Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-20 15:26:09    
Maonesho ya biashara ya Guangzhou yaweka msingi wa kuhimiza bidhaa za Afrika kusafirishwa nje

cri

Maonesho ya 101 ya bidhaa zinazosafirishwa nje na zinazoagizwa kutoka nje ya China? yaani maonesho ya biashara ya Guangzhou yatafanyika kati ya tarehe 15 na 20 mwezi huu huko Guangzhou, mji ulioko kusini mwa China.

Viwanda na makampuni 314 kutoka nchi na sehemu 36 yatashiriki kwenye maonesho hayo, ikiwa ni pamoja na viwanda na makampuni 7 kutoka nchi 6 zilizoko nyuma kimaendeleo.

Katika jumba la bidhaa zinazoagizwa kutoka nje kwenye maonesho hayo, mfanyabiashara wa bidhaa za sanaa kutoka Tanzania Bi. Wennie Mzawa kwa mara ya kwanza alihudhuria maonesho hayo ya Guangzhou yanayojulikana barani Afrika. Hali inayomfurahisha ni kuwa, wafanyabiashara wengi kutoka nchi na sehemu mbalimbali dunianiwalimwelezea nia ya kushirikiana naye, hivyo bidhaa zake zinaweza kuuzwa katika nchi nyingi zaidi nje ya Afrika.

Katika kibanda chake cha maonesho aliweka picha za mapambo na vitambaa vya hariri zenye mtindo dhahiri wa kiafrika na vinyago vyenye maumbo mbalimbali ambazo zinavutia wafanyabiashara wengi kutazama. Bi. Mzawa ana imani kuwa kutokana na maonesho hayo, bidhaa zake za sanaa zinazotengenezwa kwa mikono zitakaribishwa sana katika soko la China.

Madhumuni ya maonesho ya mwaka huu kuongeza jumba la bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, ni kuongeza uagizaji wa bidhaa kutoka nchi za nje, kupunguza shinikizo linalosababishwa na urari mkubwa wa biashara kati ya China na nchi za nje.

Naibu mkurugenzi wa kituo cha biashara na nje cha China Bw. Xu Bing alisema ili kupanua biashara kati ya China na Afrika, China inafanya juhudi kusaidia bidhaa za Afrika ziingie kwenye soko la China. Maonesho ya mwaka huu yameweka vibanda bila malipo kwa nchi nne za Afrika zikiwemo Uganda, Zambia, na Tanzania.

Kampuni ya kusafirisha nje bidhaa za mbao ya Zambia pia ilipata kibanda bila malipo. Mkuu wa idara ya soko la kampuni hiyo Bw. Haysom alisema maonesho ya biashara ya Guangzhou yanawafanya wafanyabiashara wa sehemu mbalimbali wakutane huko Guangzhou, na kutuletea fursa nyingi za biashara.

Licha ya kuonesha bidhaa na kufanya mazungumzo ya kibiashara, lengo jingine la Bw. Haysom ni kukusanya habari na kuelewa mahitaji ya soko. Kwenye kona ya kibanda chake, kuna karatasi nyingi alizokusanya zinazohusu orodha ya bidhaa na maelezo ya kampuni nyingine.

Bw. Xu Bing alisema kuwaalika wafanyabiashara wa Afrika kushiriki kwenye maonesho hayo ni hatua moja ya kuihimiza China iagize bidhaa kutoka Afrika. China pia inafanya mikutano mbalimbali ya kuzitangaza bidhaa za Afrika, na kuongeza uagizaji wa bidhaa kutoka Afrika. Katika miaka ya hivi karibuni, uuzaji wa bidhaa wa Afrika nchini China umekuwa unaongezeka sana na pengo la biashara na China linapunguza.

Tarehe 10 mwezi Aprili, mwenyekiti wa shirikisho la biashara na China la Zambia Bw. Sebastian Keplanti, alisema Zambia itatuma watu 55 wa sekta ya viwanda ya Zambia kushiriki kwenye maonesho ya biashara ya Guangzhou. ikilinganishwa na miaka iliyopita, idadi ya watu wanaotaka kushiriki kwenye maonesho hayo kwa sasa inaongezeka, hali hii inaonesha kuwa wazambia wengi zaidi wanaanza kufuatilia maonesho hayo ya bidhaa ya China.

Bw. Sebastian alipohojiwa na waandishi wa habari wa shirika la habari la China la Xinhua alisema, ushawishi wa maonesho ya biashara ya Guangzhou duniani unaongezeka siku hadi siku, na maonesho hayo ni sehemu nzuri kwa nchi mbalimbali kuelewa bidhaa za China. Alisema ujumbe wa Zambia utafuatilia sana kilimo, vifaa vya uchimbaji madini, kompyuta, bidhaa za teknolojia ya upashanaji wa habari, mashine za ujenzi wa barabara, vifaa vya ujenzi na vifaa vya umeme vinavyotumika nyumbani.

Serikali ya Zambia inafanya juhudi kuendeleza bidhaa za kilimo nchini humo na utengenezaji zaidi wa rasilimali ya madini, na kutunga hatua kadhaa za faida kuvutia uwekezaji wa nchi za nje. Wakati huo huo, serikali ya Zambia pia inavitia moyo viwanda vya Zambia kuingiza teknolojia na vifaa vya kisasa. Bw. Sebastian alisema vifaa vya China vyenye sifa nzuri na bei nafuu vinafaa sana kutumika nchini Zambia, na vinakaribishwa na viwanda nchini Zambia.

Habari zinasema, nchi za Afrika zimekuwa sehemu muhimu kwenye maonesho ya bidhaa nchini China.

Katika maonesho ya 100 ya bidhaa za Guangzhou yaliyofanyika mwaka jana, idadi ya wafanyabiashara wa Afrika waliohudhuria maonesho hayo na thamani ya biashara iliongezeka ikilinganishwa na mwaka 2005. Wafanyabiashara 9375 wa Afrika walihudhuria maonesho hayo, idadi hiyo imeongezeka kwa watu 715ikilinganishwa na mwaka jana wakati kama huu.

Thamani ya biashara ya nchi za Afrika kwenye maonesho hayo ilifikia dola za kimarekani bilioni 1.66, ambayo ilichukua asilimia 5 ya thamani ya jumla ya maonesho hayo.

Kwenye mkutano wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwezi Febuari mwaka 2003, serikali ya China ilitangaza kusamehe ushuru wa forodha wa bidhaa kutoka nchi 25 ambazo ziko nyuma kabisa kimaendeleo za Afrika. Na mwaka 2006 katika mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, serikali ya China iliongeza aina za bidhaa hizo kuwa 422.

Thamani ya biashara kati ya China na Afrika inaongezeka siku hadi siku, mwaka 2006 thamani ya bidhaa za China zilizouzwa barani Afrika ilifikia dola za kimarekani bilioni 26.7, na thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka Afrika imefikia dola za kimarekani bilioni 28.8, China ilikuwa na pengo la biashara wa dola za kimarekani bilioni 2.1.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-20