Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-23 15:29:03    
Kujiburudisha kwa vitoweo vya mboga mjini Beijing

cri

Chakula cha mboga kikiwa ni moja ya mitindo ya maisha ya afya, kinazidi kupendwa na watu wengi. Katika kipindi hiki cha leo tutawafahamisha kuhusu migahawa miwili maalumu ya chakula cha mboga iliyopo hapa Beijing. Mgahawa unaoitwa "Putiyuan" ni mgahawa maarufu na wenye umaalumu wa kipekee kati ya migahawa ya vyakula vya mboga mjini Beijing. Mgahawa huo uko kwenye hekalu Sanshengan, ambalo ni moja ya mahekalu ya kale kwenye sehemu ya kusini mwa Beijing. Hapo awali hekalu hilo lilikuwa linaendeshwa na watawa wanawake, hivi sasa hekalu hilo limekuwa ni mahali pa utalii wa kiutamaduni penye chakula na maonesho ya utamaduni wa dini ya kibudha. Hekalu hilo lililojengwa kwa matofali ya rangi ya kijivu na kuezekwa kwa vigae vya rangi ya kijani, maboriti na nguzo zake vimechorwa michoro yenye rangi mbalimbali, hekalu hilo lina nyua tatu za mbele, kati na nyuma. Kwenye ua wa mbele kuna ukumbi wa chakula cha mboga na nyumba ya chai, ukumbi wa kuonesha utamaduni wa kibudha uko kwenye ua wa kati na nyumba zilizojengwa kwenye ua wa nyuma ni za watawa wa sehemu za nje waliotembelea huko. Mgahawa wa Putiyuan na nyumba ya chai zimepambwa vizuri sana, ambapo kuna michoro mikubwa maarufu ya Dunhuang kwenye kuta zake na sanamu za budhaa ndani yake. Bibi Zhang Qing anayemiliki mgahawa wa Putiyuan ni mwumini wa dini ya kibudha, alisema hekalu lile lilikuwa ni la kifalme, tena alisimulia hadithi moja:

"Inasemekana kuwa katika enzi ya Ming, mfalme alikuwa na dada mzuri sana. Siku moja dada wa mfalme alimwona kijana mmoja aliyetoka mbali, akampenda sana, lakini mfalme alitaka dada yake aolewe na mtu mwingine aliyemtaka. Kijana yule alipoondoka huko alipanda mti mmoja kwa ajili ya dada wa mfalme, akitarajia kuwa kama watajaliwa wataweza kuonana tena chini ya mti huo. Dada wa mfalme alihuzunika sana, na aliacha maisha ya kawaida akawa mtawa wa dini ya kibudha."

Mti ule ukiwa kama ushahidi wa mapenzi, umekua kwa zaidi ya miaka 400, na bado umestawi sana katika hekalu la Sanshengan. Wachumba wengi waliokwenda kula huko huomba wabarikiwe wakiwa chini, hivyo mti ule pia unajulikana kuwa ni "mti wa ndoa". Chakula cha mboga maarufu zaidi cha mgahawa wa Putiyuan, ni chakula kinachochemshwa ndani ya jiko la mkaa, ambacho inasemekana kuwa, dada yule wa mfalme alikipenda sana. Chakula kinachochemshwa katika jiko la mkaa ni uyoga, tende nyekundu na mboga, na maji yanayotumika kuchemsha chakula, yalitengenezwa kwa nyanya, chakula hicho ni kitamu na chenye nguvu ya kujenga mwili na kufanya sura inawiri.

"Samaki aliyepikwa kwa sukari na siki" ni kitoweo kingine maarufu cha mgahawa wa Putiyuan. Mboga muhimu katika kitoweo hicho, ni aina ya tikiti linalojulikana kwa wax gourd. Mpishi analikata tikiti hilo kuwa na umbo la samaki na kulipika liwe na ladha ya samaki, kiasi ambacho walaji hudhani ni samaki wa kweli; "Vipande vidogo vya nyama ya kuku vilivyopikwa pamoja na karanga na vichipukizi vya mianzi" ni kitoweo kingine kinachopendwa na watu, "nyama ya kuku" iliyoko katika kitoweo hicho ilitengenezwa kwa maharage, lakini ladha yake ni tamu zaidi kuliko nyama ya kweli ya kuku.

Mbali na chakula cha mboga kilichopikwa na ufundi wa jadi, mgahawa wa Putiyuan una vitoweo vingine vya mboga vilivyopikwa kwa mtindo wa kitibet na vingine vilivyobuniwa na mgahawa huo, ambavyo kimoja kati yake kinaitwa "Piga ramli" msimamizi wa mgahawa huo Bw. Fan Li alisema, umaalumu wa kitoweo hicho ni kuhusu mambo yaliyoko katika ramli hizo.

"Baadhi ya uyoga na mboga zilizotumika katika kitoweo hicho zimetungwa kwenye vijiti vyembamba vyenye maneno ya baraka yakiwemo kujaliwa kupata mali nyingi, kupata utajiri mkubwa na kupandishwa cheo kwa mfululizo. Kitu kinachofurahisha zaidi ni kuwa, kati ya vijiti hivyo zaidi ya kumi, kuna kijiti kimoja kilichoandikwa maneno ya 'umepata bahati ya kulipa malipo ya fedha ya chakula'.

