Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-18 16:15:07    
Iran yaonesha tena msimamo mkali kuhusu suala la nyuklia

cri

Mwenyekiti wa shirika la nishati ya atomiki la Iran Bw. Gholam Reza Aghazadeh tarehe 17 katika mji wa Natanz alisema, kazi ya kufunga mashinepewa katika mji huo haijawahi kusimama, na Iran itajitahidi kadiri iwezavyo kukamilisha mpango wake wa kufunga mashinepewa elfu 50.

Vyombo vya habari vinaona kuwa msimamo aliouonesha Bw. Aghazadeh unadhihirisha kuwa Iran itaendelea kukamilisha mpango wake wa nyuklia pamoja na kukabiliana na shinikizo la kimataifa.

Bw. Aghazadeh alisema, kazi ya kuongeza mashinepewa kwenye kinu cha Natanz inaendelea vizuri, ingawa kazi ya kukamilisha mashinepewa elfu 50 inahitaji miaka miwili hadi mine, hata hivyo Iran inadhamiria kuukamilisha mpango huo uliowekwa.

Katika hotuba yake Bw. Aghazadeh alisisitiza kuwa ikiwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaendelea kuiwekea Iran vikwazo vipya, nchi husika hakika "ztaathirika", kwani Iran inaona mapambano ya suala la nyuklia "yataziathiri vibaya pande zote mbili". Bw. Aghazadeh amezitaka nchi za magharibi zifanye "mazungumzo ya makini" na Iran.

Vyombo vya habari vinaona kuwa lengo la Iran la kutangaza mara kwa mara mafanikio yake ya mpango wa nyuklia ni kutaka kupata faida kadiri inavyowezekana katika mvutano dhidi ya Marekani na nchi za magharibi. Sasa suala la nyuklia la Iran limekuwa kama donge la theluji linalovingirika kutoka mlimani, ambalo linazidi kuwa kubwa na kuwa mbali kila baada ya muda kupita. Iran inaona kuwa kwa sasa nchi za magharibi haziwezi kuzuia kirahisi "donge hilo la theluji" lisivingirike. Nchi za magharibi zinachoweza kufanya sasa ni kupunguza pole pole kasi ya donge hilo na mwishowe kulisimamisha. Tuache kama ni kweli au uwongo Iran imekuwa na uwezo wa kuzalisha nishati ya nyuklia kwa kiwango cha uzalishaji wa kiwanda, na kama ni kweli au uwongo imekuwa na uwezo wa "kuzifanya mashinepewa 3,000 zifanye kazi kwa pamoja", lakini kama vyombo vya habari vinavyosema kwamba msimamizi wa "donge hilo la theluji", Iran, amekwisha pata nafasi nzuri katika mvutano huo.

Kwanza, ingawa Baraza la Usalama limepitisha maazimio mawili ya kuiwekea vikwazo Iran tokea mwezi Desemba mwaka jana, lakini maazimio hayo yanahusu tu mpango wa nyuklia na mpango wa makombora, na hayahusiani na maisha ya raia wala uchumi wa taifa. Iran inaona kuwa maazimio hayo hayaathiri msingi wake wa taifa. Zaidi ya hayo, msimamo wa serikali ya Mahmoud Ahmadinejad mbali na kuungwa mkono na wahafidhina unaungwa mkono na wananchi wengi.

Pili, Iran inaona kuwa hapakosi nchi ambayo imebaki na mafanikio yake ya nyuklia baada ya "vuta nikuvute". Kwa hiyo katika suala la nyuklia, Iran siku zote inajaribu kuleta "hali iliyoiva", na inaona kwamba hatua zake zikiwa kubwa zaidi katika mpango wake wa nyuklia, itabaki na mafanikio mengi zaidi katika mazungumzo yatakayofanyika. Kutokana na hayo, maofisa wa Iran mara nyingi wanasisitiza kuwa hata kama kufunga mashinepewa elfu 50 kutahitaji muda mrefu kiasi gani, Iran itakamilisha tu mpango huo. Ni dhahiri kwamba Iran inataka kuongeza sauti yake katika mazungumzo kwa kujipatia "teknolojia ya kutosha ya nyuklia".

Lakini, wachambuzi wanaona kuwa msimamo mkali unautumiwa na Iran siku zote na kupuuza maazimio ya Baraza la Usalama hausaidii nchi za magharibi kuondoa wasiwasi wao kuhusu nia ya mpango wa nyuklia na kujenga imani kati ya pande mbili. Hali ya hivi sasa ya kutoafikiana katika suala la nyuklia la Iran inaweza tu kuvunjwa jinsi Iran itakavyochukua msimamo wake. Msimamo mkali sio utatuzi mzuri kabisa, bali ni mazungumzo tu ndiyo njia inayoweza kuepusha matokeo ya "pande zote mbili kuathirika vibaya".