Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-19 13:33:12    
Watu elfu 50 wametoa maombi ya kununua tiketi za michezo ya Olimpiki katika siku ya kwanza baada ya tiketi za michezo hiyo zianze kuuzwa

cri
Tangu tiketi za michezo ya Olimpiki ya Beijing zianze kuuzwa tarehe 15 Aprili, katika siku ya kwanza peke yake, watu zaidi ya elfu 50 walitoa maombi ya kununua tiketi zipatazo laki 2.5 kwa kupitia tovuti ya michezo hiyo kwenye mtandao wa Internet. Imefahamika kuwa, uuzaji wa tiketi za michezo ya Olimpiki utakuwa na vipindi vitatu. Kipindi cha kwanza ni kuanzia mwezi Aprili mwaka 2007 hadi mwezi Septemba mwaka 2007, ambapo tiketi zote elfu 26 za sherehe ya ufunguzi na ya ufungaji wa michezo ya Olimpiki pamoja na nusu ya tiketi za michuano zitauzwa, na watu wanaweza kutoa maombi ya kununua tiketi, halafu kupata nafasi ya kununua tiketi kwa bahati nasibu. Katika kipindi cha pili ambacho ni kati ya mwezi Oktoba na Desemba mwaka 2007, nusu nyingine ya tiketi za michuano pamoja na tiketi zilizosalia kwenye uuzaji wa kipindi cha kwanza zitauzwa, na watu watakaotangulia kutoa maombi watapata nafasi ya kuzinunua. Kipindi cha tatu kitaanza mwezi Aprili mwaka 2008 hadi michezo ya Olimpiki itakapomalizika, ambapo watu wataweza kununua moja kwa moja tiketi za michezo hiyo.

Ofisa wa kamati ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing amedokeza kuwa, inakadiriwa kuwa tiketi zote za michezo hiyo zitauzwa kwa jumla ya dola za kimarekani milioni 140. Hivi sasa watu wa China wana hamu kubwa ya kutazama michezo hiyo, na watu wa nchi za nje pia wameonesha nia kubwa ya kununua tiketi hizo kuliko ilivyokuwa kwenye michezo ya Olimpiki ya Athens mwaka 2004. Mbali na hayo kutokana na sera ya kuwa tiketi nafuu inayofuatwa na kamati ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing, tiketi za michezo hiyo zitakazoshindwa kuuzwa zinatazamiwa kuwa chache. Katika historia michezo ya Olimpiki ya Sydney ya mwaka 2000 ilitia fora katika uuzaji wa tiketi ambapo zaidi ya asilimia 90 ya tiketi ziliuzwa. Inakadiriwa kuwa, uuzaji wa tiketi za michezo ya Olimpiki ya Beijing utafikia kiwango hicho.

Imefahamika kuwa asilimia 14 ya tiketi za michezo ya Olimpiki ya Beijing zitauzwa kwa watoto na vijana kwa bei ya chini za Yuan 5 na 10, ambapo Yuan 8 ni sawa na dola 1 ya kimarekani. Hii ni sehemu ya mpango wa kueneza ujuzi na moyo wa Olimpiki miongoni mwa watoto na vijana, na kusaidia kuendeleza shughuli za michezo shuleni.

Teknolojia za kisasa za kutambua nyuso za watu zitatumika wakati michezo ya Olimpiki itakapofanyika mwaka 2008 mjini Beijing. Imefahamika kuwa vyombo vinavyotumia teknolojia hizo itaweza kutambua kwa haraka nyuso za magaidi na watu wengine wanaoweza kutenda uhalifu kutoka kwenye kundi la watu, na kuzuia watu hao wasiingie kwenye maeneo nyeti ya viwanja na majumba ya michezo. Msingi wa teknolojia hizo ni miundo tofauti ya mifupa ya watu, ambapo data kuhusu nyuso za watu wapatao bilioni 1.3, wakiwemo raia wa China na wa nchi na sehemu nyingine duniani, zitahifadhiwa kwenye maktaba ya data ya vyombo vinavyotumia teknolojia hizo. Watu watakapoingia kwenye viwanja na majumba ya michezo ya Olimpiki, vyombo hivyo vitalinganisha nyuso zao na data zilizokuwepo, hivyo kuwasaidia walinzi wagundue kwa haraka watu wa hatari. Imefahamika kuwa mbali na viwanja na majumba ya michezo ya Olimpiki, vyombo hivyo pia vitafungwa kwenye masoko makubwa 500 mjini Beijing ndani ya miaka miwili.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-19