Wateja wanaokwenda kula mara kwa mara kwenye mgahawa wa Putiyuan licha ya kuwa ni watawa, pia kuna waumini wa dini ya kibudha pamoja na watu wanaopenda chakula cha mboga. Kwa mfano mtawa Hua ni mtawa wa hakelu moja lililoko mjini Beijing, ambaye anafika huko mara kwa mara kula chakula cha mboga.

"Ni jambo la kawaida kwa sisi watawa kula chakula katika mahekalu, ni kama kula chakula katika nyumba yetu wenyewe. Mazingira ya mgahawa wa Putiyuan, siyo tu kuwa yanatupatia sisi watawa mahali pa kula chakula, bali pia yanatoa nafasi ya kula chakula cha mboga kwa watu mbalimbali wa jamii, chakula cha mgahawa huo ni maalumu sana."

Ikiwa mgahawa wa Putiyuan ni mgahawa wa chakula cha mboga cha jadi, basi sasa tunawafahamisha mgahawa mwingine wa kisasa wa chakula cha mboga. Chakula cha mboga cha kisasa ni chakula kinachounganisha umaalumu wa chakula cha mboga cha Ulaya na Marekani na umaalumu wa chakula cha mboga cha jadi cha China. Mmoja ya migahawa hiyo ni mgahawa unaoitwa Hetangyuse, maana ya jina hilo la kichina la mgahawa huo ni kando ya bwawa lenye miyungiyungi chini ya mbalamwezi. Mgahawa huo uko kwenye enel la Chaoyang lililoko kwenye sehemu ya mashariki mwa Beijing, ambao una matawi mengi mjini Beijing. Ni tofauti na mgahawa wa chakula cha mboga cha jadi, vitoweo vya mgahawa wa Hetangyuse ni kudumisha hali yake ya kimaumbile wala siyo kuiga chakula cha nyama kutoka maumbo yake hadi ladha yake. Bw. Wang Zhong ni mpishi mkuu wa mgahawa huo, alisema,

"Walaji hawawezi kuona chakula kinachotengenezwa kuwa na maumbo ya chakula cha nyama katika vitoweo vya mgahawa huo, na wala hawaoni majina ya samaki na nyama. Vitu vinavyotumika kupika chakula ni matunda na mboga za kawaida na kuonesha ladha yake halisi, wala siyo kuiga ladha ya chakula cha nyama."

Bw. Wang alisema, kati ya vyakula vya mgahawa wa Hetangyuese, licha ya kuweko vyakula vya mboga vya Hambuger, Pizza na tambi za Italia vyenye radhi inayopendwa na wageni na umaalumu wa chakula cha mboga cha kichina. Kitoweo kimoja cha mgahawa huo cha kuunganisha umaalumu wa kichina na nchi za magharibi ni kitoweo kinachojulikana kwa "Mwangaza wa jua wa Picasso", upikaji wake ni kuchanganya samli na siagi katika boga lililochemshwa na kusagwa, kisha vinatiwa kwenye maji ya maharage na kutengenezwa kuwa na umbo la tufe, na kukaangwa ndani ya mafuta hadi kuwa na rangi ya dhahabu.

Supu inayopikwa na mgahawa wa Hetangyuese pia ni tamu sana na inayopendwa na watu wengi. Supu hiyo inapikwa kwa aina ya uyoga adimu. Meneja wa mgahawa huo Bibi Xia Zehong alisema,

"Uyoga unaotumika kupika supu hiyo ni aina ya uyoga mzuri adimu, mpishi anaweka supu hiyo katika birika la chai, walaji wanapokunywa supu wanamimina supu katika vikombe kama kunywa chai."

Kuna ujia mmoja uliofunikwa kwa vioo kwenye mgahawa wa Hetangyuse, wateja wanaokwenda huko kula chakula hupenda kukaa mle ndani. Nje ya ujia huo imepandwa miti mingi ya Japanese pagoda tree, ambayo inachanua maua mengi katika majira ya Spring; watu wanaweza kuona mwezi na nyota wakati wa usiku mle ndani. Ndani ya mgahawa ule kuna chumba cha kuwekea vitabu vya kale, ambavyo vingi vinahusu dini ya kibudha, wateja wanaweza kuvisoma.

Wasikilizaji wapendwa, watu wanaopenda chakula cha mboga walitokea miaka mingi iliyopita. Watu wa kale waliamini kuwa, chakula cha mboga kinafanya watu kuwa na maadili na tabia nzuri, na kinarefusha maisha ya watu. Hapo baadaye, kutokana na kuathiriwa na dini ya kibudha, chakula cha mboga kilianza kupendwa na watu wengi. Baada ya kuendelezwa kwa miaka mingi, mapishi ya chakula cha mboga yamefikia kiwango cha juu. Endapo unapata nafasi ya kuitembelea China, usisahau kwenda kujiburudisha kwa chakula cha mboga.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-23