu na kujibu maswali hayo

Bwana Mutanda Ayub Sharifu wa huko Bungoma Kenya ametuandikia barua akitukumbusha kuhusu safari yake ya kutembelea hapa China. Anasema kusafiri kwenda China sio jambo rahisi. Na pia anakumbusha usemi wa Kiswahili, "baada ya dhiki faraja". Anasema yeye alisikiliza, anasikiliza na ataendelea kusikiliza matangazo ya Radio China kimataifa. Na anawaombea wasikilizaji wenzake wapate bahati kama yake, ili waweze kuitembelea China na wajionee ukarimu wa wachina.

Anasema anakumbuka alipofika hapa China, kama ilivyokuwa kwa mwenzake Bw Ngogo hawakujua hali ya hewa itakuwaje, kumbe kulikuwa na baridi kali. Lakini kutokana na ukarimu mkubwa wa wenyeji wake alipata nguo za kujikinga dhidi ya baridi kutoka kwa wafanyakazi a idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, na hata wengine waliweza kujitolea pesa zao kwa ajili ya matumizi madogo madogo safarini, na hizo pesa zilimwezesha kujimudu na kufurahi, anauliza ni nani ambaye hawezi kushukuru kwa ukarimu kama huo?

Bwana Mutanda anakumbusha kuwa alifahamu kuwa sio rahisi kwa mtu kupata nafasi ya tuzo maalumu kutalii nchini China, lakini anajua kuwa inawezekana. Anaamini kupitia maombi na juhudi, na kwa bahati inawezekana. Kwa hiyo anawahamasiha wasikilizaji waendelee kushiriki kwenye chemsha bongo kwani kutokana na juhudi na bahati wanaweza kupata nafasi hii. Anasema kupata ushindi kweli siyo lengo la mwisho la kushiriki kwenye chemsha bongo, la muhimu ni kupata ujuzi zaidi kuhusu China, lakini ni bahati nzuri kuwa Radio China kimataifa imeweka zawadi hiyo, ili kuwafurahisha wasikilizaji wake bahati na nafasi inapotokea. Anasema anaipa idhaa ya Kiswahili changamoto iweze kuendelea na mwendo huohuo, na bila shaka wasikilizaji wengi wataendelea kuiunga mkono Idhaa ya Kiswahili ya Radio China.

Bw Benson Irungu Njambuya wa sanduku la Posta 832, Bungoma Kenya, anasema anamshukuru mungu kwa kumwezesha kuwasiliana na Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Anaipongeza Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kwa matangazo yanayopitia shirika la Utangazaji Kenya KBC. Anasema kupitia matangazo hayo ameweza kujifunza mengi kuhusu China, na ameweza kuunganishwa na wasikilizaji wengine kutoka sehemu mbalimbali duniani. Mwisho anatoa shukrani zake za dhati kwa zawadi ya picha, anasema hakika picha ya ukuta mkuu wa China inampa kumbukumbu za enzi za kale za China.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-17