Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-19 15:53:34    
Hali ya usalama nchini Iraq inazidi kuwa mbaya

cri

Waziri mkuu wa Iraq Bw. Nuri al-Maliki tarehe 18 alisema jeshi la usalama la Iraq litapokea mamlaka ya kusimamia usalama wa taifa, lakini masaa machache tu baada ya kutoa kauli hiyo kulitokea milipuko minne mjini Baghdad, watu karibu 200 walikufa na 250 kujeruhiwa. Hili ni tukio kubwa kabisa tokea jeshi la Marekani nchini Iraq na jeshi la usalama la Iraq kuanza kutekeleza mpango mpya wa usalama mwezi Februari.

Habari zinasema, tarehe 18 mlipuko mmoja tu wa bomu la gari uliotokea katika soko la Sadriya mjini Baghdad ambalo lina wateja wengi zaidi ambao ni waumini wa madhehebu ya Shia ulisababisha vifo vya watu 118 na wengine 139 kujeruhiwa. Katika muda wa saa chache tu tokea Bw. Maliki atangaze kuwa Iraq itapokea mamlaka ya kusimamia usalama wa kitaifa kutoka majeshi ya nchi za nje, milipuko kadhaa ilitokea, na ni dhahiri kwamba milipuko hiyo ilipangwa kwa ushirikiano. Kwenye sehemu ya mlipuko watu walioshuhudia walisema, maiti zilitapakaa na watu waliokuwa ndani ya basi dogo walichomwa moto. Kwa hasira mwanamume mmoja alipiga kelele akisema, "Yuko wapi Maliki? Mwambie aje aone!"

Tokea mwezi Februari kufuatia mpango wa serikali ya Marekani kuongeza askari nchini Iraq, askari maelfu kwa maelfu wa jeshi la Marekani na jeshi la usalama la Iraq walimiminika mjini Baghdad ili kuimarisha usalama na kudhibiti vitendo vya kulipizana kisasi kati ya waumini wa madhehebu ya kidini, lakini hawajafanikiwa. Mlipuko uliotokea tarehe 18 unaashiria kwamba hali mbaya zaidi inaikabili serikali ya Maliki, ambayo inataka kurudisha hali ya usalama na amani. Sababu ni kwamba:

Kwanza, milipuko inachochea zaidi uhasama na kulipizana kisasi kati ya madhehebu ya kidini na kusababisha watu kupoteza imani na serikali ya Maliki. Mlipuko wa tarehe 18 ulikuwa unawalenga waumini wa madhehebu ya Shia, na kundi la al Qaeda linatuhumiwa kuwajibika na mlipuko huo. Kabla ya hapo "jeshi la Mehdi" lililo chini ya Bw. Moqtada al-Sadr wa madhehebu ya Shia lilikuwa kimya katika harakati za "sheria na utaratibu" zilizoanzishwa na majeshi ya Marekani na Iraq tangu katikati ya mwezi Februari, lakini sasa litafanya vitendo vingi mfululizo vya kulipiza kisasi. Kama hivyo ndivyo, hali ya usalama itakuwa mbaya na haitaweza kudhibitiwa. Zaidi ya hayo serikali ya Maliki haikufanikiwa chochote katika juhudi za kupambana na vitendo vya mauaji na kusuluhisha migongano kati ya madhehebu ya kidini. Watu wamepoteza imani na serikali yake.

Pili, tokea majeshi ya nchi mbalimbali yanayoongozwa na Marekani kusambaratisha jeshi la Saddam mwaka 2003, jeshi la Marekani limekuwa likifundisha jeshi la usalama la Iraq, lakini mlipuko wa tarehe 18 umedhihirisha kuwa jeshi hilo linalotegemea jeshi la Marekani, haliwezi kubeba jukumu la kuhakikisha usalama nchini Iraq. Namna ya kubadilisha hali hiyo ni tatizo linaloshinikiza serikali ya Maliki itafakari kwa makini.

Tatu, kutokana na kuifuata serikali ya Bush katika mpango wa kuondoa majeshi kutoka Iraq, serikali ya Maliki imekuwa katika hatari ya kutengwa na watu wa Iraq, na mlipuko uliotokea tarehe 18 hakika utaongeza malalamiko ya madhehebu ya Shia dhidi ya serikali na serikali hiyo ikipoteza uungaji mkono wa madhahebu ya Shia, msingi wake wa kisiasa utafifia zaidi.